Na Mwandishi Wetu, BATA
MSHAMBULIAJI Wilfried Bony alikuwa kila kitu Jumapili wakati Ivory Coast inaifunga Algeria mabao 3-1 katika Robo Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika.
Sasa Ivory Coast itapambana na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Jumatano katika Nusu Fainali ya kwanza.
Ivory Coast wanashiriki mashindano yao makubwa kwa mara ya kwanza bila ya mshambuliaji wake, aliyekuwa tegemeo la mabao Didier Drogba tangu Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka 2002.
Bony akifurahia na Drogba (kulia) kabla ya mkongwe huyo kustaafu soka ya kimataifa |
Baada ya kung'ara Swansea, Wilfried Bony amesajiliwa Manchester City
Kulikuwa kuna dalili mapema tangu tu makundi ya AFCON yanatajwa na wao wakiwa wamepangwa na Guinea na Mali, kwamba watamkosa mshambuliaji wa Chelsea, ambaye alistaafu soka ya kimataifa baada ya Fainali za Kombe la Dunia katikati ya mwaka jana.
“Kama Drogba hayupo si kwa sababu yetu, lakini kwa sababu zake,”alisema kocha Herve Renard kuwaambia Waandishi wa Habari. “Pamoja na hayo, ikiwa unamkosa Drogba na unampata Bony, unakuwa vizuri sana,”.
Dhidi ya Algeria, Bony alifanya kazi nzuri ya kuanza kuwasahaulisha watu wa Ivory Coast kuhusu Drogba.
Mchezaji huyo mpya wa Manchester City, alifunga mabao mawili, akimalizia krosi ya Max Gradel na mpira wa adhabu wa Yaya Toure kuipeleka Ivory Coast Nusu Fainali.
“Bony alikuwa mfungaji bora England mwaka 2014,” amesema Renard. “Na unaposema hivyo, unaelewa kila kitu. Mambo ni rahisi mno unapokuwa na wachezaji wa ubora wake na Gervinho,”.
Gervinho, ambaye alifunga bao la tatu dakika za lala salama kwa Ivory Coast, pia alisema kwamba Bony yuko katika kiwango ambacho kinasababisha timu imsahau Drogba.
“Hatuwezi kufikiria kuhusu Drogba tena,”amesema. “Bony ni mchezaji wa aina tofauti, ni mchezaji ambaye anatupa vitu vipya. Ana haiba ambayo inafanya kazi vizuri Ivory Coast, anajituma kwetu na anaendana nasi,”.
Ivory Coast inaingia Nusu Fainali ya nne kati ya sita zilizopita za Kombe la Mataifa ya Afrika na itacheza na DRC mjini Bata kesho. DRC ilifika hatua hii baada ya kuwafunga jirani zao, Kongo Brazzaville mabao 4-2 Jumamosi.
0 comments:
Post a Comment