// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); IJUE AFRICAN SPORTS, TIMU YA KIHISTORIA ILIYOREJEA LIGI KUU BAADA YA MIAKA 23 - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE IJUE AFRICAN SPORTS, TIMU YA KIHISTORIA ILIYOREJEA LIGI KUU BAADA YA MIAKA 23 - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Saturday, February 07, 2015

    IJUE AFRICAN SPORTS, TIMU YA KIHISTORIA ILIYOREJEA LIGI KUU BAADA YA MIAKA 23

    Na Mahmoud Zubeiry, TANGA
    MWAKA 1988, mataji yote makubwa ya soka Tanzania yalikwenda Tanga, Coastal Union wakichukua ubingwa wa Bara, na African Sports wakabeba ubingwa wa Muungano.
    Ubingwa wa Muungano ndiyo lilikuwa taji kubwa zaidi nchini wakati huo, michuano iliyoshirikisha timu za Bara na visiwini kumpata bingwa wa jumla wa nchi na pia wawakilishi wa michuano ya Afrika.  
    Bingwa wa Bara alikuwa anakwenda kucheza Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati pekee, lakini bingwa wa Muungano alikuwa anacheza Klabu Bingwa Afrika.
    Mshindi wa pili wa Ligi ya Muungano, alikuwa anacheza iliyokuwa michuano ya Kombe la Washindi Afrika, baadaye ikaongezeka na mshindi wa tatu akawa anacheza Kombe la CAF.
    Wachezaji wa African Sports wakiwa mazoezini Uwanja wa sekondari ya Usagara, Tanga


    Lakini sasa Kombe la CAF limeunganishwa na Kombe la Washindi na kuwa Kombe la Shirikisho wakati Klabu Bingwa Afrika imekuwa Ligi ya Mabingwa.
    Na Ligi ya Muungano hakuna tena kwa sababu, Zanzibar sasa ni mwanachama wa CAF, hivyo timu zake zinakwenda moja kwa moja kushiriki michuano ya Afrika.
    Pamoja na mambo kubadilika, lakini historia itabaki pale pale- kwamba African Sports walikuwa mabingwa wa nchi mwaka 1988.  
    African sports ilianzishwa mwaka 1936 na masnai yake ni Barabara ya 12, Tanga, waasisi wake wakiwa marehemu Mohammed Msuo, Mwajitu, na Athumani Makalo pekee aliye hai kati ya waanzilishi.
    Baadhi ya wachezaji walioipa jina Sports mwanzoni ni kama makipa Mohammed Yahya, Omar Mahadhi, mabeki Mweri Simba, Omar Zimbwe, Salim Kajembe, Muhaji Mwabuda na kiungo Amran Shiba.
    Mabingwa wa Muungano 1988, mwaka ambao Coatsal walikuwa mabingwa wa Bara walifungwa 2-0 ugenini Klabu Bingwa, mechi ya marudiano haikufanyika kwa sababu FAT ilikuwa ina madeni CAF, wapinzani wakafuzu ‘bwerere’.
    Sports ilichukua ubingwa wan nchi chini ya kocha Syllersaid Mziray ‘Super Coach’ (sasa marehemu), aliyekuwa akisaidiwa na Muhaji Mwabuda.
    Kikosi cha African Sports miaka ya 1970
    Wachezaji wa African Sports wakiwa mazoezini wiki hii

    Kikosi cha ubingwa kilikuwa kinaundwa na; Salim Waziri, Bakari Tutu, Francis Mandoza, Hassan Banda, Mhando Mdevi, Raphael John, Abbas Mchemba, Twaha Omar, Victor Mkanwa, Mchunga Bakari na Juma Burhan.
    Wachezaji wa akiba walikuwa Duncan Mwamba, Martin Mahimbo ‘Water Green’, Abdul Ahmed ‘Bosnia’, Hamza Maneno, Dadi Fares na wengineo. 
    Mahimbo alitungwa jina Water Green na Twaha Omar kwa sababu alichukua dawa ya kuchua misuli (Water Green) akaweka kwenye mswaki akidhani dawa ya meno.  
    Africans Sports ilishuka daraja mwaka 1991 na tangu hapo imekuwa ikisota kurejea Ligi Kuu bila mafanikio.
    Kwa wakati tofauti walimu mbalimbali wenye uwezo mkubwa nchini kama Charles Boniface Mkwasa, Freddy Felix Minziro na wengine wamewahi kupewa jukumu la kuirudisha Ligi Kuu Sports bila mafanikio.
    Lakini waliofanikisha ndoto za timu hiyo kurejea Ligi Kuu ni mabeki wa zamani, Joseph Lazaro aliyewika Coastal Union na Yanga SC miaka ya 1990 na Kassim Mwabuda aliyechezea Mtibwa Sugar enzi zake.
    Benchi la udundi la Sports linakamilishwa na kocha wa makipa, Abdul Mguto chini ya Meneja, Abdul Ahmed Mohammed ‘Bosnia’.
    Makocha wa African Sports, Joseph Lazaro kushoto na Kassim Mwabuda kulia
    Kocha wa makipa wa African Sports, Abdul Mgude kulia akiwapa maeleekzo makipa wake, Ally Salim, Zakaria Majaliwa (katikati) na Tokala nzau kushoto

