IMEWEKWA JULAI 24, 2013 SAA 12:27 ASUBUHI
KOCHA wa Manchester United, David Moyes anakabiliwa na baa la majeruhi, baada ya Robin van Persie kuumia wakati wakifungwa mabao 3-2 na Yokohama F-Marinos jana Japan.
Moyes alisema baada ya mechi hiyo kwamba Wayne Rooney aliyeumia nyama za paja anaendelea vizuri na atajiunga na timu mjini Manchester akiwa anatarajia mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 atacheza mechi ya kirafiki Stockholm Agosti 6.
Mwalimu huyo wa United ameendelea kusistiza Rooney hauzwi lakini pia amesema Van Persie amepata maumivu. "Tumepata wiki kadhaa za shaka,"alisema Moyes.
Kuumia kwa Robin van Persie ni pigo Manchester United
"Robin aliumia kipindi cha kwanza na hatukutaka kumpa nafasi zaidi uwanjani. Danny Welbeck pia anahisi maumivu ya nyonga wakati anatembea na tunatakiwa kuhakikisha wote wanakuwa sawa, hususan kutokana na mechi nyingi mbele yetu.
"Bado tuna mechi chache za kucheza kabla ya kuanza kwa msimu tutakaporudi nyumbani. Kama tunavyofahamu, Wayne anakuja. Ameanza mazoezi mepesi ya kukimbia na taarifa nilizopata kutoka watu wetu wa tiba ni kwamba anaendelea vizuri. Ni matumaini mambo yatakuwa kama yanavyotarajiwa.
Danny Welbeck naye ana maumivu
Moyes jana alifungwa mechi ya pili tangu aanze kazi United katika mechi ambazo tayari wamecheza kwenye ziara yao na sasa wanaelekea Osaka leo ambako watacheza mechi nyingine Ijumaa.Klabu hiyo inaendelea kuisaka saini ya Cesc Fabregas kutoka Barcelona, lakini wanakabiliwa na ugumu.
Wapinzani wao kama Manchester City tayari wametumia kiasi kikubwa cha fedha kusajili majira haya ya joto, lakini United wanasema hawana wasiwasi.
David Moyes amekuwa na mwanzo mgumu Manchester United.