MWAKA 2007, Yanga SC ilimpata kocha iliyekuwa inamfukuzia tangu mwaka 2003 bila mafanikio, Milutin Sredojevic ‘Micho’ aliyekuja kurithi mikoba ya Mmalawi, Jack Chamangwana.
Katika mwaka huo wa kwanza kazini, Micho aliifikisha Yanga hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hatua ambayo mara ya mwisho klabu hiyo ilifika mwaka 2001 na kutolewa na Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini, ikiwa chini ya kocha Charles Boniface Mkwasa.
Kwa Micho, timu yake ilitolewa na Esperance ya Tunisia kwa mabao 3-0, waliyofungwa Tunis na baadaye sare ya bila kufungana Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
MAKOCHA YANGA TANGU 1991
1. 1991: Syllersaid Mziray(marehemu)
2. 1993: Nzoyisaba Tauzany (marehemu) (Burundi)
3. 1995: Tambwe Leya (marehemu) (DRC)
4. 1997: Sunday Kayuni
5. 1997: Steve McLennan (Uinegereza)
6. 1998: Tito Mwaluvanda(marehemu)
7. 1999: Raoul Shungu (DRC)
8. 2001: Charles Boniface Mkwasa
9. 2002: Jack Chamangwana (Malawi)
10. 2004: Jean Polycarpe Bonganya (DRC)
11. 2004: Syllersaid Mziray (marehemu)
12. 2005: Kenny Mwaisabula
13. 2006: Jack Chamangwana (Malawi)
14. 2007: Milutin Sredojevic ‘Micho’ (Serbia)
15. 2007: Razack Ssiwa (Kenya)
16. 2007: Jack Chamangwana (Malawi)
17. 2008: Dusan Kondic (Serbia)
18. 2010: Kostadin Papic (Serbia)
19. 2011: Sam Timbe (Uganda)
20. 2011: Kostadin Papic (Serbia)
21. 2012: Tom Saintfiet (Ubelgiji)
22. Ernie Brandts (Uholanz)
Tayari wakati huo kanuni ya timu zinazotolewa kwenye 16 bora ya Ligi ya Mabingwa zinahamia kwenye Kombe la Shirikisho ilikwishaanza kutumika na Yanga ikahamia huko, ilipotolewa na El Merreikh ya Sudan kwa mabao 2-0 ya ugenini, wakianza na sare ya bila kufungana mjini Mwanza.
Yanga iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza nchini kufika hatua hiyo kabla ya Simba nao kufika huko mwaka 2010. Mbali na kuifikisha mbali kwenye michuano ya Afrika, Micho pia aliifikisha Yanga fainali ya ligi ndogo ambako ilifungwa na Simba kwa penalti, langoni mwa Wekundu wa Msimbazi akiwa amesimama Kaseja Juma na kuokoa penalti muhimu za akina Abdi Kassim na Abuu Mtiro.
Hakika ulikuwa mwanzo mzuri kwa kocha Micho na ilitarajiwa msimu uliofuata angeiboresha timu, hususan katika safu ya ushambuliaji ili ifanye vizuri zaidi, lakini ikawa tofauti kabisa, Micho akaondoka.
Alikuwa analipwa mshahara mzuri na Yussuf Manji wakati huo akiwa mfadhili wa klabu kabla hajawa Mwenyekiti. Alipewa gari, aina ya Rav4, nyumba na aliwezeshwa kwa kila alichotaka, ikiwemo kambi za nje ya nchi, yeye mwenyewe kusafiri kwenda kuona mechi za wapinzani wake.
Naweza kusema Micho alikuwa kocha wa kwanza baada ya muda mrefu kufanya kazi katika mazingira mazuri zaidi kwa kiwango cha huduma za klabu hiyo, lakini akaamua kuaga na kuondoka. Nini kilimkera Micho? Rahisi tu, Yanga wajuaji sana, hawapendi ukweli na hawana subira. Mambo haya matatu, kama Yanga hawatabidilika, hakuna kocha mtaalamu anayeweza kuishi nao.
Hatimaye Julai mwaka 2012 Yanga walipata kocha mwingine bora, Mbelgiji Tom Saintfiet, ambaye alidumu kwa siku 80, akiiongoza timu katika mechi 14 na kuiwezesha kutwaa taji moja, Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame.
