// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); STEWART: VIGUMU TIMU NJE YA SIMBA NA YANGA KUWA BINGWA BARA, KWA SABABU ZINABEBWA SANA NA TFF - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE STEWART: VIGUMU TIMU NJE YA SIMBA NA YANGA KUWA BINGWA BARA, KWA SABABU ZINABEBWA SANA NA TFF - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Saturday, October 12, 2013

    STEWART: VIGUMU TIMU NJE YA SIMBA NA YANGA KUWA BINGWA BARA, KWA SABABU ZINABEBWA SANA NA TFF

    Na Mahmoud Zubeiry, Dar es Salaam
    KOCHA Mkuu wa Azam FC, Muingereza Stewart Hall amesema kwamba ni kazi ngumu Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kupata bingwa nje ya Simba na Yanga kwa sababu timu hizo zinapendelewa mno na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
    Akizungumza katika mahojiano maalum na BIN ZUBEIRY jana usiku, Hall amesema kwamba timu nyingine nje ya Simba na Yanga SC ili kuwa bingwa inabidi ifanye kazi ngumu sana ambayo kwa sasa yeye na timu yake, Azam FC wanajaribu.
    Kwanza amesema ratiba ya Ligi Kuu inapopangwa inakuwa katika mazingira mazuri kwa timu hizo na mazingira magumu kwa timu nyingine ambazo zinaonekana zikitendewa haki zinaweza kuzima ubabe wa timu hizo katika soka ya Tanzania.
    Ubingwa mgumu; Kocha wa Azam, Stewart Hall amesema Simba na Yanga zinabebwa sana na TFF

    Stewart alitoa mfano hadi sasa katika mechi za Ligi Kuu ambazo tayari zimechezwa, Simba na Yanga kila moja imecheza mechi mbili tu ugenini, wakati Azam FC imecheza mechi sita ugenini, jambo ambalo amesema huwezi kulikuta katika ligi nyingine yoyote duniani.
    “Ligi lazima iwe ya uwiano sawa wa mechi za nyumbani na ugenini kwa kila timu, lakini hiyo si kwa hapa Tanzania, kuna ratiba maalum kwa ajili ya Simba na Yanga, namna hii usitegemee soka ya nchi hii ikakua,”alisema.
    Lakini pia, Stewart amesema wakati timu nyingine zinacheza mechi 13 nyumbani na 13 ugenini, kwa Simba na Yanga wanacheza mechi saba tu ugenini na hakuna sabau ya msingi katika hilo.
    “Sisi Azam ni washindani wa Simba na Yanga katika mbio za ubingwa, lakini hatupati nafasi ya kucheza na hizo timu Uwanja wetu wa nyumbani, tunacheza nao ugenini mechi zote. Kwa nini hawaji Chamazi?”alihoji Stewart.
    Lakini pia Stewart alihoji juu ya sababu ya Azam, kwenda kucheza na Ruvu Shooting Uwanja wa Mabatini, Mlandizi, wakati Simba na Yanga wanacheza na timu hiyo mechi zote Uwanja wao wa nyumbani, Taifa, Dar es Salaam.
    Gaudence Mwaikimba wa Azam kushoto anatakiwa kufanya kazi ya ziada kuisaidia timu yake itimize ndoto za ubingwa, kwa sababu Simba na Yanga zinabebwa 

