IMEWEKWA JUNI 24, 2013 SAA 1:30 ASUBUHI
SAFARI ya kiungo Mkenya Victor Wanyama kuhamia England inazidi kunukia, kufuatia klabu ya Cardiff City kutoa ofa ya Pauni Milioni 10 kwa Celtic kutaka kumnunua kiungo huyo, ambaye anatakiwa pia na Southampton.
Wanyama alisema safari yake kwenda Southampton imekufa, labda klabu hiyo ikubaliane na yeye na wakala wake juu ya mambo fulani fulani.
Southampton ilitoa ofa ya Pauni Milioni 12 iliyokubaliwa na Celtic, lakini Cardiff nayo imetoa ofa yake kwa ajili ya mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 na watampa mshahara atakaoutaka. Timu hiyo ya Malky Mackay sasa ina matumaini ya kuinasa saini ya nyota huyo wa Harambee Stars.
Anayetakiwa: Nyota wa Celtic, Victor Wanyama (katikati) anatakiwa na klabu kadhaa Ligi Kuu England
Akizungumza na mtandao rafiki wa BIN ZUBEIRY, Sportsmail, Wanyama alisema: "Kocha wangu Neil Lennon ameniambia kuhusu ofa ya Southampton, lakini wakati mambo yameenda vizuri kwa Celtic, vipengele havikuwa sahihi kwa upande wangu binafsi na wakala wangu. Nafungua milango ya ofa, lakini niko poa na muhimu Celtic wanafurahi pia.
"Mimi na wakala wangu tumekuwa pamoja na kwa muda mrefu na tupo kama familia. Tuna uhusiano mzuri sana. Amekuwa akinisaidia tangu nikiwa kijana mdogo na tunaaminiana mno baina yetu. Nafahamu atanisaidia mimi kuchukua uamuzi sahihi katika wiki chache zijazo.
Celtic ilimnunua Wanyama kwa Pauni 900,000 kutoka Germinal Beerschot ya Ubelgiji miaka miwili iliyopita na Mkenya huyo amebakiza miaka miwili katika Mkataba wake.