// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); HERI USHAMBA WA AKINA MANGARA, DUMELEZI KULIKO UJANJA WA AKINA RAGE, MANJI… - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE HERI USHAMBA WA AKINA MANGARA, DUMELEZI KULIKO UJANJA WA AKINA RAGE, MANJI… - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Wednesday, April 09, 2014

    HERI USHAMBA WA AKINA MANGARA, DUMELEZI KULIKO UJANJA WA AKINA RAGE, MANJI…

    MARAFIKI wawili walianza kazi pamoja wakiwa vijana wadogo, mmoja alikuwa mpole na asiyependa makuu, mwenzake alikuwa mwingi wa habari na anayejiona mjanja sana.
    Yule mpole baada ya muda akamtaarifu mwenzake habari za kuoa, cha ujanja akamstaajabu sana rafiki yake kuoa katika umri wa miaka 25, badala ya kuutumia vizuri ujana wake kwa kubadili wanawake.
    Baada ya muda ikatoka fursa ya mikopo ofisini kwao na wote wakachukua, yule mshamba akapeleka fedha zake kwenye ujenzi na mjanja akanunua gari.

    Mjanja akawa anamstaajabu yule mshamba kachukua mkopo wa vimilioni, lakini bado anapanda daladala. Mshamba akafanikiwa kukamilisha nyumba yake ndani ya miezi mitatu na kuhamia, hivyo kuepukana na kulipia pango ya nyumba.
    Mjanja alipopata mshahara pamoja na kununua gari akaenda kupanga nyumba nzuri ya gharama zaidi katika maeneo maarufu kwa watu wenye maisha ya juu kidogo kutoka uswahilini alipokuwa anaishi.
    Mjanja hakujua gari linahitaji huduma na matunzo na wakati huo huo mshahara wake unakatwa karibu nusu nzima kulipia deni la mkopo.
    Wakati huo mshamba akafungua vimiradi vidogo vidogo vya kumuongezea kipato na kwa ujumla maisha yake hayakuambatana na anasa hata kidogo.
    Muda mwingi aliutumia kuwa na familia yake kupanga mikakati ya kujiinua kimaisha, huku staili ya maisha ya mjanja ni starehe na kubadili wanawake. 
    Miaka mitano baadaye mjanja alikuwa ana nyumba yake, gari mbili za biashara na moja ya matumizi yake- na zaidi alifanikiwa kupata watoto wawili na mkewe.
    Mjanja hali ikabidilika na gari likamshinda, matokeo yake alikuja kuliuza kama anatupa ili angalau akidhi shida zilizomganda. Hana gari, bado anaishi nyumba ya kupanga na umri umeenda.
    Huo ndiyo wakati ambao sasa yule mshamba anaishi maisha mazuri na familia yake kwa staili ile ile ya uadilifu. Unaweza kuona jinsi gani akili inavyoweza kumuongoza mtu kufanya maamuzi yenye manufaa katika maisha yake.
    Najaribu kutafakari, ni akili zipi viongozi wetu wa soka nchini wanazitumia katika kuongoza, za kijanja kama mjanja anayezungumziwa hapa au za kishamba?
    Wazi, viongozi wetu wana akili za ujanja ujanja katika kuongoza, ambazo daima haziwezi kuleta mabadiliko.
    Bila shaka waasisi wa klabu ya Simba akina Rahim Dumelezi na Yanga na akina Tarbu Mangara, wazee wetu hao walikuwa wana akili za kishamba, ndiyo maana hawakuona umuhimu wa kuwapeleka wachezaji katika hoteli za nyota tano, badala yake wakajenga hosteli zao wenyewe.
    Simba SC wanayo pale Msimbazi na Yanga SC ni Jangwani. Lakini sasa zaidi ya miaka 40 tangu zimejengwa, viongozi wa leo wameshindwa kuziendeleza klabu hizo kutoka hapo.
    Simba na Yanga ni timu kubwa sana, lakini kwa maneno tu, leo hii hata Ashanti United wakipata viongozi wenye fikra pevu wanaweza kuzipiku klabu hizo kongwe.
    Sasa hivi Ashanti wana uwezo wa kupata Sh. Milioni 100 kama watabaki Ligi Kuu kutokana na mikataba ya udhamini wao binafsi na ile ya wadhamini wa Ligi Kuu, ukiwemo wa haki za matangazo ya Televisheni.
    Hizo ni fedha ambazo wanaweza kununua eneo nje ya mji huko na kujenga Uwanja na hosteli nzuri kwa ajili ya kambi ya timu yao. Ndiyo, Sh. Milioni 100, Ashanti au timu yoyote inakuwa na hosteli nzuri pamoja na Uwanja.
    Lakini tu viongozi wao wa sasa bado hawajawa na fikra hizo wala dhamira.
    Tumekwishazungumzia sana haja ya mabadiliko katika klabu kongwe ambayo yanaanzia katika uongozi bora, lakini matokeo yake viongozi wameishia kuwahadaa wanachama wao rahisi kudanganyika.
    Leo viongozi wa Yanga SC chini ya Mwenyekiti wao wa sasa, Yussuf Manji waliwaahidi mambo mengi wanachama wao wakati wa kampeni, ikiwemo ujenzi wa Uwanja wa kisasa na kufungua vitegauchumi katika jengo la makao makuu ya klabu.
    Liko wapi duka la vifaa vya michezo pale Jangwani? Ziko ofisi za mabenki na kadhalika ambazo wana Yanga waliambiwa zitawekwa zote.
    Kilichobaki sasa ni hadithi za longolongo kuhusu ujenzi wa Uwanja- mara sijui hati zipo wapi, mara Mansipaa inawakwamisha, na wakati huo huo siku zinaenda hadi wanakaribia kumaliza muda wao madarakani.
    Rage pale Simba SC amekuwa na longolongo nyingi za ujenzi wa Uwanja, lakini hakuna cha maana kinachoendelea naye anaelekea kumaliza muda wake.
    Imeshindikana hata kutumia nembo za klabu zao kibiashara, matokeo yake klabu zinawategemea watu, ambao wakiondoka mara moja itarudi kwenye hali ngumu.
    Tuulizane, leo Zacharia Hans Poppe akisema yeye na Simba SC basi na hatatoa msaada wake tena au Manji akiamua hivyo kwa Yanga hali itakuwaje?
    Heri ushamba wa wazee wetu akina Mangara na Rahim Dumelezi (wote marehemu), umefanya vitu ambavyo leo vimekuwa alama ya klabu hizo kongwe, lakini huu ujanja wa viongozi wa leo, bure tu! 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: HERI USHAMBA WA AKINA MANGARA, DUMELEZI KULIKO UJANJA WA AKINA RAGE, MANJI… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top