Na Mahmoud Zubeiry, IMEWEKWA JULAI 13, 2013 SAA 7:45 MCHANA
MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera ambaye pia ni kocha wa zamani wa timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars amesema kwamba maadui wakubwa wa soka ya nchi hii ni watatu, ambao ni majungu, fitina na umbeya.
Bendera aliyewahi pia kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo ameyasema hayo asubuhi ya leo wakati akifungua Mkutano Mkuu Maalum wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kwenye ukumbi wa NSSF Water Front, Dar es Salaam.
 |
Maadui watatu; Mh. Bendera akitoa hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa TFF leo. amewataja maadui watatu wa soka ya Tanzania. |
 |
Umakini katika usikivu; Wajumbe wakisikiliza hotuba ya Bendera |
 |
Tabasamu na nukuu; Rais wa TFF, Leidegar Tenga kulia akifurahia hotuba, kushoto Katibu wake, Angetile Osiah akinukuu |
Pamoja na hayo, Bendera amewasihi Wajumbe wa Mkutano Mkuu kuweka kando ubinafsi na kutanguliza mbele maslahi ya soka ya Tanzania katika kujadili mambo kwenye Mkutano huo, unaoendelea hivi sasa Water Front.
“Nataka niwakumbushe kwamba, Watanzania wote, macho na masikio yao yanatutegemea sisi. Hatupo hapa kuonyeshana nani zaidi, ila tupo hapa leo kujenga soka la Tanzania. Ubinafsi leo hii hauna nafasi. Kila mmoja miongoni mwetu aikane nafsi yake. Aseme nipo leo kujenga upya soka ya Tanzania. Ubinafsi hauna nafasi,”alisema.
Bendera alisema soka ni tofauti na michezo mingine mingi duniani kote, ambao unapendwa sana na kwa bahati nzuri unapendwa na rika zote, kuanzia watoto hadi wazee na jinsi zote pia.
Amewataka viongozi wote kuzika tofauti zao na iwe kutoka moyoni na si kinafiki. “Kila mmoja katika nafsi yake aseme ya kale yamepita. Mavi ya kale hayanuki. Tugange yajayo,”alisema Bendera.
 |
Wa Kigoma |
 |
Utamuweza bwana mdogo wewe?; Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kushoto akiwa na Makamu wa kwanza wa Rais wa TFF, Athumani Nyamlani na Makamu wa Pili, Ramadhan Nassib. |
 |
Rais wa TFF, Leodegar Tenga akiwa na James Johonson wa FIFA |
 |
Umemuona na Tenga na yule jamaa wa FIFA? Mwenyekiti wa Chama cha Soka Kagera (KRFA), Jamal Malinzi akinong'ona na Katibu wake, Pelegrinius Alex Rutayuga. |
 |
Kutoka kulia Samuel Nyalla, Dioniz Malinzi, Jamal Malinzi, Deo Lyatto na Rutayuga. |
 |
Kosa moja...; Geoffrey Nyange 'Kaburu' wa Pwani kulia akishauriana mambo na Malinzi katikati na Farid Nahdi wa Morogoro kushoto |
 |
Hawatuwezi wale; Kutoka kushoto Crescentius Magori akiwasikiliza Nyamlani (katikati) na jamaa zake |
Alisema Tanzania ipo katika kipindi cha marekebisho ili iwe na uchumi wa kati na ndiyo maana Watanzania wote hivi sasa wanatakiwa wawe na fikra za kukimbia badala ya kutembea.
“Nchi yetu ina falsafa ya big results now (matokeo makubwa sasa). Nchi yetu inaweka vipaumbele sita, ambavyo ni umeme, Reli na barabara, Kilimo, Elimu, Maji na Fedha.
“Fedha inayohitajika ni shilingi Trilioni 3.9 kwa kipindi cha miaka mitatu tu, sasa kwa kuzingatia hilo, nasi katika soka lazima tuwe na big results now. Ni wakati sasa wa kuinua kiwango chetu cha soka nchini kKote. Hatutapiga hatua kama tutaendeleza maadui hawa watatu. Fitina, Majungu na Umbeya,”alisema.
Katika Mkutano huo, ulioanza saa 4:00 asubuhi kabla ya Wajumbe kupata mapumziko ya nusu saa, saa 5:00 kwa ajili chai, kivutio kikubwa walikuwa wagombea walioomba nafasi ya Urais katika uchaguzi uliosimamishwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Jamal Malinzi na Athumani Nyamlani.
Ni matarajio, Nyamlani ambaye kwa sasa ni Makamu wa kwanza wa Rais wa TFF, ataomba tena nafasi ya Urais kupambana na Malinzi.
FIFA ilisimamisha uchaguzi wa TFF uliokua ufanyike Februari, baada Kamati ya Rufaa kuwaengua wagombea kadhaa akiwemo Malinzi katika mazingira ya mizengwe na kumuacha Nyamlani abaki kuwa mgombea pekee katika nafasi ya Urais.
Malinzi alikata rufaa FIFA na uchaguzi ukasimamishwa hadi suala hilo lilipochunguzwa na kuamriwa uchakato uanze upya. Katikati ya sakata hilo, Serikali nayo ikasimamisha Katiba mpya ya TFF iliyopitishwa mwaka jana kwa njia ya waraka, kwa sababu ni kinyume cha katiba ya mwaka 2006 na kuagiza iitishe Mkutano Mkuu kupitisha Katiba mpya kwa mwongozo wa Katiba iliyopo mezani.
Hata hivyo, baadaye pande hizo mbili, Serikali na TFF ziliketi meza moja na kufikia makubaliano ya kuwaacha kwanza FIFA waje kutatua mgogoro wa uchaguzi ndipo masuala mengine yataendelea.
 |
Bin Zubeiry kulia akiwa na Majjid Mjengwa |
Mkuu wa Idara ya Uanachama wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Primo Corvaro alikuja nchini kufanya uchunguzi wa sakata hilo na kupeleka majibu FIFA, ambao walitoa mwongoza wa kuitishwa Mkutano huu wa sasa.
Katika Mkutano wa leo, FIFA imewakilishwa na James Johnson ambaye ni Mjumbe wa Vyama na Mashirikisho wanachama wa shirikisho hilo.