KIUNGO Franck Ribery amestaafu soka ya kimataifa akiwa na umri wa miaka 31 tu.
Nyota huyo wa Ufaransa alikosa Fainali za mwaka huu za Kombe la Dunia kutakana na majeruhi aliyoyapata mazoezini siku chache kabla ya kuanza kwa michuano ya mwaka huu Brazil.
Na kwa kukosekana kwake, Les Bleus ilitolewa katika Robo Fainali baada ya kufungwa bao 1-0 na Ujerumani walioibuka mabingwa.
Uamuzi huo wa Ribery unampa fursa zaidi ya kuelekeza nguvu zake katika klabu yake, Bayern Munich.
"Nang'atuka," amesema Ribery akihojiwa na jarida la soka Ujerumani, Kicker. "Nimeona wakati umefika,".
"Nataka kuelekeza nguvu zangu kwa familia yangu na kazini kwangu Bayern Munich na kutoa nafasi kwa damu changa katika timu ya taifa.
Mkali huyo anatungika daluga zake timu ya taifa ya Ufaransa baada ya kuifungia mabao 16 katika mechi 81 tangu alipocheza kwa mara ya kwanza mwaka 2006 dhidi ya Mexico.
Licha ya kukosa Kombe la Dunia nchini Brazil, lakini alitoa mchango kwa Ufaransa wakati wa mechi za kuwania kufuzu kwenye fainali hizo akikifungia mabao matano kikosi cha Didier Deschamps.
Ribery ni mshindi mara tatu wa tuzo ya Mwanasoka Bora Ufaransa na alishika nafasi ya tatu katika tuzo za Mwanasoka Bora wa Dunia, maarufu kama Ballon D'Or mwaka 2013, nyuma ya Cristiano Ronaldo aliyeshinda na Lionel Messi aliyekuwa wa pili.
0 comments:
Post a Comment