// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); JERRY TEGETE AAMSHA HASIRA, ASEMA MSIMU UJAO NYAVU ZITAMKOMA - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE JERRY TEGETE AAMSHA HASIRA, ASEMA MSIMU UJAO NYAVU ZITAMKOMA - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Saturday, July 20, 2013

    JERRY TEGETE AAMSHA HASIRA, ASEMA MSIMU UJAO NYAVU ZITAMKOMA

    Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JULAI 20, 2013 SAA 3:54 ASUBUHI
    MSHAMBULIAJI wa Yanga SC, Jerry John Tegete amesema bado ana uwezo sana na kuumia ndiko kulikopunguza makali yake hivi karibuni.
    Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Tegete alisema kwamba maumivu yaliyomuandama misimu miwili iliyopita yamemfanya ashindwe kucheza kwa kiwango chake siku za karibuni.
    Jerry Tegete: Sijafulia, mtaniona msimu ujao

    Hata hivyo, Tegete amesema amekuwa akipambana siku zote kurudi katika kiwango chake ili awape raha mashabiki wa Yanga.
    “Nadhani msimu ujao utakuwa mzuri kwangu, nimeanza mazoezi vizuri na ninaendelea vizuri. Naamini mambo yatakuwa mazuri tena,”alisema Tegete.
    Tegete ndiye aliyekuwa tegemeo la Yanga hususan linapokuja suala la mechi za watani wa jadi, lakini tangu afunge bao pekee la ushindi Oktoba 16, mwaka 2010 dakika ya 70 mjini Mwanza, mshambuliaji huyo hajaziona tena nyavu za watani.
    Tegete alikuwa anaaminika zinapowadia mechi za watani wa jadi na hadi sasa anajivunia kufunga mabao matano katika mechi za watani, tangu ajiunge na timu hiyo msimu wa 2008/2009 akitokea sekondari ya Makongo na timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20.
    ‘Bismillah’ Tegete anatikisa nyavu za Simba ilikuwa Aprili 19, mwaka 2009 katika mechi ya marudiano ya Ligi Kuu ya Bara, iliyoisha kwa sare ya 2-2 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
    Tegete alifunga bao ambalo liliinusuru Yanga kuzama kwenye mchezo huo kwa 2-1.
    Bao la mwisho; Tegete akishangilia na baba yake baada ya kuwafunga Simba SC mara ya mwisho Oktoba 16, mwaka 2010 Mwanza

    Lilikuwa bao zuri na la utata dakika ya mwisho kabisa, akiunganisha krosi ya Mkenya Michael Barasa kutoka wingi ya kulia, ilionekana kama ameunganisha mpira nyavuni kwa kichwa, lakini kumbe alipiga mpira kwa ngumi, kwa ujanja wa hali ya juu na si refa wala mashabiki waliobaini hadi marudio ya Televisheni baadaye.
    Awali kwenye mchezo huo, kiungo Ramadhan Suleiman Chombo ‘Redondo’ alitangulia kuifungia Simba dakika ya 23, kabla ya Mkenya, Ben Mwalala kusawazisha dakika ya 48 na Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’ kufunga la pili dakika ya 62.
    Tegete akatikisa nyavu za Simba kwa mara ya pili Desemba 25, mwaka 2009 katika Nusu Fainali ya Kombe la Tusker, Yanga ikishinda 2-1 kwenye michuano ambayo pamoja na kuipa timu yake Kombe, ikiifunga Sofapaka ya Kenya 2-1 kwenye fainali, pia aliibuka mfungaji bora.
    Siku hiyo, Tegete aliwatungua Simba dakika ya 67 tu, lakini kiungo Mkenya, Hillary ‘Ford’ Echesa akawasawazishia Wekundu wa Msimbazi dakika ya 78 kwa penalti. Dakika 90 za mchezo ziliisha kwa sare ya 1-1 na mechi ikahamia kwenye dakika 30 za nyongeza- na huko kiungo Shamte Ally Kilalile akaifungia Yanga bao la ushindi, dakika ya mwisho kabisa Uwanja wa Taifa.
    Tegete akawatungua tena mara mbili Aprili 18, mwaka 2010 katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu, Yanga ikilala 4-3, dakika ya 69 na 89. Mabao ya Simba yalifungwa na Uhuru Suleiman Mwambungu dakika ya tatu, Mussa Hassan Mgosi dakika ya 53 na 74 na Hillary Echesa dakika ya 90 na ushei, wakati bao lingine la Yanga, lilifungwa na kiungo Athumani Iddi Athumani ‘Chuji’dakika ya 30. 
    Tegete aliifunga Simba kwa mara ya mwisho Oktoba 16, mwaka 2010, Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza, dakika ya 70, Yanga ikishinda 1-0. Siku hiyo, Yanga ilicheza soka mbovu, lakini nafasi pekee nzuri aliyoipata kwenye mechi iliyochezwa katika viunga alivyokulia vya Kirumba mjini Mwanza, Tegete aliitumia vizuri kwa kukwamisha mpira nyavuni.
    Je, atarudisha makali yake msimu ujao kama alivyopania mwenyewe? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: JERRY TEGETE AAMSHA HASIRA, ASEMA MSIMU UJAO NYAVU ZITAMKOMA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top