    “Lakini hii si haki, na kwa namna hii unafikiri lini timu nyingine nje ya Simba itakuwa bingwa hapa, ni vigumu sana, lazima TFF wahakikishe haki inatendeka katika Ligi hii,”alisema.
    Pamoja na hayo, Stewart amesema malengo ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa timu yake msimu huu yapo pale pale pamoja na ukweli huo wa Simba na Yanga kubebwa na TFF.
    “Tumeanza ligi katika mazingira magumu, tumekuwa na majeruhi wengi na bahati mbaya mwanzoni tu, beki wetu tegemeo Aggrey Morris akapewa kadi nyekundu, lakini tunapambana kuhakikisha tunamudu kucheza ligi katika mazingira haya magumu,”.
    “Na unaweza kuona hatupo mbali na eneo la ubingwa, tupo nafasi ya pili na wakati wowote tunaweza kupanda kileleni, tunajituma sana kama timu na kila mtu binafsi kuhakikisha tunatimiza malengo tuliyojiwekea msimu huu, kutwaa ubingwa,”alisema.    
    Akiizungumzia Ligi Kuu kwa ujumla, Stewart alisema msimu huu ni ngumu zaidi tofauti na msimu uliopita na hategemei kama kuna timu itafikisha pointi zaidi ya 56 na kwamba bingwa hataiacha kwa pointi nyingi timu itakayoshika nafasi ya pili. 
    “Kwa sababu Coastal Union imejiimarisha msimu huu, imetumia fedha kusajili wachezaji wazuri na wana timu nzuri sasa. Pia, kuna Mbeya City ni timu nzuri, kwa hivyo unaweza kuona msimu huu una mechi ngumu zaidi, kuliko msimu uliopita,”.
    “Mechi za mikoani kwa ujumla zote ngumu, Tabora kuna Rhino ni kugumu, Bukoba kuna Kagera ni kugumu, Manungu kuna Mtibwa ni kugumu, Mlandizi kuna Ruvu Shooting ni kugumu, labda unaweza kuvuna pointi Arusha kwa JKT Oljoro, lakini hata Mgambo JKT wakiwa Tanga ni wagumu pia, kama Coastal,”alisema.
    Stewart alizungumzia hali ya ubovu wa viwanja vya mikoani  nayo pia inaongeza ugumu, lakini akasikitika zaidi na hali aliyokutana nayo Uwanja wa Mkwakwani, Tanga wiki iliyopita akitoa sare ya bila kufungana na Coastal Union.
    “Tumecheza na Coastal Tanga, kumbe siku moja kabla ya mechi waliruhusu kufanyika tamasha kubwa la muziki, unawezaje kuruhusu maelfu ya watu kuutimba Uwanja usiku wa kuamkia mechi nzuri kama Azam na Coastal. Zote ni timu nzuri, lakini zilishindwa kucheza kwa ubora wao kutokana na hali mbaya ya Uwanja, tumecheza tunakanyaga chupa na kondomu uwanjani,”.
    “Hivi kwa hali kama hii unategemea soka ya Tanzania itawezaje kuendelea, unawezaje kuruhsuu tamasha la muziki katikati ya Uwanja usiku wa kuamkia mechi ya Ligi Kuu, hii ni hapa hapa Tanzania tu, siyo kwingine,”alisema.
    Akizungumzia nafasi ya timu yake msimu huu pamoja na changamoto hizo, Stewart amesema kutokana na hali halisi ya ligi, anahitaji kumaliza mzunguko wa kwanza angalau akiwa na pointi 26 ambazo ni sawa na wastani wa pointi mbili kwa mechi.
    “Katika mechi 13, ukifanikiwa kuvuna wastani wa pointi mbili kwa mchezo mmoja, ina maana utamaliza mzunguko wa kwanza na pointi 26 na kwa pointi hizo kama hautakuwa kileleni mwa ligi, basi utakuwa wa pili,”alisema.
    Kuhusu Simba SC ambao wanaongoza ligi kwa sasa, Stewart amesema kwamba haipi nafasi timu hiyo kumaliza juu ya Yanga na Azam mwishoni mwa msimu, kwa sababu msimu huu wanajaribu kujenga timu yao.
    “Nimewaona Simba SC mara mbili, na nitawaona tena kesho (leo), Simba SC wanajenga timu. Hawana uzoefu ambao wanao Yanga SC, hawajatumia fedha (kusajili), hawako vizuri pamoja na kuwasajili Warundi wawili (Amisi Tambwe na Kaze Gilbert), wanahitaji muda na wanatakiwa kuwa wavumilivu hadi msimu ujao,”alisema.
    Stewart amesema kwa mara nyingine mbio za ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu zitakuwa za Azam na Yanga SC, ingawa amesema lolote linaweza kutokea na kama si Simba, basi timu nyingine inaweza kubadilisha matokeo.
    Lakini Stewart amesema anawapa nafasi kubwa Yanga SC kutetea ubingwa kwa kuwa ndiyo timu bora katika Ligi Kuu kwa sasa kutokana na uzoefu wake- ingawa amesistiza watapambana nao hadi filimbi ya mwisho.
    Katika historia ya Ligi Kuu tangu mwaka 1966, mbali na Simba na Yanga timu nyingine zilizowahi kutwaa taji la ligi hiyo ni Mseto ya Morogoro mwaka 1975, Pan African ya Dar es Salaam mwaka 1982, Tukuyu Stars ya Mbeya mwaka 1986, Coastal Union ya Tanga mwaka 1988 na Mtibwa Sugar ya Morogoro mara mbili mfululizo, 1999 na 2000. 
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: STEWART: VIGUMU TIMU NJE YA SIMBA NA YANGA KUWA BINGWA BARA, KWA SABABU ZINABEBWA SANA NA TFF Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top