Na Mahmoud Zubeiry, Machakos
TANZANIA Bara, Kilimanjaro Stars imeanza taratibu michuano ya Kombe la
Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Challenge baada ya kutoa sare ya
1-1 na mabingwa wa zamani wa Afrika, Zambia au Chipolopolo kwenye Uwanja wa
Kenyatta, Machakos, Kenya.
Katika mchezo huo wa Kundi B, Zambia ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao
kupitia kwa Ronald Kampamba dakika ya 41, akiunganisha kwa kichwa krosi ya
Felix Katongo.
Zambia walitawala zaidi mchezo huo kipindi cha kwanza na kutengeneza nafasi
zaidi ya nne za kufunga, lakini sifa zimuendee kipa Ivon Philip Mapunda
aliyeokoa michomo kadhaa ya hatari.
Mrisho Ngassa akishangilia baada ya Said Morad (hayupo pichani) kuisawazish Stars, huku kipa wa Zambia na mabeki wake wakiwa wameduwaa |
Kipindi cha pili, Stars ilibadilika mno kiuchezaji, japokuwa wachezaji
waliomaliza kipindi cha kwanza ndiyo wote waliorejea kuanza ngwe hiyo ya lala
salama.
Kutokana na mshambulizi mfululizo langoni mwa Zambia, Bara walipata kona
dakika ya 48 ambayo ilikwenda kuchongwa na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na
kuunganishwa nyavuni na Said Morad kwa kichwa.
Baada ya bao hilo, Zambia walianza kuutafuta mpira kwa tochi na kama si
umahiri wa kipa wao, Nsabata Toaster kuokoa hatari nyingi, Stars wangeweza
kuondoka na ushindi.
Kwa matokeo hayo, Burundi inaongoza kundi hilo baada ya kuifunga Somalia
2-0 katika mchezo wa kwanza wa kundi hilo kwenye Uwanja huo.
Kikosi cha Stars kilikuwa; Ivo Mapunda, Himid Mao, Erasto Nyoni, Said
Morad, Kevin Yondan, Frank Domayo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’/Ramadhani Singano
‘Messi’ dk89, Hassan Dilunga/Athumani Iddi ‘Chuji’ dk85, Elias Maguri/Haroun
Chanongo dk72, Amri Kiemba na Mrisho Ngassa.
Chipolopolo; Nsabata Toaster, Bronson Chama, Jimmy Chisenga/Kabaso Chongo
dk67, Christopher Munthali, Rodrcik Kabwe, Stanley Nshimbi/Alex Nshimbi dk57,
Sydney Kalume, Kondwani Mtonga, Felix Katongo/Salulani Phiri dk73, Ronald
Kampamba na Festus Ndewe.
0 comments:
Post a Comment