Saintfiet alifukuzwa baada ya kusema ukweli juu ya udhaifu wa watendaji wa Yanga, wakati timu ilipokwenda kwenye mechi za mikoani za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambako wachezaji hawakupatiwa huduma bora muhimu hususan malazi, matokeo yake ikafanya vibaya.
Kwa kuwa alitoa kauli ambazo ziliwakera viongozi wa klabu, wakaamua kupambana naye. Nani anasajili wachezaji wa Yanga? Viongozi, basi wachezaji kwa uwezo wao mdogo au utashi wakaamua kucheza chini ya kiwango timu ikafanya vibaya katika mechi mbili zaidi na uongozi ukapata sababu rasmi za kumfukuza Tom.
Nakumbuka, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Clement Sanga aliwaambia Waandishi wa Habari kwamba, matokeo mabaya ndio yamefanya Saintfiet asitishiwe mkataba, akimtuhumu Mbelgiji huyo kuwa chanzo.
“Timu ilipokwenda Mbeya, ikatoka sare na Prisons akalalamikia huduma, lakini sisi taarifa tulizozipata, yeye alikwenda kulewa na wachezaji. Kuna mapungufu mengine mengi, ambayo hatuwezi kusema hadharani. Kwa mfano timu ilipotoka Mbeya, tulitaka iende moja kwa moja Morogoro, yeye akalazimisha timu irudi Dar es Salaam, tena iende tena Morogoro. Wachezaji wakachoka sana na hii tunaamini ilichangia hata kufungwa na Mtibwa.
Timu iliporudi kutoka Morogoro, tukaamua iingie kambini, yeye akapinga akisema timu kubwa kama Barcelona Ulaya, hazikai kambini, yaani anataka atupangie kazi sisi, tukaona huyu mtu haendani na maadili ya uongozi na hatufai, tukaamua kusitisha mkataba wake,” alisema Sanga.
Saintfiet aliiongoza Yanga katika mechi 14 tu ndani ya siku 80 tangu ajiunge nayo Julai mwaka jana, akirithi mikoba ya Mserbia, Kostadin Bozidar Papic na katika mechi hizo alifungwa mbili tu, dhidi ya Mtibwa 3-0 na Atletico ya Burundi 2-0.
Katika mechi hizo, zimo sita za Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, ambazo aliiwezesha Yanga kutwaa taji, ikipoteza mechi moja tu dhidi ya Atletico ya Burundi.
Ukweli ni kwamba wana Yanga wengi walisikitishwa na uamuzi wa kufukuzwa kwa Mbelgiji huyo, siku 80 tangu apokewe kwa sherehe kubwa akiwasili nchini kwa ajli ya kufanya kazi Jangwani, wakikumbuka walivyosherehekea naye ubingwa wa Kagame, alivyokuwa akiiongoza vema timu hiyo na zaidi wakakumbuka ahadi zake, ambazo hakupewa fursa ya kuzitimiza, ikiwemo ubingwa wa Afrika.
Lakini wangefanya nini, ikiwa uongozi wao ndio unaowajibika kwa wanachama na mwisho wa siku juu ya uendeshwaji wa timu, hakuna anayeweza kuwaingilia kwa sababu hilo ndilo jukumu walilopewa na wenye timu yao.
Cha kushangaza sasa, kocha aliyefuatia Yanga ni ambaye alikuwa ametoka kufukuzwa APR ya Rwanda mwaka huo huo anaajiriwa Yanga- na ambaye alikutana na Yanga ya Saintfiet mara mbili katika Kombe la Kagame mwaka jana anakafungwa mechi zote.
Alifungwa mechi ya makundi na akafungwa katika Nusu Fainali na kuipa Yanga tiketi ya kwenda kutwaa taji la tano la Kagame kwa kuifunga Azam FC katika fainali, huyo ni Mholanzi Ernie Brandts.
Yanga iliyokuwa inacheza soka nzuri chini ya Saintfiet taratibu ikaanza kupoteza ubora wake na pamoja na jitihada za uongozi kusajili wachezaji ghali, bado haikusaidia.
Chini ya Brandts, viwango vya wachezaji Yanga vilianza kufa taratibu, ingawa bado uongozi uliona ni wachezaji wenyewe ndiyo tatizo na wengine wakatupiwa virago.
