Sasa Serbia; Okwi kulia enzi zake Simba SC, hapa akiwa na shabiki mkubwa wa timu hiyo, Abdulfatah Salim Saleh, mmiliki wa hoteli maarufu Dar es Salaam, Sapphire Court |
ETOILE du Sahel ya Tunisia ipo katika mpango wa kumuuza Emanuel Okwi katika klabu moja ya Serbia, na fedha itakazolipwa italipa deni inalodaiwa na klabu ya Simba, dola za Kimarekani 300,000 zaidi ya Sh. Milioni 460 za Tanzania.
Etoile ilimnunua mshambuliaji wa kimataifa wa Uganda, Okwi kutoka Simba SC ya Dar es Salaam Januari mwaka huu, lakini imeshindwa kulipa fedha hizo hadi sasa kutokana na kukabiliwa na hali ngumu ya kifedha.
Ilibidi mwezi uliopita Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe aende Tunis kufuatilia malipo hayo na akaahidiwa kulipwa Oktoba mwaka huu.
Lakini sasa, Etoile inaweza kulipa fedha hizo mapema zaidi, iwapo itafanikiwa kumuuza Okwi Serbia kama ilivyopanga.
Hans Poppe ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, Etoile wanaweza kulipa fedha hizo kabla ya Oktoba iwapo watafanikiwa kumuuza Okwi Serbia.
Simba nayo inakabiliwa na hali mbaya kifedha na inahitaji sana fedha ili kuweka mambo yake sawa na mara kadhaa Hans Poppe amekaririwa na vyombo vya habari akiizungumzia hali hiyo na kwamba ndiyo iliyosababisha wakaachana na kocha Mfaransa, Patrick Liewig aliyekuwa analipwa dola 6,000 kwa mwezi na kuajiri mzawa, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’.