Na Mahmoud Zubeiry, DAR ES SALAAM
KOCHA Mbrazil, Marcio Maximo keshokutwa ataiongoza Yanga SC katika mchezo wa nne wa kujipima nguvu tangu ajiunge nayo akirithi mikoba ya Mholanzi, Hans van der Pluijm Julai.
Yanga SC itacheza na Thika United ya Kenya Jumatano Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo huo maalum kujiandaa na msimu mpya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, unaoanza Septemba 20, mwaka huu.
Lakini Yanga SC itaanza na mchezo wa Ngao ya Jamii, dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu, Azam FC Septemba 13, Uwanja wa Taifa.
Kikosi cha Yanga SC kilichoshinda mechi zote za kujipima nguvu Zanzibar |
Kocha Maximo akiwa na Wasaidizi wake katika moja ya mechi za Zanzibar |
Katika mechi tatu za awali ambazo Maximo ameiongoza Yanga SC, imeshinda zote visiwani Zanzibar, 1-0 dhidi ya Chipukizi Uwanja wa Gombani, Pemba na 2-0 mara mbili dhidi ya Shangani na KMKM Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Wachezaji wapya kutoka Brazil, walirejea Dar es Salaam na kumbukumbu nzuri ya kuifungia mabao timu yao hiyo mpya kwenye michezo hiyo, mshambuliaji Geilson Santana ‘Jaja’ akifunga bao pekee katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Chipukizi, wakati kiungo Andrey Coutinho akifunga bao moja kile mechi katika 2-0 za Shangani na KMKM.
Ligi Kuu inatarajiwa kuanza Septemba 20, mwaka huu, mabingwa watetezi Azam FC wakianza na Polisi Morogoro Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Septemba 20, mwaka huu, wakati Yanga SC waliomaliza nafasi ya pili wataanza na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro siku hiyo.
Washindi wa tatu, Mbeya City wataanza na JKT Ruvu ya Pwani, Uwanja wa Sokoine, Mbeya Septemba 20 na washindi wa nne, Simba SC wataanza na Coastal Union ya Tanga Septemba 21, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi nyingine za ufunguzi za Ligi Kuu zitakuwa kati ya Stand United watakaoikaribisha Ndanda ya Mtwara Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Mgambo JKT wataikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
0 comments:
Post a Comment