MAMLUKI BIN ZUBEIRY
VIEWED 1200 TIMES
Uongozi wa Young Africans unawaomba wapenzi, wanachama na wadau wa soka kuacha kusoma habari za blog ya Bin Zubeiry kutokana na kuandika taarifa zisizokuwa na ukweli huku lengo lake kubwa likiwa ni kuhakikisha timu ya Young Africans inafanya vibaya kwenye michezo yake na kuwavunja moyo viongozi wake pamoja na wachezaji.
Akiongea na mtandao rasmi wa klabu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Abdallah Binkleb amesema uongozi wao umemvumilia kwa muda mrefu juu ya habari zake za kutaka kuwavunja nguvu na kuisusa timu ili ibakie katika hali mbaya zaidi lakini kwa saaa umechoka na hatua za kisheria zinafuata.
"Kuelekea mchezo wa jumapili Waziri wa mambo ya nje anasisitiza timu ikafanye vizuri kwani inabeba bendera ya nchi, balozi anashiriki maandalizi ya kupokea timu mara itakapofika Misri lakini muandiishi huyu kazi yake imebakia kuandika uongo juu ya Yanga lengo lake ni kuondoa morali kwa wachezaji alisema" Bin Kleb
Hakuna asiyetambua kwamba Al Ahly walipokua jijini Dar es salaam alikuwa nao bega kwa bega Uwanja wa Taifa siku moja kabla ya mchezo wakati wakifanya mazoezi, wakati waandishi wenzake wakionysesha uzalendo na kuandika habari zenye mlengo wa kuisaidia timu ya Yanga kufanya vizuri.
Inafahamika kilichomuondoa Habari Cooperation na kuamua kuendesha blog ambayo halipii chochote kwa mwezi wala kwa mwaka zaidi ya kupata pesa za matangazo kutoka wadhamini wanaomdhamini kwa kulipia matangazo yao kwake na kupata idadi kubwa ya wasomaji kwa kuandika habari za Yanga.
Tunaomba aachane na habari za Yanga kwenye blog yake vinginevyo taratibu zinafanyika kuweza kuushtaki mtandao huo ambao umekosa weledi kwa kuandika taarifa za kupotosha muda wote, huku klabu ya Yanga ikiambulia kuchafuliwa na yeye kujipatia pesa kwa habari hizo.
Ni jambo la kushangaza katika dunia ya sasa ya karne ya Sayansi na Teknlojia mwandishi wa habari kuandika habari zisizokua na ukweli jambo ambalo linapelekea wapenzi, wadau na wachama kushindwa kuelewa ukweli ni upi na kuwapa kazi uongozi kujibu hoja zao.
Taarifa kwamba Uongozi ulitoa posho ya laki moja sio kweli, hiyo ni pesa iliyotolewa mfukoni na mmoja wa viongozi wa Young Africans kufuatia furaha ya ushindi mara tu baada ya kumalizika kwa mchezo, Kamati ya mashindano ilikua na zawadi nyingine ya ushindi huo ambayo wachezaji wameshakabidhiwa.
Tumewekeza kwa zaidi ya miaka miwili sasa, tumesajili wachezaji wazuri, wanapata huduma nzuri ikiwemo timu kuweka kambi nchini Uturuki mara mbili na mazingira ya michezo ya ligi kuu ikiboreshwa kwa asilimia 100, mishahara wachezaji wanapata kila mwisho wa mwezi hayo ni mabadiliko kiungozi na kuelekea kwenye mafanikio katika mchezo wa mpira wa miguu.
Suala la Ahadi/Zawadi ni nje ya mkataba kati ya wachezai na viongozi, klabu imekua na utamaduni wa kutoa Bonus kulingana na ushindi unaopatikana, au mara timu inapotoka sare hivyo ni vyema angeweza kuuliza uongozi kabla ya kuandika vitu asivyovijua.
Aliandika kuhusu uwezo wa Kocha Hans takribani kwa mwezi mzima pasipo kujua taaluma yake, Hans ni miongoni mwa makocha wachache wenye Cheti cha Ualimu wa Mpira Miguu barani Afrika CAF chenye Daraja A ambacho hutolewa kwa kocha aliyepata mafanikio tu na si kwa kusomea darasani kama ilvyo kwa madaraja mengine.
Mkataba wa SGM ulikuwa ni wa dolla 55,000 ambapo walitoa Advance ya dolla 20,000 kisha ikabakia dolla 35,000 ambazo walipaswa kuilipa Yangakabla ya kuanza kwa mchezo wenyewe, lakini SGM walitoa sababu kuwa ofisa wao aliyekua anakuja na pesa hizo amezuiliwa Cairo Airport na kuomba wapewe link waonyeshe mpira na watamalizia malipo hayo baada ya mechi, Uongozi wa Yanga ulikuwa makini na kuwakatalia kuwapa link mpaka wamalizie pesa iliyobakia kwani endapo wangepata hiyo link basi ingekuwa vigumu kumalizia malipo baada ya mchezo kumalizika.
Taarifa hizo zote na nyingine amekua akiandika bila kuwauliza viongozi wa Yanga kupata uhakika jambo linalopelekea kuamini kuwa anatumika na baadhi ya taasisi kuisakama Yanga ionekana haipo makini na kuonekana viongozi wake hawapo makini jambo ambalo sio kweli.
