IMEWEKWA JUNI 25, 2013 SAA 10:30 JIONI
KLABU ya Barcelona imeshauriwa kufikiria kumuuza Messi kufuatia kuwasili kwa Neymar, amesema gwiji wa klabu hiyo Johan Cruyff.
Mwanasoka huyo wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi amewachezea na kuwakochi vigogo hao wa Katalunya na anabakia kuwa mtu muhimu miongoni mwa mashabiki.
Cruyff amesema asingemsajili Neymar kama angekuwa bado ana nguvu katika Bodi ya Ukurugenzi ya klabu, kwani inasababisha mataizo makubwa baina ya washambuliaji hao wawili.
Mafundi: Neymar na Lionel Messi wanatarajiwa kuongoza safu ya ushambuliaji ya Barcelona kufuatia kutua kwa Mbrazil huyo
"Namba moja, nisingemsajili Neymar,"amesema Cruyff akihojiwa na gazeti la Marca. "Neymar akiwa njiani kuja, ningepanga uwezekano wa kumuuza Messi - na baadhi wangekubaliana na hilo, wengine hapana.
"Unazungumzia kuhusu timu, ni wachezaji, na vitu vinavyowazunguka... Kuna mambo mengi hapa. Ndiyo maana ni vigumu kuongoza kikosi cha wachezaji babu kubwa namna hiyo.'
Ametoa hoja zake: Johann Cruyff amesema kuwasili kwa Neymar kutasababisha matatizo katika msimu huu Barcelona
Amesema: "Ni kama mipira ya adhabu. Neymar ni mzuri sana katika kuipiga, na Messi tayari ameonyesha ni mzuri katika hilo. Nani atakwenda kupiga?
"Au kwa ukweli kwamba Neymar na Barcelona wanadhaminiwa na Nike, wakati Leo yupo na Adidas. Hayo mambo ambayo yatasababisha matatizo. Tunalazimika kusubiri ili kujionea- matokeo yake yatakuwa mabaya au mazuri,"alisema. "Ni kujihatarisha".