// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); BILA YA WATU KUWAJIBIBIKA TFF, SOKA YA NCHI HII ITAZIDI KUDIDIMIA - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE BILA YA WATU KUWAJIBIBIKA TFF, SOKA YA NCHI HII ITAZIDI KUDIDIMIA - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Wednesday, October 02, 2013

    BILA YA WATU KUWAJIBIBIKA TFF, SOKA YA NCHI HII ITAZIDI KUDIDIMIA

    IMEWEKWA OKTOBA 2, 2013 SAA 12:08 ASUBUHI
    MARA ya mwisho katika safu hii nilizungumzia uwekezaji haba katika soka ya vijana na wanawake kwa ujumla, kwa kisingizio sugu cha TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) kwamba hawana fedha.
    Nilisema pamoja na madai hayo ya TFF, lakini inafahamika kuna ruzuku ya kila mwaka ya dola 250,000 kutoka FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa) ambayo sehemu ya fedha hizo inatakiwa itumike kwa ajili ya maendeleo ya soka ya wanawake na vijana.

    Fedha hizo kutoka FIFA maarufu kama FAP kwa mwaka huu zimeletwa dola 35,000 kwa ajili ya maendeleo ya vijana, dola 10,000 wanaume, dola 37,000 Wanawake, Ufundi dola 27,0500, Marefa dola 20,000, Tiba dola 15,000, Futsal na soka ya ufukweni dola 5,000, Utawala na Mipango dola 67,000, Miundombinu dola 15,000 na dola 18,000 kwa ajili ya mambo mengine. 
    Ikumbukwe mwaka 2011, TFF ilipokea dola 300,000 zaidi ikiwa ni pamoja na bonasi ya Fainali za Kombe la Dunia zilizofanyika Afrika Kusini mwaka 2010 na kufanya jumla ya dola 550,000 wakati mwaka 2010, TFF ilipata dola 250,000 zaidi za Kombe la Dunia na kufanya jumla ya dola 500, 000.
    Bado kuna mipira inayoingia TFF kila mwaka kutoka Adidas na tangu mwaka 2003 hadi 2010 ilipokea mipira 1000 ya ukubwa wa saizi tano, ingawa kwa ajili ya vijana wanatakiwa kuomba mipira ya saizi nne. Tangu 2011 hadi 2014 tayari mipira 500 imekwishaingia pale Karume.
    Bado kila mechi inayochezwa nchini, TFF ina mgawo wake, tena mzuri- je ni kiasi gani cha fedha ambacho kinakwenda katika mfuko wa kuendeleza vijana na wanawake? Katika moja ya makato maarufu kwenye mechi za mashindanio mbalimbali nchini, kuna fungu la Jichangie, wenyewe wanasema linakwenda kwenye mfuko wa maendeleo, ni mfuko upi na fedha zake zinakwenda wapi?
    Kilichonisukuma kuandika juu ya hayo ni matokeo mazuri ya timu ya wasichana ya Tanzania kutwaa ubingwa wa michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ya kimataifa ya Airtel Rising Stars mjini Lagos, Nigeria, baada ya kuwafunga majirani Kenya bao 1-0 katika Fainali, bao pekee la Donisia Daniel. 
    Safari ya ubingwa kwa mabinti wa Tanzania ilianzia katika mechi za kundi lao, wakishinda moja dhidi ya Sierra-Leone 2-1, wakafungwa moja dhidi ya Uganda na kutoka sare ya 1-1 na Malawi.
    Katika Robo Fainali, mabinti wa kibongo wakashinda 4-2 kwa mikwaju ya penalti dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) Uwanja wa Taasisi ya Michezo, kabla ya kuifumua Uganda kwa mabao 8-1 kwenye Nusu Fainali.
    Mbali na ushindi huo wa wasichana, Tanzania pia imejishindia tuzo mbalimbali ikiwemo, kutoa Mchezaji bora kwa upande wa wasichana ambaye ni Tatu Iddi, Mfungaji bora wa mashindano kwa upande wa wavulana, ambaye ni Athanas Mdam na Mfungaji bora kwa upande wa wasichana, ambaye Shelida Boniface.
    Kwa upande wa wavulana, Niger ilifanikiwa kutetea tena ubingwa baada ya kuifunga Zambia kwa mikwaju ya penalti 7-6 katika fainali ya Airtel Rising Stars kwenye Uwanja wa Agege nchini Nigeria. Wavulana ya Tanzania walishika nafasi ya nne kati ya timu zaidi ya 16 zilizoshiriki michuano hiyo iliyofanyika kwenye viwanja vinne, Agege, Township, Legacy Pitch, Taasisi ya Michezo ya Taifa na Main Bowl.