Lakini hata wachezaji wapya bora waliosajiliwa chini ya Brandts nao viwango vinashuka kwa kasi- tazama akina Mrisho Ngassa, Mbuyu Twite, Said Bahanuzi, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Hamisi Kiiza, Frank Domayo, David Luhende, Simon Msuva, Nizar Khalfan, Kevin Yondan na hata Hussein Javu aliyesajiliwa ‘juzi’ tu, je wapo katika ubora wao wa awali?.
Nilimsikitikia sana kiungo mwenye kipaji na chipukizi, Hassan Dilunga wakati anasaini Yanga, Brandts akiwa bado kocha, ila kwa sasa matumaini ya kukuza soka yake yamefufuka, inategemea na kocha mpya atakayeingia timu hiyo.
Said Bahanuzi bado mchezaji mzuri sana. Ameuliwa na kocha bomu tu ambaye Yanga waliingia mkenge. Hussein Javu ni mchezaji mzuri sana, lakini hakufaa kwa kocha ‘maroroso’ tu, lakini mbele ya mwalimu kweli, ataibeba sana timu hiyo na hata kuwa tegemeo la timu ya taifa ya nchi.
Sasa jiulize, kwa makosa ambayo viongzi wa Yanga wamefanya kutoka kwa Saintfiet hadi Brandts kuna lolote wamejifunza?
Kumbuka tangu mwaka 1991, Brandts anakuwa kocha wa 19 kutupiwa virago Yanga na katika kipindi chote hicho ni makocha watatu tu, waliorudishwa kazini, baada ya kuondoka, ambao ni Syllersaid Mziray (sasa marehemu), Mmalawi Jack Chamangwana na Mserbia Kostadin Papic.
Baadhi ya makocha waliamua kuondoka wenyewe, lakini wengi wao walifukuzwa na tawala mbalimbali zilizopita katika klabu hiyo katika kipindi chote hicho.
Kwa nini nimeanzia 1991, ndicho kipindi ambacho vurugu vurugu za kufukuza makocha zilipoanza katika klabu hiyo, tofauti na miaka ya nyuma tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo mwaka 1939.
Mapema mwaka 1991, Yanga ilimchukua kocha maarufu zamani nchini, Syllersaid Salmin Kahema Mziray, ambaye aliondoka kwa watani wa jadi, Simba SC, baada ya kushushwa cheo kutoka Simba A hadi Simba B.
Mziray aliiongoza Yanga kwa miaka miwili, akiwa anasaidiwa na Charles Boniface Mkwasa na akaiwezesha kutwaa ubingwa wa Bara na Muungano mfululizo, sambamba na kuwafikisha Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, ambako walifungwa kwa matuta na watani wa jadi, Simba SC mwaka 1992.
Lakini baada ya hapo, marehemu Mziray aliondoka Yanga kutokana na kupata ofa nzuri kutoka Pan African, wakati huo ikiwa inafadhiliwa na Murtaza Dewji, ambaye alikuwa anaipigania irejee Ligi Kuu.
Yanga iliajiri tena kocha wa kigeni baada ya muda mrefu, ikimleta Mrundi, Nzoyisaba Tauzany ‘Bundes’ 1993 (sasa marehemu) ambaye aliendelea kufanya kazi na Mkwasa na katika mwaka wake wa kwanza, akaiwezesha timu hiyo kutwaa Kombe la Kagame mjini Kampala, Uganda.
Tauzany aliporejea katika Ligi Kuu akaendelea vizuri na kazi, lakini haikuchukua muda akaingia kwenye mgogoro na mfadhili wa klabu hiyo wakati huo, Abbas Gulalamli (sasa marehemu).
Tauzany alitumia vyombo vya habari kupambana na Gulamali na ilifikia hadi akawa anachafua jina la Mbunge huyo wa zamani wa Kilombero, Morogoro kwa kusema anafanya biashara haramu ya dawa za kulevya. Ilikuwa vita kali na mbaya zaidi hata Mrundi hiyo alikuwa anakubalika mbele ya wanachama, hivyo kumfukuza ikawa tabu. Alichokifanya Gulamali, akamrejesha kocha ambaye alifanya kazi na kupendwa mno Yanga, Tambwe Leya kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambaye awali alifanya kazi mwaka 1975 na 1976, akiiwezesha Yanga kuifunga Simba katika mechi ya kihistoria Nyamagana kabla ya kuipa Kombe la kwanza la Kagame 1975, kwa kuwafunga hao hao Simba 2-0 Uwanja wa Amaan, Zanzibar.
