// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); SIMBA SHUGHULI PEVU KWA PRISONS, YANGA SC NA KAGERA PATACHIMBIKA KAITABA KESHO LIGI KUIU - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE SIMBA SHUGHULI PEVU KWA PRISONS, YANGA SC NA KAGERA PATACHIMBIKA KAITABA KESHO LIGI KUIU - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Friday, October 11, 2013

    SIMBA SHUGHULI PEVU KWA PRISONS, YANGA SC NA KAGERA PATACHIMBIKA KAITABA KESHO LIGI KUIU

    Na Boniface Wambura, Dar es Salaam
    LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inakamilisha raundi ya nane kesho (Oktoba 12 mwaka huu) kwa mechi tatu zitakazochezwa Dar es Salaam na Bukoba mkoani Kagera.
    Simba ina fursa ya kuendelea kukamata usukani wa ligi hiyo iwapo itaishinda Tanzania Prisons ya Mbeya katika mechi itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni. Tanzania Prisons inayofundishwa na Jumanne Chale inashika nafasi ya kumi na moja katika msimamo wa ligi hiyo.
    Ili iendelee kupanda katika nafasi za juu kwenye msimamo wa ligi hiyo iliyoanza Agosti 24 mwaka huu, Tanzania Prisons ambayo katika mechi yake iliyopita ugenini ilipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mgambo Shooting inalazimika kuifunga Simba.
    Yanga wapo Kaitaba kesho

    Licha ya sare ya bao 1-1 katika mechi yake iliyopita dhidi ya Ruvu Shooting, Simba inayoongoza kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya Azam na Mbeya City matokeo mazuri katika mchezo huo ni muhimu kwao kama ilivyo kwa wapinzani wao Tanzania Prisons.
    Viingilio katika mechi hiyo vitakuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 ambapo tiketi zitauzwa uwanjani kwenye magari maalumu kuanzia saa 4 kamili asubuhi.
    Mabingwa watetezi Yanga wao watakuwa mjini Bukoba kwenye Uwanja wa Kaitaba kuwakabili wenyeji Kagera Sugar wanaofundishwa na Mganda Jackson Mayanja akisaidiwa na Mrage Kabage.
    Kagera ambayo inapishana na Yanga kwa tofauti ya pointi moja ilipoteza mechi iliyopita dhidi ya JKT Ruvu baada ya kulala kwa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex. Wakati Yanga ikiwa katika nafasi ya nne kwa pointi 12, Kagera Sugar ni ya sita kwa pointi kumi na moja.
    Simba SC na Prisons kesho

    Iwapo Kocha Ernst Brandts atawaongoza vijana wake wa Yanga kuibuka na ushindi katika mechi hiyo na Simba kufanya vibaya kwenye mechi dhidi ya Tanzania Prisons huenda akakamata uongozi wa ligi hiyo inayoshirikisha timu 14.
    Mwamuzi Zakaria Jacob wa Pwani ndiye atakayechezesha mechi kati ya Ashanti United na Coastal Union itakayopigwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamazi, Dar es Salaam.
    Raundi ya tisa ya ligi hiyo inaanza keshokutwa Jumapili (Oktoba 13 mwaka huu) kwa mechi kati ya Ruvu Shooting na Rhino Rangers (Mabatini, Mlandizi), Mgambo Shooting na Mbeya City (Mkwakwani, Tanga), Azam na JKT Ruvu (Azam Complex, Dar es Salaam) na Mtibwa Sugar na Oljoro JKT (Manungu, Turiani).
    Mechi zitakazooneshwa moja kwa moja (live) na Azam TV kupitia TBC1 wikiendi hii ni kati ya Simba na Tanzania Prisons itakayochezwa Jumamosi katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na ile kati ya Azam na JKT Ruvu itakayofanyika Jumapili kwenye Uwanja wa Azam Complex.
    Nayo Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kwa makundi yote matatu inaendelea wikiendi hii ambapo kundi B litakuwa na mechi moja tu kati ya Lipuli na Mlale JKT itakayochezwa kesho (Oktoba 12 mwaka huu) katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa.
    Kikosi cha Prisons

    Transit Camp itakwaruzana na Tessema katika Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi wakati Polisi Dar itaumana na African Lyon kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam katika mechi za kundi A zitakazochezwa kesho (Oktoba 12 mwaka huu).
    Mechi nyingine ya kundi hilo itachezwa keshokutwa (Oktoba 13 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kwa kuzikutanisha Friends Rangers na Villa Squad.
    Timu zote nane za kundi C zinashuka viwanjani kesho (Oktoba 12 mwaka huu) kusaka pointi tatu. Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Polisi Dodoma na JKT Kanembwa ya Kigoma.
    Pamba na Mwadui zitacheza katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Polisi Tabora itaikaribisha Toto Africans kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora wakati uga wa Kumbukumbu ya Karume mjini Musoma utatumika kwa mechi kati ya Polisi Mara na Stand United ya Shinyanga
    Wakati huo huo; Maombi ya vitambulisho kwa waandishi wa habari (Accreditation) wanaotaka kuripoti Fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika mwakani nchini Brazil kwa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) yataanza kupokelewa kwa mtandao Desemba 7 mwaka huu kupitia akaunti ya FIFA Media Channel.
    Mwisho wa kupokea maombi hayo itakuwa Januari 31 mwakani, hivyo kwa waandishi wanaotaka kupata vitambulisho hivyo ni lazima wawe na akaunti ya FIFA Media Channel pamoja na utambulisho wa mtumiaji wa akaunti hiyo (user ID).
    Kwa mujibu wa FIFA, kila nchi itapewa idadi maalumu ya nafasi kwa waandishi (waandishi wa kawaida pamoja na wapiga picha) baada ya mechi za mchujo za Kombe la Dunia kumalizika ambapo vigezo mbalimbali vitazingatiwa ikiwemo nchi kufuzu kwa fainali hizo.
    Hivyo, nchi ambayo itakuwa imefuzu itakuwa na nafasi zaidi kulinganisha na zile ambazo hazitakuwa na timu katika fainali hizo za Brazil.
    Mgawanyo wa nafasi zitakazotolewa kwa Tanzania utapangwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA) kulingana na maombi yatakayokuwa yamewasilishwa FIFA kupitia FIFA Media Channel.
    TFF inatoa mwito kwa waandishi wa habari za mpira wa miguu ambao hawana akaunti FIFA Media Channel kuhakikisha wanakuwa nayo mapema ili waweze kutuma maombi yao.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: SIMBA SHUGHULI PEVU KWA PRISONS, YANGA SC NA KAGERA PATACHIMBIKA KAITABA KESHO LIGI KUIU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top