Na Vincent Malouda, NAIROBI
ALIYEKUWA nahodha wa Coastal Union ya Tanzania bara na mkenya Jerry Santo ni miongoni mwa wachezaji kumi na sita waliozinduliwa na mabingwa wa Kenya, Gor Mahia.
Gor imo mbioni kujiandaa kombe la klabu bingwa barani Afrika na sasa imewasajili wachezaji kumi na sita kujaza nafasi za wachezaji walioondoka miongoni mwao Dan Sserunkuma aliyehamia Simba SC, Geoffrey ‘Baba’ Kizito kwenda Vietnam na David ‘Calabar’ Owino aliyejiunga na ZESCO United ya Zambia.
Sasa Gor Mahia ina jumla ya wachezaji 28 na wanayo nafasi mbili kufanya sajili nyingine.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zasema kuwa wana mikakati ya kumnasa straika la mahasimu wao wa jadi AFC Leopards Jacob Keli na vile vile nahodha wa Muhoroni Youth Abbas Akinyemi.
Misimu miwili iliyopita, Santo aling'ara na Coastal Union ya Tanga katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara, hiyo ni klabu ya pili kuchezea nchini humo baada ya awali kuwa Simba SC ya Dar es Salaam.
Kabla ya kurejea Kenya, Santo alijaribu kurejea Simba SC, lakini hakufanikiwa kutokana na kugoma kufanya majaribio kama alivyotakiwa na kocha wa Wekundu hao wakati huo, Mcroatia Zdravko Logarusic. Santo pia alikwenda Oman kujaribu kujiunga na Fanja ya huko bila mafanikio na hatimaye sasa amerudi nyumbani kujipanga upya.
0 comments:
Post a Comment