KIUNGO Wesley Sneijder ametaja sababu ya kukataa ofa ya kujiunga na Manchester United msimu huu ni kwa sababu alitaka kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kiungo huyo wa Galatasaray alikuwa sehemu ya kikosi cha Uholanzi kilichokuwa chini ya kocha Louis van Gaal katika Kombe la Dunia na amesema Mholanzi mwenzake huyo ni miongoni mwa makocha bora duniani.
Lakini mkongwe huyo mwenye umri wa miaka 30 aliyehusishwa kwa kiasi kikubwa na kuhamia Old Trafford amesema anafurahia maisha Uturuki.
"Louis (Van Gaal) ni mmoja wa makocha bora wenye uelewa mkubwa wa soka - na nilijua nia ya Manchester United wakati wa usajili. Walinihitaji, lakini nina furaha sana hapa Uturuki - na ni vigumu sana kuacha Ligi ya Mabingwa,"amesema.
Galatasaray inamenyana na Arsenal leo katika Ligi ya Mabingwa Ulaya na Sneijder amesema wataingia na mipango ya kuishambulia timu ya Arsene Wenger Uwanja wa Emirates.
"Arsenal inacheza soka fulani nzuri, hususan katika safu ya kiungo- hivyo ni muhimu tukafanya kila tutakachoweza kuwazuia kucheza mchezo wao. Hatujaribu tu kuuzuia mchezo wao - tunaweza kucheza soka nzuri upande wetu na tunataka kuwashambulia Arsenal - tunaamini tunaweza kushinda,"amesema.
0 comments:
Post a Comment