// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); YANGA SC WATAFUTE NAMNA NYINGINE YA KUENDESHA KLABU YAO, KUMTEGEMEA MANJI NI KUJIPA MATUMAINI HEWA - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE YANGA SC WATAFUTE NAMNA NYINGINE YA KUENDESHA KLABU YAO, KUMTEGEMEA MANJI NI KUJIPA MATUMAINI HEWA - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Wednesday, November 19, 2014

    YANGA SC WATAFUTE NAMNA NYINGINE YA KUENDESHA KLABU YAO, KUMTEGEMEA MANJI NI KUJIPA MATUMAINI HEWA

    MEZI mitano imepita tangu, wanachama 1, 560 wa Yanga SC wamuongezee muda wa mwaka mmoja madarakani, Mwenyekiti wao, Yussuf Manji.
    Jumapili ya Juni 1 mwaka huu, (2014), Mkutano Mkuu wa marekebisho ya baadhi ya vipengele vya Katiba ya Yanga uliofanyika kwenye Bwalo la Maofisa wa Jeshi la Polisi, Oysterbay, Dar es Salaam uliwaongezea mwaka mmoja Mwenyekiti Manji na Makamu wake Clement Sanga.
    Kwa wasomaji wazuri wa safu yangu hii, watakumbuka niliwahi kuandika  ni miujiza kusikia Yanga SC wana fedha hata Milioni 1 benki, lakini haishangazi kusikia klabu ina deni la mamilioni mengi, tena kwa mamia.
    Hiyo ni kwa sababu kiuchumi, Yanga SC inategemea watu na sana mtu mmoja, Manji na zaidi ya hapo ni ufadhili wa Kampuni ya Bia Tanzania (TBL)- ambao wenyewe viongozi wa klabu hiyo wamekwishasema mara kadhaa hautoshelezi bajeti ya klabu hiyo.