Tambwe alitua nchini mwishoni mwa mwaka 1994 na jukumu lake alilopewa ni Ukurugenzi wa Ufundi, ambapo yeye akaamua kutengeneza timu nzuri ya vijana, iliyopewa jina Black Stars.
Tauzany na kikosi cha Yanga chenye mastaa kibao nchini wakati huo, akafungwa mabao 4-1 na Simba SC na hapo ndipo timu nzima na kocha wao wakafukuzwa, wakabaki wachezaji saba tu ambao waliunganishwa na yosso wa Tambwe kutengeneza kikosi kipya, kilichofanya vizuri hadi kufika Robo Fainali ya Kombe la Washindi 1996.
Tambwe naye akaondolewa kwa visa na badala yake akaajiriwa kocha mzalendo, Sunday Burton Kayuni 1997 ambaye naye pia hakudumu, kwani alikfukuzwa na akaajiriwa kocha wa muda kutoka Uingereza, Steve McLennan mwaka huo huo 1997.
McLennan, kocha Mzungu wa kwanza mimi kufanya naye kazi Yanga, aliondolewa naye na nafasi yake akakaimu kwa muda aliyekuwa Msaidizi wake, Juma Pondamali ‘Mensah’.
Siwezi kusahau siku alipofukuzwa McLennan, alimfuata msaidizi wake ambaye aliachiwa timu na kumuuliza; “Juma nani ni kocha mzuri, mimi au wewe?” Pondamali akawa anacheka tu, wapo kwenye basi timu inatoka Zanzibar kwenye mechi za Ligi ya Muungano.
Yanga ikaajiri kocha wa muda, ambaye alikuwa hajulikani kabisa, Tito Oswald Mwaluvanda (sasa marehemu) ambaye katika kujikosha kwa wanachama, aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo wakati huo, Rashid Ngozoma Matunda (sasa marehemu pia) akawa anamtambulisha kama Msimamizi wa mazoezi, wakati timu inatafuta kocha.
Msimamizi wa mazoezi alichukua ubingwa wa Ligi Kuu na Ligi ya Muungano 1998, tena akiweka rekodi ya ushindi mnono zaidi katika Ligi ya Bara, mabao 8-0 waliyoifunga Kagera Shooting Stars (sasa Kagera Sugar), tena ikiwa inafundishwa na kocha wa timu ya taifa, Taifa Stars wakati huo, Zacharia Kinanda ‘Arrigo Sachi’ (sasa marehemu), Edibilly Jonas Lunyamila akifunga mabao matano peke yake.
Mungu amrehemu Kinanda, lakini siku hiyo Lunyamila alimfikishia ujumbe, kwani kocha huyo alikuwa hamtaki Eddy katika timu ya taifa- hivyo zile bao tano alizofunga ilikuwa ujumbe tosha, kwamba alikuwa anakosea.
Kana kwamba hiyo haitoshi, Mwaluvanda aliifikisha Yanga hadi hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, akiweka rekodi mbili kuifanya hiyo iwe klabu ya kwanza Tanzania kucheza hatua hiyo, yeye kuwa kocha wa kwanza mzalendo na wa mwisho hadi sasa kuifikisha timu katika hatua hiyo.
Lakini pamoja na yote, mwaka 1998 mara tu baada ya Yanga kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa, marehemu Mwaluvanda aliyekuwa anasaidiwa na Freddy Felix Isaya Kataraiya Minziro ‘Majeshi’ wakaondolewa wote na akaajiriwa kocha kutoka DRC, Raoul Jean Pierre Shungu aliyeingia na msaidizi wake, Abeid Mziba ‘Tekero’.
Hii ilimuuma sana Mwaluvanda, kwa sababu ili kuingia hatua ya makundi ilibidi azitoe Rayon ya Rwanda iliyokuwa inafundishwa na Shungu na baadaye Coffee ya Ethiopia, lakini marehemu akawa anasema afadhali angeletwa kocha mwingine, si yule ambaye ameitoa timu yake kwenye mashindano. Wakubwa wakishaamua huwezi kupingana nao.
