REFA Freddy Fautrel amekiri alifanya makosa kuwapa Monaco mabao yote matatu ya offside timu hiyo ikishinda 3-2 dhidi ya Olympique Lyon katika mchezo wa Ligue 1 nchini Ufaransa jana.
Fautrel na washika vibendera wake walishindwa kubaini kwamba mshambuliaji wa Monaco, Dimitar Berbatov alikuwa ameotea wakati anafunga bao moja na kutoa pasi za mabao mengine mawili kwa wageni hao.
“Nilitoa uamuzi mbovu ambao ulibadilisha taswira ya mchezo,” alinukuliwa Fautrel na gazeti la L'Equipe la leo. “Kulikuwa kuna washika vibendera wawili ambao walikuwa wanajisikia vibaya sana kwenye chumba cha kubadilishia nguo na kuichafua timu nzima ya marefa,”.
Kocha wa Lyon, Remi Garde alikataa kuwalaumu marefa, akisema; “Siwezi kuzungumzia hili, kwa sababu ninaweza kufungiwa,” alisema.
Ushindi huo, unawafanya Monaco wanaoshika nafasi ya pili wafikishe pointi 62 baada ya mechi 29, wakizidiwa nane na Paris St Germain, ambao jana waliifunga St Etienne mabao 2-0.
Lyon ni ya tano kwa pointi zake 45, wakizidiwa pointi nane na Lille wanaoshika nafasi ya tatu.
0 comments:
Post a Comment