    Dalili zimeendelea kujitokeza kwamba Tanzania inaweza kufanya vizuri kupitia soka ya wanawake, lakini bado TFF haijaamua kuwekeza huko kiasi cha kutosha. Kwa ujumla Tanzania tunachojua kwenye soka ni Simba na Yanga tu na akili zetu kwa kiasi kikubwa zimeegemea huko huko tu, kiasi kwamba tunashindwa kushiriki kikamilifu mchezo huu kwa maana yake halisi ya sasa.
    Baada ya timu yetu ya taifa ya wanaume, Taifa Stars inayoundwa na wachezaji kutoka timu tunazozipenda Simba na Yanga kuendeleza desturi ya kuboronga na kukosa tiketi za AFCON na Kombe la Dunia, sasa ni zamu ya timu ya wanawake, maarufu kama Twiga Stars.  
    Twiga Stars imepangiwa kucheza na Zambia katika mechi za kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) zitakazofanyika mwakani nchini Namibia.
    Twiga Stars itaanzia ugenini jijini Lusaka ambapo mechi ya kwanza itachezwa kati ya Februari 13 na 15 mwakani wakati ile ya marudiano itafanyika kati ya Februari 28 na Machi 2 mwakani jijini Dar es Salaam.
    Iwapo Twiga Stars itafanikiwa kuitoa Zambia, raundi ya pili ambayo ndiyo ya mwisho itacheza na mshindi kati ya Botswana na Zimbabwe. Mechi ya kwanza itakuwa Dar es Salaam kati ya Mei 23 na 25 mwakani wakati ile ya marudiano itakuwa kati ya Juni 6 na 8 mwakani.
    Nchi 25 zimeingia katika mashindano huku mabingwa watetezi Equatorial Guinea, makamu bingwa Afrika Kusini na Cameroon iliyoshika nafasi ya tatu katika fainali zilizopita zikiingia moja kwa moja katika raundi ya pili.
    Hii Twiga Stars chini ya kocha wake aliyeiwezesha kucheza Fainali za Afrika mara ya kwanza Afrika Kusini mwaka 2009, imekwishawahi kuzifunga Zimbabwe na Zambia na inaweza kufanya hivyo tena na kufanikiwa kukata tiketi ya Fainali za Afrika, lakini hiyo itategemea na maandalizi yatakavyokuwa.
    Kocha wa sasa timu hiyo, Rogasian Kaijage hana hata uhakika wa programu yake, kwa sababu bila shaka anakutana na kauli za ‘fedha hakuna’ kutoka kwa mabwana wakubwa pale TFF. Haya ndiyo mambo ambayo yalimshinda Charles Boniface Mkwasa, akaamua kuitema timu hiyo, maana anajitolea kwa uzalendo wake, lakini waliobeba dhamana ya soka ya nchi hawajali na hawathamini.   
    Ujanja ujanja tu umetawala, wanasubiri kutumia njia za panya- kesho waingilie mlango wa uani pale Ikulu, wamfuate Mama Salma Kikwete kumuomba aisaidie timu, au wamtafute Rahma Al Kharoos ‘Malkia wa Nyuki’- hali hii hadi lini?
    Lazima kuwe na mipango, lazima watu wafanye kazi iliyowapeleka pale TFF na si kuishia kuchat tu facebook kutwa nzima, jioni wanahamia baa wanalewa hadi usiku wa manane, wanaamkia ofisini wamechoka, akili hazifanyi kazi vizuri, wanasubiri kupokea simu za Waandishi wa Habari wawajibu kifedhuli. Hatuwezi kufika kwa staili hiyo. 
    Lazima watu kila kukicha wabangue bongo zao, kufikiria namna ya kuikwamua soka ya Tanzania- na si kwenda ofisini kupoteza muda, wanasubiri usiku wakapige deiwaka za u-MC kuongeza kipato, wanatekelezaje majukumu yako hawa? Wanatakiwa wajiulize na si kufikiria ‘bata tu’ huku soka ya Tanzania inazidi kudidimia.
    Haya sasa, timu ya wanawake, inahijtaji maandalizi ambayo ni fedha na muda upo wa kutosha. Hatutarajii mwisho wa siku timu itawekwa kambini kwenye hosteli ‘mbovu’ ya TFF pale Karume yenye mbu kibao na lishe ya kubabaisha pamoja na maji moja chupa ndogo. Mchezaji anafanya mazoezi magumu, anatakiwa anywe maji mengi. Apate lishe bora, alale vizuri, posho nzuri ya kambini, ili aweze kuweka fikra zake sawa kwa ajili ya mchezo. Tusubiri tuone itakavyokuwa. Siku njema.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: BILA YA WATU KUWAJIBIBIKA TFF, SOKA YA NCHI HII ITAZIDI KUDIDIMIA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top