Onyo kwa Morocco; Samatta kushoto akiwa na Tressor Mputu. Amefunga leo akiichezea Mazembe. |
MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta jioni hii ameifungia bao muhimu la ugenini timu yake, TP Mazembe ikilala 2-1 katika mchezo wa marudiano wa kuwania kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika mjini Maputo, Msumbiji dhidi ya wenyeji Liga Maculmana.
Samatta anayechezea timu hiyo pamoja na Mtanzania mwenzake, Thomas Emmanuel Ulimwengu, alifunga bao hilo dakika ya 45 na kufanya matokeo yawe 1-1 kufuatia wenyeji kutangulia kupata bao kupitia kwa Liberty dakika ya 11.
Hata hivyo, kipindi cha pili baada ya dakika tano tu, wenyeji walipata bao la ushindi, lililofungwa na Pelembe. Juhudi za mabingwa hao wa Afrika mara nne kutoka mji wa Lubumbashi DRC kusawazisha hazikuzaa matunda hadi kipyenga cha mwisho.
Kwa matokeo hayo, Mazembe imejikatia tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho baada ya kushinda 4-0 katika mchezo wa kwanza Lubumbashi.
Mazembe iliangukia katika kapu la kuwania kucheza hatua ya makundi ya Shirikisho, baada ya kutolewa katika Raundi ya Tatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Baada ya mchezo wa leo, Samatta na Ulimwengu wataondokea Afrika Kusini kwenda Marakech kuungana na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kwa ajili ya mchezo wa Kundi C kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia mwakani dhidi ya wenyeji Morocco.
Stars, inayodhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia ya Kilimanjaro, jioni hii inatarajiwa kumenyana na Sudan katika mchezo wa kirafiki mjini Addis Ababa na kesho itaondoka Ethiopia kupitia Cairo, Misri kwenda Morocco.
Samatta alifunga mabao mawili katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Morocco kwenye mchezo wa kwanza mwishoni mwa Machi mwaka huu, bao lingine akifunga Ulimwengu.