Tutakwenda AFCON na CHAN; Yussuf Bakhresa anaamini Stars itatimiza ndoto za muda mrefu |
WAKALA wa wachezaji anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), Alhaj Yussuf Said Salim Bakhresa amesema kwamba, pamoja na timu ya soka ya taifa, Taifa Stars kufungwa mabao 4-2 jana na Ivory Coast, lakini ilicheza vyema na kwa mwenendo huu, kuna matumaini ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka 2015.
Akizungumza na BIN ZUBEIRY jana, Yussuf alisema kwamba timu ilicheza vizuri na kuna wakati hadi Ivory Coast walichanganyikiwa wakati matokeo yalipokuwa 2-2 kabla ya kupata bao la tatu kwa penalti.
Yussuf amesema ni vyema Watanzania wakaendelea kuisapoti timu yao, kwani Ivory Coast ni timu kubwa na nzuri yenye wachezaji wenye uwezo na uzoefu mkubwa kuliko Tanzania.
“Mimi naona kwa sasa hapa Afrika, Ivory Coast ndiyo timu bora. Lakini soka ya jana imeonyesha nasi uwezo wetu uko juu. Tulipata mabao mazuri, pengine kuliko ya kwao yote. Tulifungwa kutokana na makosa ambayo yanarekebishika, nimeridhishwa na kiwango cha timu,”alisema.
Yussuf alisema kwamba ana matumaini pia Taifa Stars itafuzu kwenye Fainali za Wachezaji wanaocheza Ligi za nchini mwao pekee (CHAN), kwani katika kikosi cha jana wataondoka wachezaji wawili tu, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu.
“Tutamkosa Samatta na Ulimwengu, lakini tuna wachezaji wazuri badala yao kama Mrisho Ngassa na John Bocco. Bado wapo chipukizi wengine wanaoinukia vizuri kama Simon Msuva, yule Haruna Chanongo, kwa kweli nina matumaini sana na hii timu,”alisema Yussuf.
Ivory Coast jana ilifanikiwa kusonga hatua ya pili na ya mwisho katika kuwanai tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia, baada ya kuifunga Tanzania mabao 4-2 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa Kundi C kanda ya Afrika.
Mtanange wa jana Taifa |
Kwa ushindi huo, Ivory Coast imetimiza pointi 13 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote katika kundi hilo na sasa itasubiri kucheza na mmoja wa washindi wengine wa makundi mengine tisa ili kuwania kwenda Brazil mwakani.
Tanzania inabaki na pointi zake sita na inaporomoka hadi nafasi ya tatu, huu ukiwa mchezo wa kwanza kufungwa nyumbani katika kampeni hizi na Morocco inapanda hadi nafasi ya pili kwa pointi zake nane baada ya kuifunga Gambia jana inayoendelea kushika mkia kwa pointi yake moja.
Katika mchezo huo uliochezeshwa na refa Mehdi Abid aliyesaidiwa na Hamza Hammou, Bauabdallah Omar wote kutoka Algeria, hadi mapumziko Ivory Coast tayari walikuwa mbele kwa mabao 3-2.
Stars ndiyo waliokuwa wa kwanza kupata bao mfungaji Amri Ramadhani Kiemba dakika ya kwanza tu aliyepokea pasi ya Mbwana Ally Samatta kufuatia mpira wa kurushwa na Erasto Edward Nyoni kusababisha kizazaa langoni mwa Tembo wa Abidjan.
Nyoni alirusha kama amepiga kwa mguu karibu kabisa na kibendera cha kona kufuatia beki Suleiman Bamba kumpitia Thomas Ulimwengu na kutoa nje na mpira ukaokolewa kabla ya kumkuta Samatta aliyempelekea mfungaji.
Ivory Coast wakasawazisha bao hilo dakika ya 15 kupitia kwa Lacina Traore baada ya mabeki wa Stars kuzembea kuokoa na Yaya Toure akafunga la pili kwa mpira wa adhabu dakika ya 23, nje kidogo ya eneo la hatari.
Bao hilo lilitokana na wachezaji wa Stars kupanga ukuta wao vibaya na kumpoteza maboya kipa wao, Juma Kaseja.
Stars ilirudi mchezoni na kufanikiwa kusawazisha bao hilo dakika ya 35 mfungaji Ulimwengu aliyeunganisha krosi maridadi ya Shomary Kapombe.
Hata hivyo, Ivory Coast wakapata penalti rahisi baada ya Gervinho kujiangusha wakati anakabiliana na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ Yaya Toure akaenda kumtungua Kaseja dakika ya 43.
Kipindi cha pili Stars ilikianza vizuri na kushambulia mara nyingi langoni mwa Ivory Coast, lakini wakaishia kukosa mabao ya wazi.
Mabadiliko yaliyofanywa na kocha Mdenmark, Kim Poulsen dakika ya 87 kumtoa kiungo Mwinyi Kazimoto na kumuingiza mshambuliaji Vincent Barnabas yaliigharimu Tanzania kwa kufungwa bao la nne na kupotea kabisa mchezoni.
Baada ya kutoka Kazimoto, aliyetekeleza majukumu yake vizuri leo, Ivory Coast wakatawala sehemu ya kiungo na kutengeneza bao la nne lililofungwa na Bonny Wilfred dakika ya 88.