// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); MZIGO TUMEUTUA SALAMA, LAKINI… - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE MZIGO TUMEUTUA SALAMA, LAKINI… - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Sunday, April 20, 2014

    MZIGO TUMEUTUA SALAMA, LAKINI…

    MSIMU wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara umehitimishwa jana kwa Azam FC kutawazwa kubwa mabingwa wapya baada ya kumaliza na pointi 62 dhidi ya 56 za waliokuwa mabingwa watetezi, Yanga SC baada ya mechi zote 26.
    Azam ilijihakikishia ubingwa wa Ligi Kuu Jumapili iliyopita, baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-1 Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya na kufikisha pointi 59 ikiwa na mchezo mmoja mkononi ambazo zisingeweza kufikiwa na timu yoyote baada ya mechi za mwisho jana. 
    Licha ya kuwa timu ya kwanza kuifunga Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine Aprili 13, mwaka huu, Azam FC pia inakuwa timu ya kwanza nje ya Simba na Yanga kutwaa ubingwa wa Bara tangu mwaka 2000 Mtibwa Sugar ilipofanya hivyo
    Azam inakuwa timu ya saba nje ya Simba SC kutwaa taji la Ligi Kuu, baada ya Cosmo mwaka 1967, Mseto mwaka 1975, Pan Africans mwaka 1982, Tukuyu Stars mwaka 1986, Coastal Union 1988 na Mtibwa Sugar mara mbili mfululizo 1999 na 2000.
    Ashanti United ya Ilala, Dar es Salaam inayomaliza ligi na pointi 25, inaungana na JKT Oljoro ya Arusha iliyomaliza na pointi 19 na Rhino Rangers ya Tabora pointi 16 kuipa mkono wa kwaheri Ligi Kuu msimu wa 2013/2014 na nafasi zao zinachukuliwa na Ndanda FC ya Mtwara, Polisi ya Morogoro na Stand United ya Shinyanga zilizopanda kwa ajili ya msimu ujao. 
    Mbali na Azam kumaliza kileleni na pointi 62, Yanga SC pointi 56 nafasi ya pili, Mbeya City ya Mbeya imemaliza nafasi ya tatu kwa pointi zake 49, Simba SC ya nne pointi 38, Kagera Sugar ya tano pointi 38 pia, Ruvu Shooting ya sita pointi 38, Mtibwa Sugar ya saba pointi 31, JKT Ruvu ya nane pointi 31 Coastal Union ya tisa pointi 29, Prisons ya 10 pointi  28 na JKT Mgambo ya 11 pointi 26.
    Wakati tunamaliza Ligi Kuu pamoja na kufurahia kufika salama, lakini ukweli ni kwamba kuna mapungufu mengi yaliyojitokeza ndani ya msimu huu ambayo yangeweza hata kusababisha athari kubwa.
    Miongoni mwa hayo ni suala la uchezeshaji wa marefa, mfumo na muundo mzima wa ligi yetu ikiwa ni pamoja na kanuni kutozingatiwa, au kuwa na kanuni ambazo hazikidhi vigezo vya kimataifa.
    Kanuni ya tano ya Ligi Kuu inasema; “(1) Uwanja wa nyumbani ni ule uliochaguliwa na timu husika na Uwanja wa ugenini ni ule ambao timu pinzani imekaribishwa kucheza. (2) Kutokana sababu za kiusalama au Uwanja, kutofikika au sababu nyingine yeyote ya msingi, TFF kwa kushauriana na timu husika, edapo timu yoyote haina Uwanja wa nyumbani unaofaa kwa mashindano ya Ligi, timu husika inaweza kuchagua kwa idhini ya TFF, Uwanja mwingine wowote, hata nje ya mji huo au Mkoa ili mradi Uwanja huo uwe jirani na mkoa wa timu husika ndani ya Tanzania Bara na uwe na sifa zinazokubalika,”.
    Kuna tatizo katika kanuni hii, ukipitia kanuni nyingine nyingi duniani, zinaweka wazi kwamba timu itakuwa na Uwanja mmoja tu wa nyumbani, lakini kanuni hii ya ligi yetu imefumbwa na matokeo yake timu kama Ruvu Shooting, Mtibwa Sugar Azam FC na Prisons msimu huu zimetumia Uwanja zaidi ya mmoja wa nyumbani.
    Ruvu, Mtibwa na Azam zimeruhusiwa kutumia viwanja vyao kwa mechi zote za Ligi Kuu isipokuwa zile zinazohusu Simba na Yanga, kwa sababu timu zote za Kariakoo, Dar es Salaam zina mashabiki wengi.   
