Na Mahmoud Zubeiry, Nairobi
BAO pekee la Haroun Athumani Chanongo dakika ya 57 limetosha kuipa Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars ushindi mwembamba wa 1-0 dhidi ya Somalia mchana wa leo katika mchezo wa Kundi B, Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge Uwanja wa Nyayo, Nairobi, Kenya.
Kwa matokeo hayo, Stars imetimiza pointi nne baada ya awali kutoa sare ya 1-1 na Zambia katika mchezo wake wa kwanza na mustakabali wake wa kuingia Robo Fainali utategemea matokeo ya mechi za mwisho za kundi hilo.
Katika mchezo wa leo, Stars ilikuwa inaanza vizuri kutokea nyuma, lakini wanapofika kwenye eneo la wapinzani wanaharibu, ama kwa kupeana pasi mbovu au kupokonywa mipira kirahisi.
Na hakukuwa na uelewano kabisa baina ya washambuliaji wa Stars, Elias Maguri, Amri Kiemba na Mrisho Ngassa hali ambayo ilifanya mabeki wa Somalia wacheze kwa uhuru zaidi.
Somalia walicheza vizuri kipindi cha kwanza na kukosa mabao mawili ya wazi, kutokana na juhudi za kipa Ivo Mapunda kuokoa hatari zote.
Kipindi cha pili, kocha Mdenmark Kim Poulsen alianza na mabadiliko, akiwatoa Kiemba na Maguri na kuwaingiza washambuliaji wawili a Simba SC, Ramadhani Singano na Haroun Chanongo ambao walibadilisha mchezo.
Pasi nzuri ya Singano ‘Messi’ iliunganishwa nyavuni na Chanongo dakika ya 57 kuipatia Stars bao hilo pekee.
Baada ya bao hilo, Stars iliendelea kushambulia kupitia kwa Singano na Chanongo, lakini wakaishia kukosa mabao ya wazi. Somalia nayo iliendelea kushambulia lango la Stars na kuishia kukosa mabao mawili ya wazi, sifa zimuendee Ivo Mapunda.
Kim Poulsen alimtoa Mrisho Ngassa dakika ya 79 na kumuingiza Farid Mussa, lakini mabadiliko hayo hayakuleta jipya upande wa Stars.
Kikosi cha Stars leo kilikuwa; Ivo Mapunda, Himid Mao, Erasto Nyoni, Said Morad, Kevin Yondan, Frank Domayo, Salum Abubakar, Athumani Iddi ‘Chuji’, Elias Maguri/Haroun Chanongo dk46, Amri Kiemba/Ramadhani Singano ‘Messi’ dk46 na Mrisho Ngassa/Farid Mussa dk79.
Somalia; Mohamed Sherif, Hassan Ali Roble, Mohammed Tahlil Shidane, Aden Hussein Ibrahim, Hassan Hussein Mohamed, Daud Abdullah Hassan, Sidi Mohamed Omer, Mohamed Abdi Hayow/Mahmoud Adi Mohamed dk63, Jabril Hassan Mohamed, Mohamed saleh Hussein na Sadaq Abdulkadir Mohamed/Deki Abdullah Nur dk88.
0 comments:
Post a Comment