Na Frank Sanga, Dar es Salaam |
Mashabiki wanapenda soka la England kwa sababu huwezi kutabiri matokeo. Ni ngumu sana kujua nani atashinda katika mechi ijayo.
Uzuri wa ligi hiyo ni kuwa Chelsea wanaweza kufungwa na Crystal Palace au Aston Villa na bado maisha yatakwenda tu.
Manchester United wanaweza kufungwa na West Bromwich au Cardiff na bado maisha yatakwenda na hakuna atakayelalamika. Hayo ndiyo maisha ya soka ya kila siku katika soka la Ulaya.
Waamuzi wa soka Ulaya kwa asilimia kubwa wanafanya makosa ya kibinadamu uwanjani. Kama tulivyoona hivi karibuni mwamuzi alimpa kadi nyekundu mchezaji asiye sahihi. Ni makosa ya kibinadamu, lakini yanayoumiza mashabiki. Lakini maisha lazima yasonge mbele.
Licha ya makosa hayo ya kibinadamu ya waamuzi, bado wamekuwa wakijitahidi sana kuchezesha mpira kwa uwezo wao na kufuata sheria 17 za soka.
Jambo jingine ambalo limefanya mashabiki wengi Tanzania kufuatilia soka la Ulaya na hasa England ni kutokana na kurushwa moja kwa moja na televisheni.
Ingawa kwa Tanzania baadhi ya klabu zinaona ni kesi ya jinai mechi zao kurushwa laivu na televisheni, kwa wenzetu maonyesho hayo ya runinga yamefanya ligi yao iwe na msisimko wa hali ya juu duniani kote.
Ingawa ligi ya Tanzania ipo katika hatua ya chini sana, lakini kwa mbali nimeanza kuona dalili kuwa miaka michache ijayo ligi inaweza kuwa na mvuto.
Unaposikia Yanga na Simba zimeanza kupoteza mechi na likaonekana ni jambo la kawaida, ujue soka letu sasa linaelekea kule kunakostahili.
Unapoona timu yenye wachezaji wa thamani ya Sh500 milioni wanapoteza mchezo dhidi ya kikosi chenye thamani ya Sh 10 milioni, ujue tumefika mahali pazuri.
Kama Simba na Yanga zinaweza kuwa zinaingia uwanjani zikawa hazina uhakika wa kupata ushindi ujue soka letu limeanza kubadilika na miaka michache ijayo tutakuwa mahali pazuri.
Ukiona waamuzi wa soka hawaogopi tena kuwapa penalti Mgambo dhidi ya Yanga, ujue kuna dalili njema ya soka letu na hakika tumechelewa sana.
Ukiona mwamuzi anawanyima penalti Simba licha ya Ramadhani Singano kufanyiwa faulo ndani ya eneo la hatari ujue kuwa waamuzi sasa wanajiamini na hicho ndicho kinachotakiwa. Mwamuzi anapaswa kuwa na uhakika kwa uamuzi wake kwa asilimia mia moja.
Ukiona huko vijijini watu wanakusanyika katika vibanda kuangalia Azam TV inapoonyesha mechi laivu za Ligi Kuu Bara ujue tunakokwenda ni pazuri.
Kama mashabiki wanalipa kiingilio cha Sh 500 kwenye vibanda kuangalia mechi za Ligi Kuu Bara kwenye Azam TV, basi ujue kuwa tumefika mahali pazuri na miaka michache ijayo ligi yetu itabadilika sana.
Ukiona imefika mahali viongozi wa Yanga wamekaa kimya kuhusu Azam TV, ujue wameona umuhimu wake na ndio maana licha ya kuapa kwa majina yote, kituo hicho cha televisheni kimekuwa kikionyesha mechi za Yanga bila tatizo.
Ukiona mashabiki wa Yanga na Simba wanakubali kuwa kuna timu nyingine inaweza kuwa bingwa tofauti na wao, ujue kuwa tumefika mahali pazuri ila kitu ambacho kinaniuma ni kwamba tumechelewa sana kufika hatua hiyo.
Hakuna anayepaswa kulaumiwa kwa lolote kwa sasa, lakini ninaona dalili njema za ligi yetu kuwa na msisimko Afrika yote miaka michache ijayo. Kwa vyovyote itakavyokuwa ni jambo la muhimu kuona kuwa kuna mwanga fulani unakuja mbele. Tusubiri tu.
(Frank Sanga ni Mhariri Mtendaji wa gazeti la Mwananchi na makala hii imetoka kwenye safu yake ya gazeti la Mwanaspoti leo)
0 comments:
Post a Comment