    Kwa sababu hiyo unaweza kuona ni kiasi gani Manji ni mtu muhimu sana ndani ya Yanga SC, ambaye hata akosee hakuna anayeweza kupingana naye akaeleweka.
    Ndiyo maana, mwishoni mwa msimu alisema hatagombea tena uongozi, lakini baadaye akarudi kwa kishindo akisema anafuta kauli yake ya kutogombea na kuahidi mambo mengi.
    Alisema mpango wa ujenzi wa Uwanja wa kisasa upo pale pale, atasajili wachezaji wapya bora na kumleta kocha Mbrazil, Marcio Maximo. Maximo amekuja na anaendelea na kazi Yanga SC, wachezaji wa Kibrazil, Genilson Santana Santos ‘Jaja’ na Andrey Coutinho wapo klabuni.
    Akafanikiwa kuwashawishi wanachama wamuongezee mwaka mmoja zaidi madarakani- na baada ya Maximo kutua na akina Jaja ndani ya miezi mitano ya mwaka mmoja, Manji ana deni la kutimiza ahadi ya ujenzi wa Uwanja wa Kaunda.
    Nilisema, kwa ujio wa Maximo tu na akina Jaja, Manji anaweza kuwafanya wana Yanga wasahau kuhusu ujenzi wa Uwanja wa kisasa.
    Hiyo ni kwa sababu, wana Yanga walio wengi wanaridhika sana wakiiona timu yao inatamba katika Ligi ya nyumbani na kupamba kurasa za magazeti.
    Fikra endelevu- yaani kuiona taswira ya klabu hiyo inabadilika na kuwa yenye hadhi, yenye kujimudu kiuchumi hayo si mambo ambayo wana Yanga wengi wanayafikiria sana.
    Kufungwa na Simba SC, wanavumilia lakini hawapendi, ila hata kama wakifungwa, lakini wakawa mabingwa wa Bara inatosha.
    Thamani ya klabu ni rasilimali zake na inavyoweza kuzitumia kujinufaisha kiuchumi- Yanga SC achilia mbali kuwa na mamilioni ya wapenzi na maelfu ya wanachama, ina majengo zaidi ya mawili.
    Wenye kuifahamu historia ya klabu, wanasema Yanga SC mbali na jengo la makao makuu pale Jangwani, wana jengo Mtaa wa Mafia na Tandale. Pia, Yanga SC ina nyumba ya NHC pale eneo la Fire, ambayo wamewahi kuishi kocha Mromania, Victor Stanslescu, marehemu Tambwe Leya na Charles Boniface Mkwasa. 
    Haijulikani nyumba ya NHC kama walipanga au waliuziwa katika maghorofa ya Fire, lakini hadi mwanzoni mwa muongo uliopita ilikuwa bado kwenye himaya ya klabu hiyo.
    Ajabu Yanga SC haipati fedha hata senti moja kutokana na majengo yake yote hayo, angalau jengo la makao makuu wameweka ofisi na wakati mwingine huwa kambi ya wachezaji.
    Kuweza angalau kulitumia jengo la makao makuu kwa ofisi na kambi ni baada ya Manji kulifanyia ukarabati mwaka 2007, lakini kwa zaidi ya miaka 10 kabla ya hapo, lilikuwa halitumiki kwa uchakavu. Lilikuwa kama boma.
    Yanga SC kama klabu, haina uwezo wa kujiendesha bila fedha za Manji kwa sasa na kwa hali halisi huwezi kuona atatokea mfadhili gani mwingine siku za karibuni katika klabu hiyo.
    Na Manji analijua hilo, ndiyo maana hababaishwi na mwana Yanga yeyote, akiamua anatangaza kumfuta uanachama yeyote anayetaka kupingana naye.    
    Mikwara ikizidi anatingisha kiberiti hagombei tena, akijua fika wana Yanga wataingiwa na ‘ubaridi’ wakiufikiria mustakabali wa klabu bila yeye.
    Na wana Yanga wanaamua kuwa wapole kwake, kwa sababu wanakumbuka msoto ambao klabu ilipitia tangu kutoweka kwa wimbi la wafadhili wengine wa Kiasia waliomtangulia Manji, akina Abbas Gulamali, Mohammed Viran ‘Babu’ (wote sasa marehemu), Murtaza Dewji na wengineo. 
    Yanga SC ilifikia kuwa timu inayocheza uwanjani, huku jukwaani watu wanatembeza bakuli kukusanya michango angalau wachezaji wapewe posho, kabla ya Manji kuibuka mwaka 2006 kuokoa jahazi na kubadili taswira nzima ya klabu kiasi fulani. 
    Bahati mbaya ambayo Yanga inaipata siku zote, ni kukosa viongozi wabunifu ambao wanaweza kutengeneza mipango ya kuifanya ijitegemee.
    Mara kadhaa tunatoa mifano ya jezi tu za Yanga SC, timu hiyo inapocheza mashabiki hufanana na wachezaji wao uwanjani kwa mavazi, lakini klabu hainufaiki hata kwa senti moja.
    Yanga SC inapoteza si chini ya Sh. Milioni 500 kila mwaka kutokana na mauzo ya jezi pekee- bado ingeweza kupata fedha zaidi kama ingeuza bidhaa nyingine zenye nembo yake kwa mashabiki wake.
    Yanga SC bado ingeweza kuingia ushirika na makampuni kadhaa ya utengenezaji na uuzaji bidhaa kuyaruhusu yatumie nembo ya klabu kwenye bidhaa hizo kwa kulipana.
    Lakini yote haya yanahitaji viongozi wabunifu, ambao watajitolea kwa dhati kuamua kuisaidia klabu. 
    Na bahati mbaya sana Manji ambaye wakati anaingia madarakani watu walijenga imani kubwa juu yake, naye ameshindwa kubadilisha hali ndani ya klabu kama kiongozi mkuu.
    Amekuwa mtu wa kutatua shida za kila siku tu ndani ya klabu ili iendelee kucheza Ligi Kuu yetu, lakini utekelezaji haswa wa dhamira ya kuifanya Yanga SC iwe klabu fulani yenye hadhi inayoendana na ukubwa wake, hauonekani.
    Amekuwa mtu anayetumia machafuko ya hali ndani ya klabu kutoa ahadi nyingi tamu za kuwatuliza ‘jazba’ wanachama, lakini mwisho wa siku hakuna lolote.
    Na kwa staili hii, ipo haja sana Yanga SC watafute njia mbadala za kuiletea maendeleo yenye kuonekana klabu yao, kulio kuendelea kumtegemea Manji. Alamsiki. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC WATAFUTE NAMNA NYINGINE YA KUENDESHA KLABU YAO, KUMTEGEMEA MANJI NI KUJIPA MATUMAINI HEWA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top