Mambo ya Coastal; Hoteli ya Raskazone, Tanga ambako Coastal wataweka kambi msimu mzima |
MABINGWA wa mwaka 1988 Ligi Kuu ya Tanzania Bara, Coastal Union ya Tanga wamepania kurejesha taji lao hilo msimu ujao na sasa wanaandaa mazingira ya wachezaji wao kuwa na maisha mazuri ili wafikirie kazi tu.
Pamoja na kuboresha maslahi ya wachezaji wake, kusajili wachezaji bora- Coastal pia imefikiria suala la makazi mazuri ya kudumu kwa nyota wake.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Coastal, Alhaj Nassor Ahmed Mohamed Hussein Bin Slum ameiambia BIN ZUBEIRY kwamba wamekodisha hoteli ya kitalii, Raskazone, Tanga kwa msimu mzima kwa ajili ya kambi ya wachezaji wake.
“Na hii ni kwa muda tu wakati wenyewe tupo kwenye mchakato wa kutafuta eneo letu wenyewe tutengeneze kambi yetu nzuri na ya kisasa,”alisema mmiliki huyo wa maduka ya Bin Slum Tyres.
Coastal inayofundishwa na kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Zanzibar, Hemed Morocco msimu uliopita ilitoa ushindani katika Ligi Kuu, ingawa haikufanikiwa kuwa ndani ya tatu bora.
Na msimu huu inataka kumalizia biashara iliyoianza mwaka jana, baada ya kusajili wachezaji bora kutoka timu mbalimbali nchini, wakiwemo beki Juma Nyosso, kiungo mshambuliaji, Haruna Moshi ‘Boban’ kutoka Simba SC na kiungo Mkenya, Crispin Odula Wadenye kutoka Bandari ya Kenya.
Timu hiyo yenye historia ya kutoa wachezaji bora na wa kihistoria katika soka ya Tanzania kama Mwameja Mohamed, Abdallah Saleh Sabebe, Waziri Mahadhi na wengineo, pia makipa wake wananolewa na kipa hodari wa zamani wa kimataifa nchini, Juma Pondamali ‘Mensah’.
Morocco kulia akiwa na Boban baada ya kukamilisha usajili
Bin Slum amesema Coastal itaingia kambini baadaye mwezi huu kuanza maandalizi ya msimu mpya na itahusisha ziara ya mechi kadhaa za kirafiki ndani na nje ya nchi.
Mwaka jana katika kujiandaa na msimu, Coastal ilifanya ziara Mombasa nchini Kenya na mwaka huu kuna uwezekano ikarejea huko.