Shungu aliipa Yanga Kombe la tatu la Kagame, katika michuano iliyofanyika mjini Kampala, Uganda 1999, lakini mwaka 2000 akaondolewa na akaajiriwa Charles Boniface Mkwasa ‘Master’, ambaye naye mwishoni mwa mwaka 2001, akatupiwa virago pia.
Tangu 2002 hadi sasa ni miaka 10 tu, lakini katika kipindi hicho Yanga imefundishwa na makocha 11, tena wengine wakifukuzwa na kurudishwa kwenye kipindi hicho.
Alipoondolewa Master Mkwasa, akaajiriwa Mmalawi Jack Lloyd Chamangwana ambaye mwaka 2003, alifukuzwa na mwaka 2004 akaajiriwa kocha kutoka DRC, Jean Polycarpe Bonghanya ambaye naye hakudumu, mwaka huo huo akaondolewa na kurudishwa Syllersaid Mziray.
Marehemu Mziray alikuwa anasoma ishara za nyakati tu, naye alipoona upepo unaelekea kuwa mbaya akamuachia timu aliyekuwa Msaidizi wake, Kenny Mwaisabula.
Mwaisabula akaendelea na kazi hadi msimu wa 2005, lakini baadaye mwaka huo akaondolewa na kurejeshwa Chamangwana, ambaye alifanya kazi hadi 2007 alipompsha Mserbia, Milutin Sredojevic ‘Micho’.
Micho aliondoka kwa sababu ambazo hadi leo bado hazieleweki, kwani alikubalika na timu ilikuwa inafanya vizuri. Alipoondoka Micho, timu akabakia nayo, aliyekuwa kocha wa makipa, Mkenya Razack Ssiwa.
Ssiwa akaiongoza Yanga kutwaa Kombe la Tusker mwaka 2007 mjini Mwanza, lakini aliporudi kwenye ligi, timu inafanya vibaya, naye akatupiwa virago na kurejeshwa Chamangwana.
Chamangwana naye akaondolewa na kuajiriwa tena Mserbia, Profesa Dusan Savo Kondic, aliyekuja na Wasaidizi wawili, Spaso Sokolovoski na Civojnov Serdan. Kondic naye mwaka 2010 akafukuzwa na kuajiriwa Mserbia mwenzake, Kostadin Papic, ambaye naye alifukuzwa na kuajiriwa Mganda Sam Timbe.
Timbe pamoja na kuipa timu Kombe la nne la Kagame mwaka 2010, alifukuzwa miezi miwili baadaye na kurejeshwa Papic, ambaye pia hata kabla msimu kumalizika akatupiwa virago na kuajirwa Mbelgiji, Saintfiet.
Saintfiet alifukuzwa baada ya siku 80, akiiongoza timu katika mechi 14, akishinda 12, sare moja na kufungwa mbili- huku akiacha Kombe la tano la Kagame Yanga.
Brandts naye baada ya kuiongoza Yanga katika mechi 50, akiiwezesha kushinda mechi 29, sare 13 na kufungwa nane, amefukuzwa, akiwa ameipa timu taji moja la ubingwa wa Ligi Kuu msimu uliopita na msimu huu hadi sasa akiwa ameifanya timu hiyo iongoze Ligi Kuu baada ya mzunguko wa kwanza.
Sawa tu kwa Brandts kuondolewa, kwa sababu kiwango cha timu kilishuka na kipindi chake ndicho ambacho uongozi ulitumia fedha nyingi zaidi kusajili tena wachezaji bora, lakini faida ya maana haikuonekana, ila kabla yake, kuna makocha wa maana waliondolewa katika timu hiyo ambao, wangeweza kuiletea manufaa klabu.
Wazi baada ya makosa ambayo viongozi wa Yanga wamefanya siku za karibuni katika suala la makocha, inaweza kuwa wamejifunza kitu, lakini je watakuwa tayari kubadilika na kuukubali ukweli wanapokoslewa na walimu? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri kuona. Nianze mapema kuwatakia heri ya mwaka mpya wapendwa wasomaji wangu. Namshukuru Mungu kwa kuniweka pamoja nanyi kwa miaka mingi, tangu naitwa bwana mdogo hadi sasa ‘babu’. Mungu atujaalie sote maisha marefu na ufanisi katika mambo yetu. Amin.
0 comments:
Post a Comment