Mtibwa Sugar wameshinda mechi ya pili mfululizo leo Ligi Kuu na sasa wanafukuzana na Azam FC kileleni
MTIBWA Sugar imepata ushindi wa pili mfululizo Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara jioni ya leo, baada ya kuichapa Ndanda FC ya Mtwara mabao 3-1 Uwanja wa Manungu Turiani, Morogoro.
Ushindi huo unawafanya mabingwa hao wa zamani wa Ligi Kuu, watimize pointi sita baada ya mechi mbili, lakini wanakaa nafasi ya pili nyuma ya Azam FC yenye wastani mzuri zaidi wa mabao.
Mabao ya Mtibwa inayofundishwa na Mecky Mexime leo yamefungwa na Ame Ally dakika ya 36 na Ally Shomary mawili dakika ya 42 na 47, wakati bao pekee la Ndanda iliyoanza ligi kwa ushindi wa 4-1 dhidi ya Stand United mjini Shinyanga, leo limefungwa na Iddi Kulachi dakika ya 54.
Katika mechi nyingine, Mbeya City ambayo kama Ndanda na Stand, zinadhaminiwa na kampuni ya Bin Slum Limited, imeshinda 1-0 dhidi ya Coastal Union ya Tanga Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya, bao pekee la Deogratius Julius dakika ya 40 kwa penalti.
Mgambo JKT imefungwa nyumbani bao 1-0 na Stand United ya Shinyanga, bao pekee la Mussa Said dakika ya 13.
Azam FC imeshinda 2-0 dhidi ya Ruvu Shooting ya Pwani Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam, mabao yote akitupia Mrundi Didier Kavumbangu, ambaye sasa anafikisha mabao manne, baada ya awali kufunga mawili pia katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Polisi Morogoro.
Simba SC imelazimishwa sare ya 1-1 na Polisi Morogoro Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam bao lao likifungwa na Mganda, Emmanuel Okwi na la Maafande likifungwa na Danny Mrwanda.
0 comments:
Post a Comment