• HABARI MPYA

        Sunday, September 01, 2013

        SIMBA SC NA MAFUNZO SASA KUPIGWA KESHO JIONI UWANJA WA TAIFA

        Na Prince Akbar, IMEWEKWA SEPTEMBA 1, 2013 SAA 12:22 ASUBUHI
        MCHEZO maalum wa kirafiki baina ya Simba SC na Mafunzo ya Zanzibar uliokuwa ufanyike leo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam sasa umesogezwa mbele hadi kesho saa 11:00 jioni Uwanja huo huo mkubwa na mzuri kuliko vyote nchini.
        Sababu? Mwandaaji wa mechi hiyo, George Michael Wakuganda amesema kwamba wameusogeza mbele mchezo huo ili kuwapa fursa wapenzi wa Simba SC leo kwanza washuhudie mechi ya wapinzani wa jadi England, Manchester United dhidi ya wenyeji Liverpool Uwanja wa Anfield.
        Kesho mtawaona; Kaze kulia na Tambwe kushoto watatambulishwa kesho jioni Uwanja wa Taifa katika mchezo dhidi ya Mafunzo 

        “Kwa kuzingatia hilo, sasa mechi maalum ya Simba SC kuwatambulisha wachezaji wake wapya watatu, Kaze Gilbert, Amisi Tambwe na Henry Joseph utafanyika Jumatatu kuanzia saa 11:00 jioni,”alisema Wakuganda. 
        Baada ya kupatiwa Hati za Uhamisho wa Kimataifa (ITC), wachezaji hao kutoka Burundi, beki Kaze Gilbert na mshambuliaji Tambwe Amisi wataonekana kwa mara ya kwanza wakiichezea Simba SC mjini Dar es Salaam kesho, wakati Henry Joseph anarejea nyumbani  baada ya miaka minne ya kucheza Ulaya.  
        Mwenyekiti huyo wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage alilazimika kwenda Burundi kufuata ITC za wachezaji hao wiki iliyopita baada ya kuona zinachelwa kufika nchini.  
        Hiyo inakuwa mara ya pili kwa Rage, ambaye ana uzoefu wa kuongoza soka kwa zaidi ya miongo mitatu, kuingilia kati suala la uhamisho wa wachezaji wa kimataifa, baada ya miaka miwili iliyopita, kulazimika pia kusafiri kwenda Jamhuri ya Afrika ya Kati kushughulikia uhamisho wa mchezaji Gervais Kago.
        Amerudi; Henry Joseph ataonekana tena kesho akiichezea Simba SC tangu aondoke mwaka 2009 kwenda Ulaya

        Wachezaji wengine wa kigeni wa Simba ni Joseph Owino na Abel Dhaira. Henry aliondoka Simba SC mwaka 2009 kujiunga na Kongsvinger ya Norway na sasa anarejea nyumbani baada ya kumaliza Mkataba wake huko.   
        • Blogger Comments
        • Facebook Comments
        Item Reviewed: SIMBA SC NA MAFUNZO SASA KUPIGWA KESHO JIONI UWANJA WA TAIFA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry