IMEWEKWA JULAI 3, 2013 SAA 12:21 ASUBUHI
KWA namna yoyote ile Simba na Yanga ndizo mhimili mkuu ya soka ya Tanzania na ustawi wa timu hizo ni faraja kubwa kwa mchezo huo nchini.
Soka ni mchezo wa watu na kwa kuwa Simba na Yanga ndizo timu zenye wafuasi wengi kwa sasa, basi ndizo zinazoibeba kandanda ya nchi hii.
Ujio wa timu mpya, imara na zenye mipango thabiti na ya kisasa kama Azam FC ni jambo zuri, tena sana, kwani pamoja kuongeza mhimili madhubuti wa soka ya nchi hii, pia zinaleta changamoto kwa klabu zetu kongwe, Simba na Yanga.
Wazi, mafanikio ya Azam FC ndani ya muda mfupi yanazisuta Simba na Yanga ambazo zipo kwa muda mrefu na kuna kila dalili, wanachama na wapenzi wa klabu hizo nao sasa wanatamani kuwa kama timu ya Alhaj Said Salim Bakhresa.
Kwa kuzingatia ukweli huu, kwetu Waandishi wa Habari tuna wajibu wa kutumia vyema kalamu zetu, kuhakikisha tunasaidia maendeleo ya soka ya nchi hii kwa kuhakikisha pamoja na ujio wa Azam, lakini Simba na Yanga nazo zinazinduka.
Tatizo kubwa la timu hizo, pamoja na kwamba kwa sasa zinaongozwa na viongozi wa kisasa, lakini bado zinaendeshwa katika mfumo wa kizamani na ambao ni kama wa kukariri. Hazibadiliki.
Simba na Yanga hazina mipango, dira wala mwelekeo. Zipo kwa ajili ya kucheza Ligi Kuu na kudumisha mila ya upinzani baina yao, basi. Simba ikifikia hatua fulani, Yanga nao watapambana kufikia hatua hiyo, ili mradi tu waende sawa na wapinzani wao.
Inawauma sana Yanga SC, wakati wanazidiwa kwa mafanikio na wapinzani wao kwenye michuano ya Afrika kwa maana ya kufika mbali, lakini pia hata nyumbani, Simba SC ndiyo wanashikilia rekodi ya kuwafunga mabao mengi watani wao hao katika mechi moja.
Kumbuka, Simba SC ilifika Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1974 na kutolewa kwa mbinde, kwa penalti na Mehallal El Kubra ya Misri na mwaka 1993 ikafika Fainali ya Kombe la CAF na kufungwa na Stella Abidjan ya Ivory Coast.
Kwa Yanga, mafanikio yao makubwa katika michuano ya Afrika ni kufika Robo Fainali tu ya Ligi ya Mabingwa mara tatu, 1969, 1970 na 1998 na Kombe la Washindi 1996.
Na katika mechi za watani, Simba iliwafunga watani wao hao 6-0 mwaka 1977 na ikaifunga 5-0 mwaka 2012, wakati ushindi mnono wa Yanga kwa wapinzani wao hao ni 5-0 za 1968.
Kama kuna siku ambayo wana Yanga watafurahi hadi kukufuru ni watakapolipa 6-0, lakini ni vigumu kwa kuwa Simba SC wanaonekana kutaka kuilinda milele rekodi hiyo.
Kwa kweli Simba na Yanga SC ndizo zimeifanya soka ya Tanzania ifike hapa ilipo na kama nchi hii ingebahatika kuwa na viongozi wazuri, basi kwa kutumia uwepo wa klabu hizo, tungeivusha mbali zaidi ya hapa soka ya nchi hii.
Simba na Yanga siku zote mashabiki wake wanazifikiria kuwa bora kama au kuliko hata Real Madrid na ndiyo maana zimechelewa kuchangamkia biashara ya kuandaa na kuuza wachezaji, badala yake zenyewe ndizo zimekuwa wateja wazuri wa kununua wachezaji wa nje.
Simba na Yanga wamecheza hadi Wazungu, tatizo moja tu zimekosa viongozi wa kuziwezesha kuwa imara kiuchumi na kuweza kujitegemea, tofauti na zilivyo sasa zinategemea mapato ya milangoni, misaada ya wafadhili na wadhamini ili kujiendesha.
Simba na Yanga ni klabu tajiri kuliko hata baadhi ya klabu zinazocheza Ligi Kuu ya England kama zingeweza kutumia vizuri rasilimali ya mamailioni ya mashabiki wake.
Naamini, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) ambayo inatangaza bia yake ya Kilimanjaro Premium Lager kwenye jezi za timu hizo inanufaika mno na inajivunia uwekezaji huo kwa maana ya kwamba ni wenye ufanisi.
Mechi mbili tu kwa msimu baina ya mahasimu hao, zinazochezwa mbele ya mashabiki 120,000 (60,000 kila mechi) na kushuhudiwa na mamilioni kupitia Televisheni- pekee zinamlipa mdhamini dau alilowekeza kwa mwaka mzima katika klabu hizo.
Lakini ajabu bado klabu hizi hazijapata viongozi wenye kutambua thamani ya klabu hizo na kufunguka zaidi kimipango katika kuzifanya ziwe na hadhi zaidi na kuweza kujimudu, tofauti na ilivyo sasa zinategemea misaada zaidi.
Nataka kununua kofia ya kiwango kizuri cha ubora au fulana zenye nembo ya timu hizo, nitavipata wapi? Mwingine anataka kununua jezi, kitambaa, kishikia funguo, bendera ndogo ya kuweka kwenye gari lake na hata kubwa ya kufunga nyumbani au kwenye eneo la biashara yake. Atapata wapi?
Wapo wanaotamani pia siku moja kununua hata bidhaa ya kunywa au kula, ambayo itakuwa na nembo ya timu hizo, lakini hawana ndoto za kufanikiwa.
Kama Simba na Yanga wanaamini mafanikio ya haraka ya Azam yametokana na uwezo wa kifedha wa bilionea Alhaj Bakhresa, basi wajue na klabu zao zinapaswa kutengeneza uwezo wa kifedha ndipo zifikirie siku moja kushindana na Tout Puissant Mazembe, lakini si kwa kutegemea misaada ya Zacharia Hans Poppe na Yussuf Mehboob Manji. Jumatano njema.