// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); AZAM IMEPATA KOCHA MWINGINE BORA, LAKINI ATADUMU? - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE AZAM IMEPATA KOCHA MWINGINE BORA, LAKINI ATADUMU? - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Sunday, December 01, 2013

    AZAM IMEPATA KOCHA MWINGINE BORA, LAKINI ATADUMU?

    AZAM FC imeajiri kocha wa tano wa kigeni jana katika kipindi cha miaka sita ya kushiriki kwake Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ambaye ni Mcameroon Joseph Marius Omog iliyempa Mkataba wa miaka miwili.
    Baada ya kupanda Ligi Kuu, kocha wa kwanza mgeni kuajiriwa alikuwa ni Neider dos Santos kutoka Brazil, wa pili akawa Mbrazil pia Itamar Amorin wa tatu Muingereza Stewart Hall na wa nne Mserbia Boris Bunjak.

    Leo tungekuwa tu tunahesabu Omog ni kocha wa sita ndani ya misimu sita ya Azam kuwapo Ligi Kuu, kama tu klabu hiyo isingemrejea kocha iliyemfukuza na kumuajiri Bunjak, Stewart Hall Desemba mwaka jana.
    Walifukuzwaje sasa? Katika msimu wake wa kwanza, Azam ikiwa bado inaundwa na wachezaji wengi waliopandisha timu, ilimfukuza Santos baada ya kufungwa na Simba SC.
    Itamar aliondoka kwa sababu ya kuzidiwa nguvu na wachezaji wasio na nidhamu mbele ya uongozi- wakati Stewart mara ya kwanza aliondolewa tu katika mazingira ambayo hayakueleweka kabisa. Basi, walimchoka tu na wakamuajiri Bunjak.
    Mserbia huyo naye, pamoja na kuiongoza vizuri timu ikiwa kwenye mbio za ubingwa hadi mwishoni mwa mzunguko wa kwanza, baada ya kufungwa na Simba SC tu, naye akafukuzwa. Akarudi Stewart na akafanikiwa kuzifunga Simba na Yanga katika Ligi Kuu msimu huu, lakini haikutosha baada ya mzunguko wa kwanza, akaambiwa aondoke.
    Busara ilitumika kwa kumbana yeye mwenyewe atangaze kujiuzulu na akafanya hivyo, lakini ukweli ni kwamba Stewart alifukuzwa na sababu kubwa ni timu kupelekwa kambini Afrika Kusini kwa wiki mbili, lakini imerudi nyumbani haichezi soka ya kiwango cha juu ambacho wenye timu walitarajia.
    Kambi ya wiki mbili, urejee nyumbani ucheze kama Barcelona. Hiyo ni babu kubwa. Wachukue Al Ahly ya Misri wapeleke Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya wakacheze na Prisons au Mbeya City kama watashinda. Wakati mwingine tunapaswa kutazama hata mazingira yetu kabla ya kuchukua maamuzi.
    Siwezi kuwalaumu Azam kwa kubadilisha makocha kama shati, lakini wanapaswa tu kujiuliza kama mwenendo wanaokwenda nao ni sahihi na pia kutazama sababu ambazo zinawasukuma kuachana na kocha mmoja hadi kwenda kwa kocha mwingine.
    Mapinduzi ya Azam katika soka ya Tanzania yasiishie katika kuwa na Uwanja mzuri tu na akademi, bali pia katika sera na mfumo wa uendeshwaji. Azam lazima ijitofautishe sana na Simba na Yanga.
    Simba na Yanga zinafukuza makocha na kusingizia wachezaji wamehujumu timu, ili kujikosha kwa wanachama wake- lakini Azam pale kuna presha gani? Inafahamika, wapo watu ni tatizo pale Azam kwa sababu hawana majukumu mengi, kwa hivyo wanatumia muda mwingi kupiga mizengwe na kupika majungu tu, hali ambayo wakati mwingine inawakwaza hadi wachezaji.
    Ukweli ni kwamba Azam lazima ibadilike kwa ujumla na pia inahitaji Mtendaji Mkuu wa klabu, mwenye upeo wa juu na mweledi ambaye atahakikisha pia uendeshwaji wa akademi unakuwa wenye tija na si kulundika tu vijana pale bila mpango wowote hadi wanazeeka hawajanufaika na lolote.
    Leo hii Azam akademi inafanya vibaya katika Kombe la Uhai, zinaletwa siasa za wachezaji kuchukuliwa timu ya taifa ndio kumeathiri timu- hapana vyema Azam wakaangalia tatizo la msingi, maana akademi ile ina vijana wengi na mafunzo ni kila siku.
    Akademi ijivunie matunda ya wachezaji wake kuchukuliwa timu ya taifa, lakini pia itazame matokeo ya Kombe la Uhai kwa jicho la tatu. Tukirejea kwenye suala la makocha, sasa Azam imepata kocha mwingine bora kama ilivyo bahati yao, Omog aliipa A.C. Leopard FC ya Kongo Brazzaville Kombe la Shirikisho Afrika mwaka jana.
    Mchezaji huyo wa zamani wa Yaounde ni mwalimu wa kiwango cha juu cha ufundishaji soka na elimu ya viungo aliyehitimu vizuri mafunzo yake katika Chuo cha Vijana na Michezo, INJS mjini Yaounde. Alikwenda kujiendeleza kielimu nchini Ujerumani na kwa pamoja na Pierre Njili na Martin Ndtoungou walipata Stashahada za ukocha na leseni za UEFA daraja la B mwaka 1987. 
    Aliporejea nchini mwake, Joseph Marius Omog, alifundisha timu kadhaa kama Fovu ya Baham na Aigle ya Menoua na akazifikisha fainali ya Kombe la Cameroon klabu zote. 
    Mwaka 2001 aliteuliwa kuwa Msaidizi wa kocha Mjerumani, Winfried Schafer katika timu ya taifa ya Cameroon, Simba Wasiofungika chini ya Nahodha Samuel Eto’o haswa kutokana na kujua kwake Kijerumani, kwa sababu kocha huyo alikuwa hazungumzi Kiingereza wala Kifaransa, lugha za Cameroon. 
    Mwaka 2003 aliteuliwa kuwa kocha Mkuu wa timu ya taifa baada kuondoka kwa Winfried Schafer, lakini akafukuzwa mwaka 2010 kutokana na matokeo mabaya na kushindwa kuiwezesha Cameroon kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika.
    Akaamua kutoka nje ya nchi na mwaka 2011 alijiunga na A.C. Leopard ya Kongo na kuiwezesha kutwaa Kombe mwaka huo huo na kuipa tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho. 
    Na akafanikiwa kuiwezesha timu hiyo kutwaa Kombe hilo la Afrika kwa kuifunga Djoliba ya Mali mabao 2-1 katika mchezo wa marudiano na kutengeneza ushindi wa jumla wa 4-3.
    Wazi hapa Azam FC imepata mwalimu mwingine bora, mwenye uzoefu wa kuishi na wachezaji wakubwa duniani katika timu kama akina Eto’o na Alex Song anayekuja kurithi mikoba ya Stewart Hall.
    Lakini uongozi na wamiliki wa Azam, wanapaswa kujua kwamba mwalimu huyo atahitaji muda ili kuleta mafanikio Chamazi na wawe tayari kuwa na subira hiyo kwa kumpa muda. Wahadha asalam alaykum.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: AZAM IMEPATA KOCHA MWINGINE BORA, LAKINI ATADUMU? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top