SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeelezea masikitiko makubwa kufuatia kifo cha kipa na Nahodha wa timu ya taifa ya Afrika Kusini, Bafana Bafana.
Senzo Meyiwa aliyekuwa na umri wa miaka 27, ambaye pia alikuwa Nahodha wa Orlando Pirates alipigwa risasi na majambazi siku moja baada ya kuiongoza timu yake kwenye ushindi wa 4-1 dhidi ya Ajax Cape Town kwenye robo fainali ya kombe la Ligi.
Mchumba wa marehemu Senzo Meyiwa, Kelly Khumalo akiwasili nyumbani kwao, eneo la Vosloorus kufuatia kifo cha mwenzi wake huyo aliyekuwa kipa wa Orlando Pirates na Bafana Bafana kwa kupigwa risasi jana.
Katika salamu zake kwa Chama cha Soka Afrika Kusini (SAFA), TFF imesema kifo cha ghafla cha Nahodha huyo wa Bafana Bafana ni pigo kubwa kwa familia yake, klabu yake ya Orlando Pirates, familia ya mpira wa miguu na taifa zima la Afrika Kusini.
“Shirikisho la Soka Tanzania na familia ya mpira kwa ujumla iko nanyi katika kipindi hiki cha maombolezo,”imesema sehemu ya salamu hizo iliyotiwa saini na Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Joas Selestine.
Nakala ya salamu hizo imetumwa kwa Mwenyekiti wa Ligi Kuu ya Afrika Kusini (PSL) na Mwenyekiti wa klabu ya Orlando Pirates.
Senzo Meyiwa (kulia, akiidakia Afrika Kusini)
0 comments:
Post a Comment