KIUNGO mshambuliaji chipukizi wa Simba SC, Haroun Athumani Chanongo amesema anataka kuutumia msimu mpya kukuza kiwango chake, ili baadaye aje kuwa tegemeo la timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Anataka nafasi; Haroun Chanongo anataka kukuza kiwango chake awe mchezaji tegemeo timu ya taifa |
“Ni sawa kwa sasa. Ukitazama kikosi kinachopangwa na ukaona mimi niko benchi, ni sawa. Sawa kabisa. Naheshimu uwezo wa wachezaji wanaopewa nafasi. Lakini nina wajibu sasa wa kukuza kiwango change ili nipate nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Stars,”alisema.
Chanongo amesema kwamba amesikitishwa na Stars kutolewa katika michuano ya kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Ubingwa wa Mataifa wa Afrika (CHAN), zinazohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee, lakini analazimika kukubali matokeo.
“Soka ina matokeo matatu, kushinda, sare au kufungwa. Tumepata moja ya matokeo hayo lakini majukumu yanaendelea. Cha muhimu kwangu ni kukuza kiwango changu niendelee kuwa mchezaji wa timu ya taifa na siku moja niwe mchezaji wa kuanza,”alisema.
Kuhusu Simba SC, Chanongo amesema hatarijii wepesi hata huko kwa kuwa klabu imesajili wachezaji wapya na hata waliokuwapo wanajibidiisha kukuza viwango.
“Simba SC kuna changamoto kubwa. Bila wachezaji wapya, kuna vijana wenzangu tuliopandishwa nao kutoka timu B kama Edward (Christopher), Singano (Ramadhan) ambao wanafanya bidii kukuza viwango,”.
“Na ni wachezaji wazuri ambao wamewahi kuitwa timu ya taifa kabla yangu. Mtu kama Edward ni majeruhi ndiyo yaliyomrudisha nyuma, ila sasa kapona na atarudi juu tu. Unaweza kujionea ushindani wa namba utakaokuwepo pale,”alisema.
Stars ilifungwa 3-1 Jumamosi na wenyeji Uganda, The Cranes, Uwanja wa Mandela, Namboole na kutolewa jumla ya mabao 4-1, baada ya awali kufungwa 1-0 Dar es Salaam wiki mbili zilizopita.
Siku hiyo, Chanongo aliingia uwanjani dakika ya 78 kumpokea John Bocco ‘Adebayor’ wa Azam FC, wakati huo tayari jahazi la Stars limekwishatota na hakuweza kubadilisha matokeo.