Sure Boy (kulia) atakabidhiwa tuzo yake Mchezaji Bora wa Oktoba kesho Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam
Na Princess Asia, DAR ES SALAAM
MCHEZAJI bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara mwezi uliopita, Oktoba, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ wa Azam atakabidhiwa tuzo yake kesho.
Mtoto huyo wa kiungo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Abubakar Salum ‘Sure Boy’ atakabidhiwa tuzo hiyo kabla ya mchezo wa Ligi Kuu, baina ya timu yake, Azam FC dhidi ya Coastal Union Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Wadhamini wa Ligi Kuu, kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom watampa kiungo huyo wa Taifa Stars Sh. Milioni 1 na tuzo maalum.
Sure Boy ni mchezaji bora wa pili wa mwezi tangu kuanza kwa msimu huu wa Ligi Kuu, baada ya Anthony Matogolo wa Mbeya City kushinda tuzo ya Septemba.
Ligi Kuu inaendelea wikiendi hii na mbali na Azam FC kuwa wenyeji wa Coastal, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Yanga SC wataikaribisha Mgambo JKT pia ya Tanga.
0 comments:
Post a Comment