NAHODHA wa kikosi cha Italia kilichobeba Kombe la Dunia mwaka 2006 nchini Ujerumani, Fabio Cannavaro amehukumiwa kifungo cha miezi 10 jela kwa kukiuka amri ya kutofika katika nyumba yake iliyozuiliwa na Mamlaka.
Cannavaro mwenye umri wa miaka 41, amekuwa akichunguzwa kwa tuhuma za kukwepa kodi na Oktoba Mamlaka mjini Naples ilizuia mali za karibu Pauni 732,737 zinazohusishwa na mchezaji huyo wa zamani wa Real Madrid na Juventus pamoja na mkewe.
Kaka wa Cannavaro, Paolo mwenye umri wa miaka 33, ambaye anachezea timu ya Ligi Kuu Italia, Sassuolo, naye amehukumiwa kifungo cha miezi sita na mkewe Daniela Arenoso mwenye umri wa miaka 40 miezi minne.
Watatu hao wamekata rufaa na kifungo chao kimesitishwa hadi mwisho wa rufaa yao.
Cannavaro amehukumiwa miezi 10 jela, ingawa kifungo chake kimesitishwa kupisha rufaa yake
Ndugu hao akina Cannavaro na Arenoso waliponzwa na kwenda kutembelea nyumba hiyo wakati ipo kizuizini.
Cannavaro alishinda tuzo ya Mwanasoka Bora wa Dunia, Ballon d'Or mwaka 2006 baada ya kuiongoza Italia kutwaa Kombe la Dunia. Akahamia Real Madrid baada ya hapo, ambako alikwenda kutwaa mataji mawili ya La Liga na vigogo hao wa Hispania.
Beki wa klabu ya Yanga SC ya Tanzania, Nadir Haroub Ali, amepewa jina la utani Cannavaro kutokana na Mtaliano huyo aliyeichezea mechi 136 Azzuri.
0 comments:
Post a Comment