• HABARI MPYA

    Thursday, November 14, 2013

    ZANZIBAR HEROES YAPIGA KAMBI BWAWANI HOTEL

    Na Salum Vuai, Zanzibar
    KIKOSI cha wachezaji 22 cha timu ya taifa ya Zanzibar Heroes, jana kimeingia kambini katika hoteli ya Bwawani kujiandaa na michuano ya  Chalenji, inayotarajiwa kuanza Novemba 27 mwaka huu nchini Kenya.
    Katibu Mkuu wa Chama cha Soka Zanzibar ( ZFA) Kassim Haji Salum, ameliambia gazeti hili kuwa, kambi hiyo inakadiriwa kugharimu shilingi milioni 22, kwa ajili ya huduma za chakula na malazi kwa wachezaji hao na viongozi watano.
    Zanzibar One; Kipa namba moja wa Heroes, Mwadini Ally bado hajajiunga na timu kwa sababu yuko katika kambi ya Taifa Stars

    Alisema kikosi hicho kitabaki kambnini hadi kitakapoondoka kwenda Kenya Novemba 25 kwa ajili ya ngarambe hizo zinazoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).
    Katika hatua nyengine, Katibu huyo alisema bado ZFA inahitaji misaada zaidi katika kuigharamia timu hiyo, ikiwemo fedha za posho kwa wachezaji na viongozi.
    Aliziomba kampuni na mashirika mbalimbali kuendelea kuichangia timu hiyo, ambayo inakwenda Kenya kupeperusha bendera ya Zanzibar, katika mashindano hayo ambayo Uganda ndiyo mabingwa watetezi.
    Kassim alisema, jana walipokea hundi ya shilingi 1,500,000 kutoka kwa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) ukiwa mchango wake katika maandalizi ya timu hiyo, na hivyo kufikisha shilingi milioni 12 ambazo taasisi kadhaa zimeichangia Zanzibar Heroes.
    Wakati huohuo, timu hiyo ya taifa ya Zanzibar, juzi iliichabanga Kimbunga inayocheza ligi daraja la kwanza mabao 5-0 katika mchezo wa kujipima nguvu uliochezwa uwanja wa Ngome Fuoni.
    Huo ni mchezo wa tatu kwa timu hiyo, ambapo kabla ilicheza na Kijichi na Miembeni, na kuibuka na ushindi sawa wa bao 1-0 katika kila mechi.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: ZANZIBAR HEROES YAPIGA KAMBI BWAWANI HOTEL Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top