IMEWEKWA JULAI 3, 2013 SAA 12:33 ASUBUHI
KLABU ya Galatasaray ya Uturuki imefufua mazungumzo na Chelsea na ipo tayari kutoa Pauni Milioni 16 kumnunua kiungo Mnigeria, John Obi Mikel.
Mtaalamu huyo aliungana na The Blues mwaka 2006 - akisajiliwa na Jose Mourinho - baada ya mzozo mkubwa wa usajili uliozihusisha Manchester United na Lyn Oslo ya Norway.
Lakini anaweza kuondoka baada ya miaka sita mara tu baada ya kocha huyo kurejea Chelsea, na klabu hiyo ya Uturuki ipo tayari kumnasa.
Yuko njiani? John Obi Mikel, aliyeichezea Nigeria katika Kombe la Mabara, anaweza kujiunga na Galatasaray akitokea Chelsea
Kifaa: Kiungo Mikel amekuwa Stamford Bridge tangu ajiunge na timu hiyo mwaka 2006 akiwa na umri wa miaka 19 kutoka Lyn Oslo
Dili hilo litafanya Mikel aungane tena Didier Drogba, ambaye amejiunga na Galatasaray msimu uliopita baada ya kuondoka Chelsea kuhamia Shanghai Shenhua ya China.
Mikel amebakiza miaka minne katika Mkataba wake Stamford Bridge, lakini akiwa kwenye Kombe la Mabara na Nigeria alisema mustakabali wake ni tata.
"Nina miaka minne katika mkataba wangu na Chelsea, lakini unafahamu, katika soka huwezi kubashiri, siku moja upo hapa, siku inayofuata unaweza kuondoka,"alisema.
Walipokuwa pamoja: Akihamia Galatasaray, Mikel ataungana na mchezaji mwenzake wa zamani wa Chelsea, Didier Drogba