// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); BENDI ZETU ‘ZIMEZALIWA MAPACHA’ NYIMBO ZAO NAZO ‘ZINAZALIWA MAPACHA’ - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE BENDI ZETU ‘ZIMEZALIWA MAPACHA’ NYIMBO ZAO NAZO ‘ZINAZALIWA MAPACHA’ - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Monday, February 02, 2015

    BENDI ZETU ‘ZIMEZALIWA MAPACHA’ NYIMBO ZAO NAZO ‘ZINAZALIWA MAPACHA’

    ZAMANI ulikuwa hupati shida ya kuzitofautisha bendi zetu, sekunde ya kwanza tu wimbo unapoanza utajua wazi kuwa unasikiliza wimbo wa bendi gan. Si taarab, si muziki wa dansi lakini siku hizi thubutu yake, utakoma na roho yako.
    Enzi hizo ukisikiliza taarab ya Bima Modern Taarab, JKT, Melody, Babloom, All Stars, Muungano, TOT na nyinginezo hupati shida kuzipambanua nyimbo zao hata uzikutie katikati – upigaji wa kila bendi ulijitofautisha na nyingine, tena kipindi hicho hakuna hata kurusha majina ya wapiga vyombo lakini bado utajua huu ni wimbo wa kundi fulani.
    Lakini siku hizi mmmhhh! Karibu vikundi vyote vya hii kitu inaitwa modern taarab vinafanana – vikundi viwili vitatu viko juu kisha vikundi vilivyo chini vinaamua kusafiria nyota za wenzao, vinaanza kuiga kila kinachofanywa na wenzao, nyimbo zinafanana, tabia hii inazidi kukomaa siku hadi siku, wasanii wanaambukizana ‘ujinga’ wa kukosa ubunifu.
    Usiposikia sauti ya mwimbaji (mwenye uimbaji wa kipekee) wala huwezi kujua ni wimbo wa kundi gani na ukijidai kusikiliza majina ya wapiga vyombo ili ujue ni bendi gani ndo utapotea kabisa.

    Kwenye taarab kuna wasanii fulani wasiozidi kumi ambao wameshikilia soko la taarab hususan kwa upande wa studio – hawa utawasikia karibu katika kila bendi, utawasikia hata katika nyimbo binafsi za waimbaji wanaoamua kutoka kivyao vyao, mbaya zaidi ni kwamba ndugu zetu hao hawana juhudi za kujibadilisha kutoka wimbo mmoja hadi mwingine, kazi za mikono yao ni zile zile hazibadiliki.
    Tuachane na taarab, twende kwa ndugu zetu wa dansi. Huku ndo kuna maajabu zaidi mpaka unajiuliza ni kitu gani kinaendelea katika dunia hii ya muziki huu tunaoamini kuwa ndio muziki pendwa zaidi hapa nchini kuanzia enzi na enzi.
    Tafuta wimbo wa “Chatu” wa Safari Sound (Wana wa Ndekule), kuna solo fulani la Kassim Rashid linaanzisha wimbo – solo lile hutalisikia tena popote pale, halafu katikati ya wimbo utakutana na saxaphone ya King Maluu ambayo nayo hutaisikia kwenye wimbo mwingine wowote ule. Chukua nyimbo za MK Group “Ngoma za Magorofani” sikiliza namna ala zinavyopangiliwa katika namna ambayo hutaifananisha na bendi nyingine. Joseph Mulenga wa Sikinde, OSS, Bima Lee na wa MK Group ni watu wanne tofauti. Kassim Mponda wa Msondo, Sikinde na Bima Lee ni watu watatu tofauti – huu ndio ubunifu unaokesekana leo hii.
    Nimetoa mifano michache sana kuonyesha ni namna gani wanamuziki wa zamani walikuwa wabunifu lakini siku hizi wasanii wetu wametawaliwa na uvivu, ujuaji, ubishi na papara. 
    Wanamuziki wetu wa sasa wanashindwa kutofautisha nyimbo moja hadi nyingine, wimbo unavyoanza huwezi kujua ni wimbo gani, ukiukuta katikati pia huwezi kujua ni wimbo gani …Ok hilo unaweza ukalivumilia lakini mbaya zaidi ni kwamba tabia hiyo inakomaa na sasa wanashindwa hata kutofautisha bendi na bendi.
    Ukienda Akudo Impact, FM Academia, Mashujaa Band, Extra Bongo, Twanga Pepeta na nyingine nyingi, mfumo ni ule ule, muziki ule ule, sebene zile zile, rap zile zile, hakuna tena utambulisho (identity) wa bendi moja hadi nyingine. Msanii mmoja au wawili wakitoka bendi fulani kwenda bendi nyingine basi ujue anakwenda kuambikiza ladha ile ile aliyotoka nayo kwenye bendi yake ya zamani – kubadilika kwao ni mwiko.
    OSS iliwahi kuchukua wanamuziki ‘vichwa’ saba kwa mpigo kutoka Sikinde lakini bado muziki wa OSS na Sikinde haukufanana, Komandoo Hamza Kalala, Eddy Shegy na Adam Bakari waliondoka Vijana Jazz wakiwa tegemeo wakaenda kufufua Washirika Stars lakini bado muziki wa Vijana Jazz na Washirika haukufanana, mifano kama hii ipo mingi sana ambapo ndani yake utakutana na bendi kama Tuncut Almas, Ngorongoro Heroes na Sambulumaa ambazo nazo hazikufanana licha ya asilimia kubwa ya wanamuziki mastaa waliounda bendi hizo kuwa ni wale wale.
    Hali hii imeletwa na bendi zinazojiita bendi za dansi la kizazi kipya, ukiwatazama Msondo, Sikinde na Njenje wako na muziki wao ule ule - haujapoteza utambulisho licha ya baadhi yao kuingiza damu mpya nyingi katika bendi zao lakini bado uongozi unakikisha utamaduni wa bendi unalindwa.
    Miaka michache iliyopita ilikuwa rahisi kuzitofautisha Diamond Sound, FM Academia, Twanga Pepeta, TOT na Chuchu Sound lakini hali ikaanza kubadilika taratibu kadri bendi hizi zilivyogeuzwa kuwa mtambo wa kuzalisha bendi mpya ndivyo balaa lilipokuwa linaibuka. 
    Kuna haja ya kuwepo kwa juhudi za makusudi za kujikwamua kwenye mtego huu, vinginevyo tutaendelea kulaumu media bure lakini kumbe mengine tunajitakia wenyewe, hebu tujifunze basi hata kwa wadogo zetu wa bongo fleva wanaounyofoa muziki wa dansi taratibu na kuuhamishia kwao – sikiliza “Mwana Dar es Salaam” ya Ali Kiba kuna ka-rumba katamu ambako hukuwahi kukasikia hapo kabla kwenye nyimbo zake, sikiliza nyimbo za Yamoto Band zikianza tu unajua hiyo Yamoto Band.
    Bendi zinafanana, nyimbo zinafanana, tungo zinafanana, show zinafanana – ni hali hiyo inayonifanya nianze kuamini kuwa hizi bendi zetu hizi zimezaliwa mapacha na sasa nazo zinazaa nyimbo mapacha. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: BENDI ZETU ‘ZIMEZALIWA MAPACHA’ NYIMBO ZAO NAZO ‘ZINAZALIWA MAPACHA’ Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top