Wanarudi kazini; Wachezaji Taifa Stars wakiwa mazoezini mwezi uliopita. Leo wanaanza tena mazoezi Uwanja wa Karume, Dar es Salaam. |
TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inatarajiwa kuingia kambini leo katika hoteli ya Tansoma, Dar es Salaam kujiandaa na mechi dhidi ya Uganda, The Cranes kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) zitakazofanyika mwakani nchini Afrika Kusini.
Wachezaji walioteuliwa na Kocha Mdenmark, Kim Poulsen katika kikosi hicho ni David Luhende (Yanga SC), Aggrey Morris (Azam), Aishi Manula (Azam), Ally Mustafa (Yanga), Amri Kiemba (Simba), Athuman Idd (Yanga), Frank Domayo (Yanga), Haroun Chanongo (Simba), John Bocco (Azam), Juma Kaseja (Simba), Juma Luizio (Mtibwa Sugar) na Kelvin Yondani (Yanga).
Wengine ni Khamis Mcha (Azam), Mrisho Ngasa (Simba), Mudathiri Yahya (Azam), Mwadini Ali (Azam), Mwinyi Kazimoto (Simba), Nadir Haroub (Yanga), Salum Abubakar (Azam), Shomari Kapombe (Simba), Simon Msuva (Yanga) na Vincent Barnabas (Mtibwa Sugar).
Taifa Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager itacheza na Uganda Julai 13 mwaka huu, saa 9:00 Alasiri kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye mjini Kampala, Uganda.
Kim anatarajiwa kutumia mechi hizo za kufuzu CHAN kuwapoza machungu Watanzania, baada ya kupoteza nafasi ya kwenda katika Fainali za Kombe la Dunia Brazil mwakani, kufuatia kufungwa mabao 4-2 na Ivory Coast katika mchezo wa Kundi C mwezi uliopita Dar es Salaam.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga SC, Clement Sanga jana amewaondoa hofu wapenzi wa soka nchini kuhusu wachezaji wa timu yake walioitwa kwenye kikosi cha Stars.
Kulikuwa kuna habari kwamba, Yanga ambayo itaondoka Julai 5 Dar es Salaam kwenda kanda ya Ziwa kwa ziara ya wiki moja, haitaruhusu wachezaji wake kujiunga na kambi ya Stars, lakini Sanga jana amesema wataripoti timu ya taifa leo.