Wanaendelea kula bata; Kevin Yondan kulia na Athumani Iddi 'Chuji' hawakutokea mazoezini leo |
YANGA SC imeanza mazoezi leo asubuhi kwenye Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam, lakini kipa mpya, Deo Munishi ‘Dida’, beki Kevin Yondan na viungo Athumani Iddi ‘Chuji’ na Haruna Niyonzima hawakutokea.
Kocha Mholanzi, Ernie Brandts amerejea usiku wa jana kutoka kwao alipokuwa kwa mapumziko na leo ameanza kazi, lakini katika orodha yake wachezaji wa msimu ujao, nane hawakutokea, hivyo akalazimika kufanya mazoezi na wachezaji 17, akiwemo Mrisho Ngassa aliyesajiliwa kutoka kwa mahasimu Simba SC.
Wachezaji ambao hawakutokea mbali ya Dida, Yondan, Chuji na Niyonzima ni beki Rajab Zahir aliyesajiliwa kutoka Mtibwa Sugar na kipa Yussuf Abdul, kiungo Rehani Kibingu na mshambuliaji George Banda waliopandishwa kutoka timu B.
Mbali na Ngassa, aliyerejea Yanga SC baada ya misimu mitatu ya kuzitumikia Azam FC (misimu miwili) na Simba SC msimu mmoja, wengine waliohudhuria mazoezi ya leo ni kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ mabeki, Oscar Joshua, David Luhende, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Abdul, Mbuyu Twite, Salum Telela na Ibrahim Job aliyerejeshwa baada ya kumaliza kuitumikia kwa mkopo African Lyon.
Wengine ni viungo Nizar Khalfan, Abdallah Mguli aliyepandishwa kutoka timu B na Frank Domayo na washambuliaji Simon Msuva, Jerry Tegete, Shaaban Kondo mchezaji huru mpya na Didier Kavumbangu.
Brandts aliyeipa Yanga SC ubingwa wa Bara msimu ulioisha atainoa timu hiyo kwa siku tatu tu kuanzia leo kabla ya kwenda katika ziara ya mechi za kirafiki Kanda ya Ziwa, katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Tabora.
Yanga itacheza na KCC ya Uganda Julai 6 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na Julai 7 itarudiana na timu hiyo ya Kampala mjini Shinyanga kabla ya kuelekea Tabora, ambako Julai 11, itamenyana na Rhino FC iliyopanda Ligi Kuu msimu huu.