Tunatambua ana masilahi na upande gani, na timu gani ila kwa sasa tunaomba aachane na klabu ya Yanga aandike taarifa za upande unaotumia kuhakisha anaiharibia Yanga, akumbuke Yanga ilikuwepo na itaendelea kuwepo, wengine wanakuja na kuondoka kama upepo.
Mwisho tunaomba aachane na taarifa za Yanga aendelee kuandika habari za wafadhili wake wanaomsadia kwani hata wao habari ni nzuri, habari za Yanga ziwe nzuri au mbaya zitaendelea kuandikwa na waandishi wenye weledi na wanaoheshimu taasisi zinawapowaptia habari.
Mungu Ibariki Young Africans Mungu Ibariki Tanzania. (Taarifa hii imewekwa kwenye tovuti ya klabu ya Yanga SC)
HABARI INAYOLALAMIKIWA NA UONGOZI WA YANGA NI HII;
Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
UONGOZI wa Yanga SC umesema kwamba Sh 100,000 walizopewa kila mchezaji baada ya mechi dhidi ya Al Ahly ya Misri Jumamosi, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zilikuwa ni posho za mafuta ya gari zao, lakini usiku wa leo watapelekewa posho nzuri baada ya ushindi wa 1-0 siku hiyo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga SC, Mussa Katabaro ameiambia BIN ZUBEIRY jioni hii kwamba, anashangazwa na madai ya wachezaji hao kwamba wamepewa posho kiduchu wakati ukweli ni kwamba walipewa fedha kwa ajili ya mafuta ya gari zao.
“Sisi tuna utaratibu wetu tuliojiwekea kwa ajili ya hatua hii na wachezaji wetu watafurahi sana baada ya mechi ya marudiano iwapo wataitoa Al Ahly, siku ile tuliwapa fedha kidogo kama posho ya mafuta ya gari zao, kwa sababu walipewa mapumziko ya siku mbili kabla ua kurudi kambini,”alisema Katabaro.
Aidha, Katabaro alisema kwamba uongozi wa Yanga SC jioni ya leo utawapelekea posho nzuri wachezaji wake waliopo kambini hoteli ya Bahari Beach, wakati donge nono linawasubiri baada ya mchezo wa marudiano, wakifanikiwa kuwatoa mabingwa hao wa Afrika.
Pamoja na hayo, habari zaidi kutoka ndani ya Yanga SC, zinasema kwamba wachezaji wote wa klabu hiyo, leo wamelipwa mishahara yao ya Februari- hivyo wataondoka kesho kwenda Misri wakiwa vizuri.
Mchana wa leo, BIN ZUBEIRY iliwanukuu wachezaji wa Yanga SC wakilalamika morali yao imeshuka kuelekea mchezo wa marudiano na Al Ahly ya Misri Jumapili hii mjini Cairo kuwania kutinga Hatua ya 16 Bora Ligi ya Mabingwa Afrika kwa sababu wamepewa posho kiduchu baada ya mchezo wa kwanza Jumamosi walioshinda bao 1-0.
Wakizungumza na BIN ZUBEIRY kwa masharti ya kutotajwa majina yao, wachezaji hao walisema kwamba, mara baada ya mchezo wa Jumamosi viongozi waliwapelekea posho ya Sh. 100,000 kila mchezaji na kuahidi kurudi kuwaongezea, lakini hawajatokea hadi leo na hakuna salamu zozote.
“Hatufanyi hivi kwa nia mbaya tunataka wana Yanga wote wajue kitu ambacho viongozi wametufanyia baada ya kupigana na kufanya jambo la kihistoria Jumamosi,”alisema mmoja wa wachezaji hao.
Mchezaji mwingine akasema kwamba wanaamini kitu walichokifanya ni kikubwa na cha kihistoria ambacho kimewafurahisha wana Yanga wengi, lakini hawasiti kuweka wazi wameingiwa kinyongo kwa posho kiduchu waliyopewa.
“Afadhali fedha isingepatikana, lakini fedha imepatikana nyingi ya viingilio (sh. Milioni 448), halafu unawapa wachezaji laki laki, kweli jamani hiyo ni haki?,”alilalamika mchezaji mwingine.
Juhudi za kumpata Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Kimataifa ya Yanga SC, Seif Ahmed ‘Magari’ hazikufanikiwa na baadhi ya viongozi wengine waliopigiwa akiwemo Ofisa Habari, Baraka Kizuguto hawakupatikana walipotafutwa.
Lakini juzi, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) lilitangaza mapato ‘yaliyogunwa’ kutokana na idadi ya watu kuwa wengi na viingilio vilikuwa vikubwa.
TFF ilisema mechi hiyo ya Yanga dhidi ya Al Ahly ambao ni mabingwa wa Afrika iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliingiza Sh. 448,414,000.
Kikosi cha Yanga kinatarajiwa kuondoka kesho Dar es Salaam kwenda Cairo tayari kwa mchezo huo wa marudiano Jumapili.
(BIN ZUBEIRY ina ushahidi wa kutosha juu ya habari hizi, na baada ya taarifa hizo za Bin Kleb, tunafikiria hatua za kuchukua bila kuiathiri Yanga kama klabu, bali mtoaji wa taarifa)
0 comments:
Post a Comment