Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
KOCHA Mzambia, Patrick Phiri amepewa mechi mbili zijazo, dhidi ya Mtibwa Sugar Jumamosi hii na Ruvu Shooting wiki ijayo, kuhakikisha anainasua Simba SC kwenye dimbwi la sare, vinginevyo atavunjiwa mkataba wake.
Akizungumza katika Mkutano na Waandishi wa Habari leo, makao makuu ya klabu Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Simba SC, Stephen Ally amesema Phiri anaweza kuondolewa baada ya mechi hizo mbili iwapo matokeo hayatakuwa mazuri.
Ally amesema kwamba sababu ya Kamati ya Utendaji kufikia maamuzi hayo ni kwamba, wakati anaajiriwa Agosti mwaka huu, Phiri alipewa kila alichokihitaji ili kujenga timu.
Kocha Patrick Phiri amepewa mechi mbili Simba SC afanye vizuri, vinginevyo anatimuliwa |
Phiri alifanya vizuri katika mechi za kirafiki, lakini baada ya kuanza kwa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzaia Bara ametoa sare mechi zote tano na Jumamosi wiki hii atakuwa Uwanja wa Jamhuri dhidi ya vinara, Mtibwa Sugar.
Aidha, Katibu huyo amesema kwamba wachezaji watatu waliosimamishwa, viungo Shaaban Kisiga ‘Malone’, Amri Kiemba ‘Jeshi la Jiwe’ na Haroun Chanongo watakutana na Kamati ya Nidhamu keshokutwa kujibu tuhuma zao.
Watatu hao, walisimamishwa baada ya mechi dhidi ya Prisons Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, Simba SC ikitoa sare ya 1-1 na wenyeji wao hao, waliosawazisha dakika mbili za mwisho.
Kiemba na Chanongo wanatuhumiwa kucheza chini ya kiwango, wakati Kisiga anadaiwa kuwatolea majibu ya kifedhuli viongozi kabla ya mechi na Prisons.
Katika hatua nyingine, Ally amesema Kamati ya Utendaji imepiga marufuku mtu yeyote kuzungumza habari za klabu, isipokuwa Rais, Evans Aveva, Makamu wake, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ na Katibu huyo.
Zaidi ya hapo, Wajumbe wa Kamati ya Utendaji na viongozi wa Kamati, watazungumza kwa ruhusa maalum ya uongozi.
Ally pia amesema kwamba Mkutano Mkuu wa wanachama uliopangwa kufanyika Desemba, sasa utakuja mapema zaidi kulingana na hali iliyopo.
Kwa ujumla tangu arejee Simba SC Agosti mwaka huu kurithi mikoba ya Mcroatia, Zdravko Logarusic Phiri ameiongoza timu hiyo katika mechi 14, kati ya hizo akishinda nne, zote za kirafiki, kufungwa tatu na kutoa sare saba, tano za Ligi Kuu.
Mechi ya kwanza, Simba SC chini ya Phiri ilishinda 2-1 dhidi ya Kilimani City, baadaye 2-0 dhidi ya Mafunzo na 5-0 dhidi ya KMKM zote za kirarfiki visiwani Zanziabr.
Baadaye Simba SC iliichapa 3-0 Gor Mahia ya Kenya katika mchezo mwingine wa kirafiki, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kufungwa 1-0 na URA mchezo wa kirafiki pia Dar es Salaam.
Tangu kipigo hicho cha URA, Simba haijashinda mechi yoyote nyingine, kwani zilizofuata ilitoa sare ya 0-0 Ndanda kirafiki Mtwara, 2-2 na Coastal Union, 1-1 na Polisi Moro, 1-1 na Stand United zote za Ligi Kuu Uwanja wa Taifa.
Baada ya hapo, Simba SC ikaenda Afrika Kusini kwa kambi ya kujiandaa na mechi dhidi ya watani, Yanga SC ambako katika mechi tatu ilizocheza, ilitoka 0-0 na Orlando Pirates kabla ya kufungwa 4-2 na Bidvest Wits na baadaye 2-0 na Jomo Cosmos.
Iliporejea kutoka Afrika Kusini imecheza mechi mbili zaidi za Ligi Kuu na zote kutoka sare tena, 0-0 na watani wao, Yanga SC Uwanja wa Taifa na 1-1 Prisons.
Sasa hatima ya Phiri itaamuliwa na mechi mbili zijazo za Ligi Kuu kwa mujibu wa uongozi wa Simba SC- maana yake Mzambia huyo yuko chini ya shinikizo.
REKODI YA PHIRI SIMBA SC...
0 comments:
Post a Comment