    Uwanja wa Liberty uliopo eneo la Swansea unaotumiwa na Swansea City wenye kuingiza watu 20,750, Uwanja wa Selhurst Park uliopo eneo la South Norwood, Jijini London unaotumiwa na Crystal Palace una uwezo wa kuingia mashabiki 26,255, Uwanja wa KC Stadium uliopo eneo naHull City uliopo eneo la Kingston Upon una uwezo wa kuchukua mashabiki 25,400, lakini timu zote msimu huo zimechezea mechi zao zote Ligi Kuu ya England kwenye viwanja hivyo zikiwemo za dhidi ya timu zenye mashabiki wengi ulimwengu mzima kama Liverpool, Manchester United na Arsenal.
    Manchester United wakiwa kwenye Uwanja wao, Old Trafford hucheza mbele ya mashabiki 75,731, Arsenal ikiwa Uwanja wa Emirates hucheza mbele ya mashabiki 60,338, Manchester City wakiwa kwenye Uwanja wa Etihad Campus hucheza mbele ya mashabiki 47,405 na Liverpool ikiwa Uwanja wake wa Anfield hucheza mbele ya mashabiki 45,276- lakini vimelazimika kufuata kanuni kwa kucheza mechi zake za ugenini katika viwanja vya mashabiki wachache kama Liberty.
    Huwezi kuona sababu ya msingi ya kukiuka kanuni za kimataifa katika ligi yetu zaidi ya kufikiria mapato zaidi kupitia Simba na Yanga- bila kujali kwamba tunazinyima haki zao timu nyingine kwa kutozipa fursa ya kucheza nyumbani mechi zote, au kuzionea baadhi ya timu zinazochezeshwa ligi kwa mujibu wa kanuni zinazotambulika dunia nzima, nyumbani na ugenini.
    Azam Complex ni Uwanja wa nyumbani wa Azam FC, lakini msimu huu umetumiwa pia kama wa nyumbani wa Ashanti United na JKT Ruvu, kwa sababu timu hizo hazina Uwanja na zikicheza Taifa, ni hasara kwa sababu hazina mashabiki.
    Uwanja wa Taifa ni mali ya Serikali na kila unapotumika kwa mechi za Ligi Kuu kuna malipo yanatakiwa sasa timu zenye mashabiki wenye uwezo wa kulipa gharama hizo ndizo zimeruhusiwa kuutumia.
    Kimsingi Uwanja wa Taifa ni kwa ajili ya Simba na Yanga- si mbaya hata Italia, AC Milan na Inter Milan zinatumia Uwanja mmoja, San Siro, nazo zinakwenda kucheza ugenini bila kujali ukubwa au udogo wa Uwanja, lakini huku Tanzania fedha mbele.
    Lakini wakati mwingine unaweza kudhani kuna timu zinatengenezewa mazingira ya kufanya vizuri, mfano mechi ya mwisho kati ya Prisons na Ashanti United kwa nini ilipelekwa Morogoro?
    TFF ilitaka mechi zote za kufunga msimu, zianze na kumalizika muda mmoja, hivyo Prisons waliokuwa wenyeji wakaambiwa watacheza Jamhuri, Morogoro badala ya Mbeya, kwa sababu siku hiyo timu nyingine ya mkoani humo, Mbeya City ilikuwa inacheza Sokoine.  
    Kama Mbeya hakuna Uwanja mwingine unaokidhi sifa za Ligi Kuu, kuna mikoa ya jirani na huo yenye historia ya kucheza Ligi Kuu, kama Iringa wenye Uwanja wa Samora au Majimaji wenye Uwanja wa Majimaji, kwa nini Prisons wasipelekwe karibu na kwao?
    Kucheza nyumbani ni kipaumbele ambacho lazima TFF ihakikishe inazipa haki hiyo timu zote za Ligi Kuu bila kujali suala la fedha. Kanuni imezungumzia suala la usalama, basi kuwe na idadi maalum ya tiketi kulingana na mahitaji ya Uwanja na zikiisha basi waliofanikiwa ndiyo watazame mechi. 
    Haiyumkiniki Ashanti wakacheze kwenye Uwanja mgumu wa Mlandizi, wakati Simba na Yanga zinachezea mechi zote nyumbani dhidi ya Ruvu Shooting, lazima kile kitu kinachoitwa haki kitendeke kwa timu zote.
    Ipo haja ya kanuni hii kufanyiwa marekebisho na kuanzia msimu ujao, timu zitumie viwanja vyao na hoja ya mashabiki isipewe nafasi ya kutufanya tuwe na ligi ovyo ovyo.
    TFF ifikirie namna ya kuifanya Ligi Kuu iingize mapato mengi bila kutofautiana na kanuni zinazotumika karibu dunia nzima. Alamsiki.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: MZIGO TUMEUTUA SALAMA, LAKINI… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top