Amerejea; Kocha Brandts (katikati) akiwa na Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh (kulia) na BIN ZUBEIRY (kushoto). Mholanzi huyo amerejea jana na leo anaanza kazi Loyola. |
KOCHA Mholanzi, Eernie Brandts amerejea nchini usiku wa jana na asubuhi hii anaelekea Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam kuanza kukinoa kikosi chake kwa ajili ya msimu mpya.
Beki huyo wa kimataifa wa zamani wa Uholanzi, anatarajiwa kukutana na sura mpya mazoezini leo, akiwemo mshambuliaji aliyesajiliwa kutoka kwa mahasimu, Simba SC, Mrisho Ngassa na kipa Deo Munishi ‘Dida’ aliyesajiliwa kutoka Azam FC.
Kijana mpya; Mrisho Ngassa atakuwepo mazoezini Loyola leo |
Ngassa aliyekuwa Mwanza kwa mapumziko, amerejea Jumapili na leo atakuwepo Loyola kuanza rasmi kazi katika klabu aliyojiunga nayo tena majira haya ya joto baada ya kuiacha kwa misimu mitatu akienda Azam FC misimu miwili na msimu wa mwisho Simba SC.
Brandts aliyeipa Yanga SC ubingwa wa Bara msimu ulioisha atainoa timu hiyo kwa siku tatu tu na baada ya hapo itakwenda katika ziara ya mechi za kirafiki Kanda ya Ziwa, katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga na Tabora.
Yanga itacheza na KCC ya Uganda Julai 6 Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza na Julai 7 itarudiana na timu hiyo ya Kampala mjini Shinyanga kabla ya kuelekea Tabora, ambako Julai 11, itamenyana na Rhino FC iliyopanda Ligi Kuu msimu huu.
Mazoezi ya leo yanatarajiwa kuhusisha wachezaji wote wa Yanga, wakiwemo wapya, ukiondoa waliotemwa akina Said Mohamed, Nurdin Bakari, Nsajigwa Shadrack na Godfrey Taita.
Deo Munishi 'Dida' |
Brandts ataendelea kuifundisha Yanga katika Uwanja ambao haridhishwi nao na tayari mara kadhaa ameuambia uongozi juu ya Uwanja bora wa mazoezi, lakini ombi lake halitekelezwi.
Brandts anaamini iwapo atapatiwa Uwanja bora wa mazoezi, basi atafanya kazi nzuri na Yanga itakuwa tishio katika michuano ya ndani na nje pia.