// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); YANGA SC WAKUBALI MATOKEO NA WAJIPANGE UPYA, KUWAPA KIFUTA JASHO WACHEZAJI NI MUHIMU - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE YANGA SC WAKUBALI MATOKEO NA WAJIPANGE UPYA, KUWAPA KIFUTA JASHO WACHEZAJI NI MUHIMU - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Monday, March 10, 2014

    YANGA SC WAKUBALI MATOKEO NA WAJIPANGE UPYA, KUWAPA KIFUTA JASHO WACHEZAJI NI MUHIMU

    KLABU ya Yanga SC imeendeleza utamaduni wake wa kuaga mapema kwenye michuano ya Afrika, baada ya jana kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika kwa penalti 4-3 kufuatia sare ya jumla ya kufungana bao 1-1 na Al Ahly katika mechi mbili za Dar es Salaam Alexandria.
    Yanga SC iliyoshinda 1-0 wiki iliyopita Dar es Salaam, jana ilifungwa 1-0 baada ya dakika 90 kwenye mchezo wa marudiano Uwanja wa Border Guard mjini Alexandria. 
    Kipa Deo Munishi ‘Dida’ alipangua penalti mbili mfululizo ya nne na ya tano zilizopigwa na Saed Mowaeb na Hossan Ashour, wakati za Abdalllah Said, Gedo, Mahmoud Trezeguet na Mohamed Nagieb zilimpita, lakini Yanga SC nao wakakosa penalti mbili mfululizo ya nne na ya tano.
    Dida jana alipangua penalti mbili

    Oscar Joshua alipiga penalti nzuri ikaguswa na kipa Sherif Ekramy Ahmed na kugonga mwamba na kurudi uwanjani, wakati Said Bahanuzi akapiga nje upande wa kushoto wa lango.  
    Sherif Ekramy Ahmed alipangua penalti ya mwisho ya Yanga SC iliyopigwa na Mbuyu Twite na kuwavusha Hatua ya 16 Bora mabingwa hao wa Afrika.
    Waliofunga penalti za Yanga SC ni Nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Didier Kavumbangu na Emmanuel Okwi.
    Hadi mapumziko hakuna timu iliyofanikiwa kupata bao, Yanga SC wakicheza mchezo wa kujihami na mashambulizi ya kushitukiza.
    Mrisho Ngassa alicheza vyema katika safu ya kiungo mchezeshaji akiwapa pasi nzuri washambuliaji Emmanuel Okwi, Simon Msuva, Didier Kavumbangu na Hamisi Kiiza.
    Kiungo mkabaji Frank Domayo alishirikiana vizuri na mabeki wa kati Kevin Yondan na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wakati mabeki wa pembeni Mbuyu Twite kulia na Oscar Joshua kushoto walifanya kazi nzuri ya kuzuia na kusaidia mashambulizi.
    Kipa Deo Munishi ‘Dida’ alifanya kazi nzuri ya kulinda lango na kuwapanga mabeki wake, pia akianzisha haraka mashambulizi kila alipodaka mpira.
    Dakika ya 21 mshambuliaji hatari wa Ahly, Amr Gamal alipata pasi nzuri ndani ya 18 akapiga nje kabisa kulia mwa lango.
    Dakika ya 23 Abdallah Said alipiga shuti kali akiwa nje ya 18 likatoka nje sentimita chache kushoto mwa lango na Yanga SC iliwashitua kwa mara ya kwanza Ahly dakika ya 29 baada ya winga Simon Msuva kushindwa kuumiliki vyema mpira mrefu akiwa anatazamana na kipa ukamgonga na kutoka nje kulia mwa lango. 
    Mabeki wa Ahly waliwadhibiti washambuliaji wa Yanga dakika zote 45 za kipindi cha kwanza.
    Kipindi cha pili, Yanga SC walikianza vizuri wakiwabana Al Ahly na kudhibiti mashambulizi yao, huku wao wakiendelea kushambulia kwa kushitukiza.
    Dakika ya 55 Simon Msuva almanusra aipatie bao Yanga SC baada ya kupiga shuti akiwa ndani ya 18, lakini likatoka nje sentimita chache upande wa kushoto wa lango akiwa upande wa kulia amebanwa na mabeki wawili wa Ahly.
    Ahly wakajibu shambulizi hilo haraka na kupata mpira wa dhabu ambao ulipopigwa dakika hiyo hiyo ya 55 ukasababisha kizaazaa langoni mwa Yanga, lakini Cannavaro akaokoa.
    Yanga SC ilipata pigo dakika ya 65 baada ya nyota wake, Mrisho Ngassa kuumia na kutolewa nje nafasi yake ikizibwa na Athumani Iddi ‘Chuji’ dakika ya 66.
    Ahly ilipata bao lake dakika ya 71, mfungaji Sayed Moawad.  
    Baada ya bao, Ahly walikuwa wanashambulia mfululizo,  sifa zimuendee kipa Dida aliyeokoa michomo kadhaa na mingine kutoka nje.
    Baada ya dakika 90 kumalizika Ahly ikishinda 1-0, mchezo ulihamia kwenye mikwaju ya penalti na ndipo, safari ya Yanga ilipofikia tamati michuano ya Afrika, wakiendeleza utamaduni wao wa kutolewa mapema.
    Kikosi cha Yanga SC leo kilikuwa; Deogratius Munishi 'Dida', Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro, Kevin Yondan, Frank Domayo, Simon Msuva, Mrisho Ngassa/Athumani Iddi ‘Chuji’ dk66, Didier Kavumbagu, Hamisi Kiiza/Said Bahanuzi dk85 na Emmanuel Okwi.
    Kweli, Yanga jana imeendeleza utamaduni wake wa kuaga mapema michuano ya Afrika, lakini angalau safari hii tumeshuhudia wakishindana dhidi ya timu ngumu.
    Penalti hazina mwenyewe na mara nyingi zimekuwa zikiwaumbua hata wachezaji nyota wenye kuaminiwa, hivyo hakuna sababu ya kumlaumu yeyote kati ya nyota wa Yanga walipoteza penalti zao.
    Kikubwa ambacho Yanga SC wanatakiwa kufahamu ni kwamba, wametolewa katika Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu wa 2014, lakini huo si mwisho wa michuano hiyo, mwakani na daima itaendelea kufanyika.
    Yanga SC wakubali matokeo, wamalizane vizuri na wachezaji wao kwa kuwapa kifuta jasho baada ya kupigana kiume jana na bahati mbaya wakatolewa, na baada ya hapo waelekeze nguvu zao kwenye Ligi Kuu.
    Kuelekeza nguvu zao kwenye Ligi Kuu kwa maana ya kutafuta tena nafasi ya kucheza michuano ya Afrika mwakani, ili wajaribu kusahihisha makosa yao na itakuwa vyema wakitetea ubingwa na kurudi tena Ligi ya Mabingwa. Pole Yanga SC, sasa wajipange upya, huo ndiyo mpira, kuna kushinda, kushindwa na sare- na ili timu zisonge mbele, lazima nyingine zitolewe.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: YANGA SC WAKUBALI MATOKEO NA WAJIPANGE UPYA, KUWAPA KIFUTA JASHO WACHEZAJI NI MUHIMU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top