    Kikosi chao kilichoirejesha Sports Ligi Kuu kinaundwa na Yussuf Abdul, Halfan Twenye, Mussa Ajiran, Juma Shemvuni, Mwaita Ngereza, Sultan Juma, Ramadhani Hamidu, Ally Ramadhani na Ally Shiboli.
    Wengine ni James Mendi, Nyanda Kaziyoba, Tokala Nzau, Ayub Masoud, Ally Issa, Mussa Chambe, Ally Ahmed, Fadhili Kizenga, Evarstus Munjwahuki, Maulid Abbas, Nzara Ndaro, Rashid Ally, Hussein Issa, Zakaria Majaliwa, Issa Yassin, Paul Muna, Mohamed Rashid na Kassim Juma.
    Sports imepandishwa na wachezaji wengi wazuri, vijana wadogo, lakini kipaji cha kumulikwa haswa ni beki wa kati, Juma Shemvuni.
    Hadi kufanikiwa kutimiza ndoto za kurejea Ligi Kuu, Sports ilipata misaada ya wadau mbalimbali, lakini zaidi kampuni ya Bin Slum Tyres Limited.
    “Kwa kweli tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa Mohammed Bin Slum, amekuwa na msaada mkubwa sana kwetu katika harakati za kupanda,”anasema Bosnia.
    Lakini Bosnia pia anawashukuru Meya Mstaafu, Mneki Kisauji, Mohammed Ratco, Yanga Omary, Nuru Smart na Mwenyekiti wa klabu yao wa sasa, Hassan Kessy kwa misaada yao mikubwa ambayo miaka 23 baadaye inairejesha Sports Ligi Kuu.
    Bosnia anasema Sports itaendelea kutamba na ngoma ya Kimanumanu kwani hiyo ndiyo asili ya timu na popote ambako timu hiyo itakwenda kucheza, kigoma hicho kitakuwepo.
    Hata hivyo, Sports wameonyesha kusikitishwa mno na kitendo cha ‘kutoswa’ na ndugu zao, Yanga SC  wakati wanasotea kurejea Ligi Kuu kwa miaka yote 23 na mbaya zaidi, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yussuf Manji aliwakana.
    Bosnia amesema kwamba Yanga SC wanatakiwa kufahamu kwamba udugu si kufanana, bali ni kufaana; “Katika kuhangaika kwetu ili turejee Ligi Kuu, sisi tulikwenda kuomba msaada Yanga SC, hawakutusaidia. Tena tuliandika barua hadi kwa Manji, jibu tulilopewa, eti Manji haitambui African Sports,”amesema Bosnia.
    Meneja huyo amesema kwamba waliumia sana kukanwa na ndugu zao hao wa asili na damu, lakini wakaamua kupambana kwa namna nyingine hadi wamefanikiwa kurejea Ligi Kuu kwa msaada wa watu wengine.
    “Coastal Union ni wapinzani wetu wa jadi hapa Tanga, lakini angalau wao walitusaidia katika vita yetu ya kupanda na tangu hapo tukaunda umoja wa “Tanga kwanza”. Kwa hiyo sasa hivi, timu za Tanga ni kitu kimoja kwa manufaa ya mkoa wa Tanga,”amesema.
    Pamoja na hayo, Bosnia amesema udugu wa kihistoria baina yao na Yanga SC hauwezi kufa, isipokuwa hauna thamani tena baada ya kaka zao hao kuanza kutouthamini.
    “Utabaki udugu wa kufanana kwa bendera na jezi, Wasitarajie msaada wowote kutoka kwetu, baada ya wao wenyewe kuanza kutukana. Hatumaanishi tumeua udugu, huo upo, lakini hauna thamani tena,”amesema.
    Sports imejihakikishia kurejea Ligi Kuu baada ya kufikisha pointi 44 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine ya Kundi A, ikiwa imebakiza mechi mbili dhidi ya Kurugenzi na Friends Rangers.  
    Karibu tena Ligi Kuu African Sports ‘Wana Kimanumanu’, mabingwa wa Jamhuri 1988, wenye historia ya kuibua vipaji vilivyogeuka lulu ya taifa tangu marehemu Mwalimu Julius Nyerere Rais wa nchi, ilipotoa nyota kama Omar Mahadhi na Omar Zimbwe.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: IJUE AFRICAN SPORTS, TIMU YA KIHISTORIA ILIYOREJEA LIGI KUU BAADA YA MIAKA 23 Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top