KLABU ya Inter Milan imetenga dau la Pauni Milioni 20 kumsajili Fernando Torres ambazo Chelsea wanaweza kuzihitaji ili kumtoa mshambuliaji huyo anayeshikilia rekodi ya kusajiliwa kwa bei kubwa England.
Torres amebakiza zaidi ya miaka miwili katika mkataba wake unaomfanya alipwe mshahara Pauni 150,000 kwa wiki aliosaini miaka mitatu iliyopita kutoka Liverpool kwa ada ya uhamisho ya Pauni Milioni 50 na Jose Mourinho anaweza kusajili mchezaji wa bei mbaya kuziba nafasi yake.
Nyota wa Atletico Madrid, Diego Costa, wa Monaco Radamel Falcao na wa AC Milan, Mario Balotelli ni miongoni mwa washambuliaji ambao wanawaniwa na Chelsea ambayo hata hivyo itabidi izingatie kanuni ya Umoja wa Vyama vya Soka Ulaya (UEFA) ya matumizi ya fedha kiungwana.
Mmiliki mpya wa Inter mfanyabiashara wa Indonesia, Erick Thohir amesema hatapoteza mamilioni mengi katika kuijenga upya timu, lakini amemsaidia kocha Walter Mazzarri Januari kwa kumpa Pauni Milioni 17 kumsajili Hernanes.
Wawakilishi wa klabu hiyo ya Italia walikuwa kwenye mazungumzo na Chelsea wakati wa usajili wa Januari juu ya Juan Mata na kuwapa ofa ya kuwarejeshea Fredy Guarin. Hata hawakufanikiwa baada ya Mata kuuzwa Manchester United na sasa Wataliano hao wamerudi tena kujaribu kumpata Mspanyola mwingine, Torres.
Suala la Torres linafuatia Inter kutangaza kumsajili Nahodha wa Manchester United, Nemanja Vidic kwa ajili ya msimu ujao.
Klabu hiyo ilithibitisha kumpata mchezaji huyo Jumatano na picha ya Vidic ikapostiwa kwenye ukurasa wa Twitter wa Inter sambamba na ujumbe: "Hapa ni Vidic akisaini Mkataba. Tutakuona Juni, Nemanja!'
Makubaliano yaliyofikiwa ni ya misimu mitatu ambao utamfanya Vidic astaafu vizuri kwa maana ya hadhi na maslahi akiwa na klabu nyingine kubwa Ulaya.
Matarajio: Kocha wa Inter, Walter Mazzarri tayari amempata beki wa Manchester United, Nemanja Vidic
0 comments:
Post a Comment