// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); NINI MBEYA CITY, JKT OLJORO ILIONGOZA LIGI KUU, LEO IKO WAPI? - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE NINI MBEYA CITY, JKT OLJORO ILIONGOZA LIGI KUU, LEO IKO WAPI? - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Wednesday, October 16, 2013

    NINI MBEYA CITY, JKT OLJORO ILIONGOZA LIGI KUU, LEO IKO WAPI?

    MSIMU wa 2011/2012 Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ilipokea timu mpya kabisa kutoka Arusha, JKT Oljoro ambayo ilipanda kwa kishindo na kuonyesha ni timu hatari kweli.
    Oljoro ilimaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ikiwa kileleni mwa ligi hiyo na watu wakaamini kwamba timu hiyo itaendelea kuwa tishio. Ilikuwa inashinda mechi nyumbani na ugenini na katika mzunguko wa kwanza ilifungwa mechi moja tu, tena ya kwanza nyumbani na Simba SC, baada ya hapo haikukamatika.
    Watu waliitabiria makubwa Oljoro- kwa wapenzi wa muda wa mrefu wa soka ya nchi hii waliitabiria kurudia maajabu ya Tukuyu Stars ya Mbeya ambayo ilipanda Ligi Kuu mwaka 1986 na moja kwa moja kuchukua ubingwa.

    Lakini katika mzunguko wa pili, Oljoro ilipoteza makali yake na mwisho wa msimu ikamaliza katika nafasi ya sita kwa pointi 35, wakati Simba SC iliyoibuka bingwa ilimaliza na pointi 62, washindi wa pili, Azam FC pointi 56, wa tatu, Yanga SC 49, wanne Mtibwa Sugar 42 na wa tano Coastal Union 39.
    Msimu uliofuata, Oljoro ilishuka hadi nafasi ya nane na msimu huu timu hiyo ya Jeshi la Kujenga Taifa ni moja kati ya vibonde wa Ligi Kuu pamoja na Ashanti United ya Dar es Salaam na wengi wanaitabiria kwamba huu ndiyo msimu wao wa mwisho katika ligi hiyo.
    Wapi walikosea JKT Oljoro, ama walilewa sifa na kupoteza malengo, dira na mwelekeo, au walibahatisha tu cheche walizoingia nazo? Vigumu kujua, lakini ukweli ndiyo wanaelekea kubaki historia Ligi Kuu.
    Msimu huu unaoendelea, ukiwa unakimbilia mwishoni mwa mzunguko wa kwanza, Ligi Kuu pia imepokea mgeni mwingine ambaye ameonyesha ni tishio, Mbeya City, timu inayomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya.
    Hadi sasa timu hiyo ipo katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi yenye ushindani zaidi, kwa pointi zake 17 sawa na Azam walio nafasi ya pili kwa wastani wa mabao- wote wakiwa wanazidiwa pointi moja na Simba SC walio kileleni kwa pointi zao 18.
    Kama ilivyokuwa kwa Oljoro, Mbeya City nayo kwa sasa inasifiwa sana na inatabiriwa mengi na kwa kuwa ni timu ya Mbeya, basi wanaihusisha sana na mafanikio ya Tukuyu Stars.
    Kupata timu ya ushindani katika Ligi Kuu baada ya Simba, Yanga na Azam ni jambo ambalo wengi wetu tunalilia, kwa imani kwamba ushindani zaidi ndiyo uimara wa ligi yetu.
    Coastal Union wanajua matatizo yao, wafadhili wamekuwa wakiwekeza fedha nyingi kwa usajili na maandalizi, lakini mambo hayawi kama inavyotarajiwa.
    Mtibwa Sugar na Kagera ni timu ambazo zinacheza ligi ili zisishuke na zaidi kukamia mechi dhidi ya Simba na Yanga- hazina malengo ya ubingwa na kwa sababu hiyo zinapoteza sifa ya kuwa timu za ushindani, japokuwa zinamilikiwa na makampuni makubwa ya kibiashara.
    Hizo JKT Ruvu na Ruvu Shooting nazo zinacheza ligi ili zisishuke tu, basi. Hazina malengo zaidi. Azam imeonyesha dhamira kweli ya kushindana na Simba na Yanga na imeonekana.
    Katika misimu miwili mfululizo, timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa imeweza kushika nafasi ya pili katika ligi hiyo, hivyo kujipatia tiketi ya kucheza Kombe la Shirikisho Afrika. Msimu wa kwanza ilikuwa nyuma ya Simba SC na msimu wa pili ikawa nyuma ya Yanga SC.
    Dhamira ya Azam inaonekana kuanzia katika uwekezaji na maandalizi- na hata inapotokea ikayumba kidogo, wahusika hushituka na kufanyia kazi mapungufu haraka sana- wazi timu hiyo ni faraja kubwa katika soka ya Tanzania, vinginevyo tungeendelea na ukiritimba wa Simba na Yanga.
    Bado nawatazama kwa jicho la tatu Mbeya City- wanakwenda vizuri wakishinda mechi nyumbani na ugenini na hadi sasa hawajafungwa mechi hata moja. Nafurahishwa na maneno ya kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi yenye kuashiria hawawezi kulewa sifa.
    Nafurahishwa na namna ambavyo Halmashauri ya Jiji la Mbeya inavyoihudumia timu hiyo vizuri, muda wote wa mashindano inakuwa kambini katika hosteli ya chuo cha Mzumbe pale Mbeya na ninaamini wanatembea kwa tahadhari kubwa wasije wakajikwaa.
    Lakini pamoja na yote, bado ni mapema sana kusema chochote kuhusu Mbeya City, angalau tuwasubiri hadi baada ya mzunguko wa pili, maana JKT Oljoro ilikuja na moto mkali kuliko wao, lakini leo iko wapi? Eid Mubarak.              
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: NINI MBEYA CITY, JKT OLJORO ILIONGOZA LIGI KUU, LEO IKO WAPI? Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top