// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); KWA UMAGUMASHI HUU TUSITARAJIE KUFIKA POPOTE ZAIDI YA KUZIDI KUICHIMBIA KABURI SOKA YETU - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE KWA UMAGUMASHI HUU TUSITARAJIE KUFIKA POPOTE ZAIDI YA KUZIDI KUICHIMBIA KABURI SOKA YETU - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Sunday, October 13, 2013

    KWA UMAGUMASHI HUU TUSITARAJIE KUFIKA POPOTE ZAIDI YA KUZIDI KUICHIMBIA KABURI SOKA YETU

    NDANI ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kuna ligi mbili, ya timu za wakubwa na timu za vijana. Hii ipo ndani ya kanuni na kila timu ya Ligi Kuu inapaswa kuwa na timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20 bila hivyo haikidhi vigezo vya kushiriki ligi hiyo.
    Na hata wakati wa usajili timu huwasilisha majina ya vikosi vya kwanza ya wachezaji waliowasajili na pia wachezaji wa timu zao za pili. Hata msimu huu pia, kila timu ya Ligi Kuu ina timu ya vijana. Timu zote 14 katika ligi hiyo zimekidhi sifa na vigezo vya kushiriki ligi hiyo.
    Kwa mujibu wa kanuni na taratibu za TFF juu ya mfumo wa ligi, kabla ya kuchezwa mechi za wakubwa, hutangulia mechi za vijana.

    Na hii ni kwa lengo zuri tu, kuandaa wachezaji wa baadaye wa klabu na timu za taifa na kwa ujumla kuandaa nyota wa baadaye. Kimsingi timu zinapaswa kuwa na timu za vijana kwanza kwa manufaa ya klabu zenyewe, lakini pia kwa manufaa ya soka ya Tanzania kwa ujumla.
    Pamoja na hayo, kumekuwa na dosari nyingi katika ligi ya vijana na hakuna dalili za Bodi ya Ligi wala TFF kushughulikia mapungufu yanayojitokeza.   
    Kikubwa ligi hiyo ya vijana haina sifa za kuitwa ligi , kwa sababu haieleweki na timu hazichezi mechi kikamilifu. Ni timu za Dar es Salaam tu ndizo ambazo humenyana zenyewe kwa zenyewe kikamilifu na wakati mwingine, baadhi ya timu huwa hazipeleki vikosi vyao vya vijana uwanjani.
    Kwa mfano Yanga akicheza na Simba SC, mechi yao itatanguliwa na timu za vijana- lakini Mtibwa Sugar akicheza na Coastal Union hakuna mechi za vijana baina ya timu hizo, sana mwenyeji atacheza na timu nyingine ya mkoani hapo, ambayo si ya ligi.
    Kwa kifupi ni kwamba klabu hazisafirishi wachezaji wao wa timu za vijana katika mechi za mikoani, sasa jiulize hiyo ni ligi gani?
    Bila shaka tunafanya mzaha na pamoja na ukweli kwamba faida za kuwa na ligi madhubuti ya timu za vijana tunazijua- na kwa staili hii tunazidi kuiwekea mazingira magumu soka yetu.
    Tuna mashindano mengi ya kuibua vipaji nchini, kuanzia ya shule za msingi, sekondari, Copa Coca Cola, Airtel Rising Stars, Rollingston, Uhai Cup na mengine, lakini tunakosa msingi wa kuwaendeleza vijana na ndiyo maana wengi hupotea baada ya kuibuka vizuri.
    Tangu mwaka 2005 hadi leo ni wachezaji wengi wameibuliwa kutokana na mashindano hayo na vipaji vyao hakika viliduwaza wengi hata wakatabiriwa kufika mbali, lakini leo ni wachache tu waliopo katika mfumo wa soka yetu. Wengine sijui wanauza, nyanya, vibaka au wanaimba bongo fleva- lakini tumepoteza. 
    Na kwa sababu ya kupuuza uwekezaji wa msingi katika soka ya vijana, ndiyo maana hivi sasa hatuna timu nzuri za vijana, na kwa kuwa hatuna timu nzuri za vijana kwa sasa, basi tusitarajie hata siku moja kuwa na timu nzuri ya wakubwa ya taifa. Tutaishia kuwa wa kubahatisha hivi hivi.
    Lakini pia hata ligi yetu, wachezaji wazuri wataendelea kuwa wale wanaonunuliwa kutoka nchi za nje kama ilivyo sasa akina Didier Kavumbangu, Amisi Tambwe wa Burundi, Kipre Balou na Kipre Tchetche wa Ivory Coast na Haruna Niyonzima wa Rwanda.
    Tutaendelea kuwatukana na kuwashutumu wachezaji wetu bila sababu za msingi, wakati tatizo lipo katika mfumo wetu. Azam iliwasajili akina Kipre baada ya kuvutiwa nao ilipowaona na timu yao ya taifa ya vijana iliyokuja kushiriki Kombe la Challenge mwaka 2010.
    Lakini hao akina Kipre hata wenyewe hawana ndoto za kuchezea timu yoyote ya taifa ya nchini mwao wakiwa Tanzania- kwa sababu kuna wachezaji wengi bora kule. Ila kwa hapa Tanzania ndiyo mastaa wetu na wanaongoza kulipwa fedha nyingi, Milioni 4 kila mmoja kwa mwezi.
    Kama wachezaji wa timu 14 za vijana watacheza kikamilifu ligi ya vijana nyumbani na ugenini, amini mwisho wa msimu klabu zitanufaika na timu ya za taifa pia. Kimsingi, tunahitaji ligi japokuwa mbili za vijana, mbali na hii ya U20, iwepo na ya U17 pia, lakini kwa kuwa mambo ambayo hayaingizi fedha kwa viongozi wa soka yetu huwa hayafikiriwi kabisa.
    Uwekezaji una maana pana- iwapo utawekeza katika ligi hizo za vijana, matunda yake ni kuwa ni ligi bora zaidi ya wakubwa baadaye ambayo itakuwa na mvuto zaidi. Inaweza kuvutia wawekezaji zaidi na hata kuvutia watu zaidi kuingia viwanjani.
    Waswahili wanasema usione vinaelea, vimeundwa nami naongezea,  vitu vizuri vinagharamiwa. Kama tunataka kuwa na timu nzuri za taifa kuanzia za vijana, ligi nzuri ya wakubwa lazima tuwekeze. Lazima tuwe na ligi ya vijana yenye kumaanisha. Mwisho wa msimu tunamjua bingwa, mshindi wa pili, mfungaji bora, kipa bora na timu bora na si huu umagumashi tunaoenda nao hivi sasa. Jumapili njema.  
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    0 comments:

    Item Reviewed: KWA UMAGUMASHI HUU TUSITARAJIE KUFIKA POPOTE ZAIDI YA KUZIDI KUICHIMBIA KABURI SOKA YETU Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top