NIGERIA imetanguliza mguu mmoja hatua ya 16 Bora ya Kombe la Dunia kufuatia ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Bosnia jana mjini Cuiaba katika mchezo wa Kundi F.
Shukrani kwake mshambuliaji wa Stoke City, Peter Odemwingie aliyefunga bao hilo pekee la ushindi dakika ya 29 dhidi ya timu ya mchezaji mwenzake wa kjlabu hiyo ya England, Asmir Begovic, akimalizia kazi nzuri ya Emmanuel Emenike.
Timu hiyo ya Edin Dzeko inaaga Kombe la Dunia baada ya kufungwa mechi mbili mfulullizo, baada ya awali kufungwa 2-1 na Argentina katika mchezo wa kwanza, ingawa itacheza mechi ya kukamilisha ratiba dhidi ya Iran.
Cheupe dawa; Mshambuliaji Peter Odemwingie akikimbia kushangilia baada ya kuifungia Nigeria bao muhimu usiku wa kuamkia leo |
Nigeria sasa inatimiza pointi nne na kukaa nafasi ya pili nyuma ya Argentina ambayo tayari imefuzu kwa pointi zake sita. Nigeria itaomba sasa Bosnia ijikaze na kuibana japo kwa sare Iran, ili hata kama Super Eagles itafanyiwa roho mbaya na Argentina iweze kufuzu 16 Bora.
Iran ina pointi moja na kama ikiifunga Bosnia itafikisha pointi nne maana yake kama Nigeria itafungwa na Argentina timu ya pili ya kufuzu kwenda 16 Bora kutoka kundi hilo, itaamuliwa kwa wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa. Kikosi cha Nigeria kilikuwa: Enyeama, Oshaniwa, Yobo, Omeruo, Ambrose, Onazi, Mikel, Babatunde/Uzoenyi dk75, Musa/Ambeobi dk66, Odemwingie na Emenike.
Bosnia-Herzegovina: Begovic, Mundza, Sunjic, Spahic, Lulic 6/Salihovic dk58, Besic, Misimovic, Medunjanin/Susic dk64, Hajrovic/Ibisevic dk57, Pjanic na Dzeko.
Mshambuliaji wa Nigeria, Peter Odemwingie (kushoto) akimfunga kipa wa Bosnia Asmir Begovic
0 comments:
Post a Comment