KLABU ya Manchester United imeizawadia ushindi wa kwanza Liverpool Uwanja wa Old Trafford baada ya miaka mitano, kufuatia kuchapwa mabao 3-0 jioni hii katika mchezo wa Ligi Kuu ya England.
Kiungo Steven Gerrard amefunga mabao mawili kwa penalti dakika za 34 na 46 wakati Luis Suarez amefunga bao lake la 25 msimu huu dakika ya 84 kukamilisha ushindi mnono wa 3-0.
Gerrard alifunga penalti ya kwanza baada ya beki wa United, Rafael kuunawa mpira kwenye eneo la hatari na Nahodha huyo wa Wekundu wa Anfield akafunga tena kwa tuta lingine kufuatia Phil Jones kumchezea rafu Joe Allen kipindi cha pili.
Nahodha huyo wa England angeweza kuifungia Liverpool hat-trick ya kwanza Old Trafford tangu mwaka 1936 kama mkwaju wake wa tatu wa penalti usingegonga mwamba baada ya Nemanja Vidic kumchezea rafu Daniel Sturridge.
Vidic alitolewa nje kwa kadi nyekundu kwa rafu hiyo - hiyo ikiwa mara ya nne anatolewa kwenye mechi dhidi ya Liverpool, ingawa marudio ya picha za Televisheni yalimuonyesha Sturridge akijirusha ili kupata penalti.
Matokeo hayo yanaifanya Liverpool itimize pointi 62 baada ya mechi 29 na kupanda nafasi ya pili, ikiishusha Manchester City yenye pointi 60 za mechi 27 katika nafasi ya nne na Arsenal yenye pointi 62 za mechi 29 sasa ni ya tatu, Chelsea ikiendelea kuongoza kwa pointi zake 66 za mechi 30.
Man United sasa inazidi kupoteza kabisa matumaini ya kutetea taji, kwani inabaki na pointi zake 48 baada ya mechi 29 katika nafasi ya saba.
Huwezi amini: Luis Suarez akisherehekea baada ya kuifungia LIverpool bao la tatu Uwanja wa Old Trafford
Suarez akiwapa 'dole gumba' wachezaji wenzake baada ya kufunga, huku Wayne Rooney akiwalalamikia wachezaji wenzake wa United
Wachezaji wa Liverpool wakimpongeza Gerrard baada ya kufunga
Aibu yao wenyewe: United baada ya kuchapwa bao la tatu
0 comments:
Post a Comment