Rais JK anawasili Tanga leo na ziara yake itapambwa na walimbwende wa Miss Tanga ambao shindano lao linafanyika kesho Uwanja wa Mkwakwani |
WASHIRIKI wa shindano la Miss Tanga 2013 wamepata fursa ya pekee ambayo pengine warembo woote watakaoshiriki Miss Tanzania mwaka huu hawataipata.
Vimwana hao ambao watapanda jukwaani kesho kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini hapa katika shindano lao, watakutana ana kwa ana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete leo.
Rais Kikwete anatarajiwa kuwasili mkoani Tanga leo kwa lengo la kuzindua mradi wa kanda maalumu ya uwekezaji katika eneo la viwanda Pongwe wenye ukubwa wa eneo la Hekari 67.7 kwa viwanda na Hekari 4.3 kwa eneo la makazi.
Na katika zoezi hilo, washiriki wa Miss Tanga nao wamealikwa kupamba shughuli hiyo na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Luteni Mstaafu, Chiku Gallawa.
LutenI Chiku, alisema mradi huo wa kanda maalumu ya uwekezaji, ulioanzishwa na Tanga Economic Corridor Limited (Industrial Park Developer), Kampuni inayoundwa kwa ubia baina ya Halmashauri ya Jiji la Tanga yenye hisa asilimia 48 na Good PM group LTD kupitia Africa Future, yenye hisa asilimia 51, ambayo ni taasisi isiyo ya kiserikali inayowezesha uendelezaji wa miundombinu Afrika.
Alisema makubaliano yaliyopo ni Halmashauri ya Jiji la Tanga kuchangia eneo na Good PM Group Limited kuwekeza katika miundombinu na mradi mzima unatarajiwa kugharimu kiasi cha dola za Kimarekeni Milioni 277, kati ya hizo dola Milioni 40 zitatumika kuendeleza miundombinu na dola Milioni 237 zitatumika kwa uwekezaji wa moja kwa moja katika viwanda vyote.
Mafundi mabinti wa Kitanga; Washiriki wa Miss Tanga wakiongozwa na mwalimu wao Asia Yahya kucheza shoo ya ufunguzi mazoezini jana ukumbi wa Lavida Loca |
Mkuu huyo wa Mkoa alisema baada ya mradi huo kukamilika unatarajiwa kutoa fursa za ajira kwa vijana zaidi ya 2,000 katika viwanda 17 vinavyotarajiwa kujengwa mkoani hapa, ili kuweza kuleta maendeleo kwa wakazi wa mkoa na wilaya zake.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa wa Tanga, aliwataka wananchi wote kujitokeza kwa wingi kumlaki mheshimiwa Kikwete katika Uwanja wa ndege Tanga kuanzia saa 4:00 asubuhi na kushiriki katika uzinduzi wa mradi huo utakaofanyika kata ya Pongwe mjini hapa. Shindano la Miss Tanga linafanyika kesho Mkwakwani na litasindikizwa na burudani ya wasamii mbalimbali nyota, akiwemo msanii wa kundi la Tip Top Connetcion la Manzese, Tunda Man.
Mkurugezi wa Kampuni ya DATK Entertainment, waandaaji wa shindano hilo, Asha Kigundula ameiambia BIN ZUBEIRY jana kwamba, amekubali wito wa kuwatoa warembo wake kushiriki zoezi la Mheshimiwa Rais kwa moyo mkunjufu.
Kwa upande wa maandalizi, Asha amesema yanaendelea vizuri na vimwana wapo kambini katika moja ya hoteli za Kitalii hapa Tanga, wakijifua kwenye ukumbi wa Lavida chini ya walimu watatu, Mwanaidi Mbwana, Mariam Bandawe na Asia Yahya.
Aliwataja warembo hao ni Hawa Ramadhan (18), Hazina Mbaga (19), Like Abdulraman (19), Jack Emannuel (18), Wahida Mbwambo(20), Tatu Hussein(19), Mwanahamisi Mashaka(20), Neema Abdallah (18), Winfrida Gutram (21), Lulu Mbonea (19) na Aisha Rashid (21).
Miss Tanga 2013, inadhaminiwa na BIN ZUBEIRY Blog, CXC Africa, Executive Solutions, Busta General Supply, Mkwabi Enterprises, Lusindic Investment LTD, Lavida Pub, Jambo Leo, Staa Spoti, Five Brothers, Cloud's Media Group, Michuzi Media Group, Saluti5, Kajuna, JaneJohn, Kidevu, The Habari na assengaoscar.blogspot.com.
Asha amesema Miss Tanga 2013 ataondoka na zawadi ya Sh. 500,000, wa pili 300,000, wa tatu, 250,000 na wanne na watano, kila mmoja atapata 200,000, wakati watakaobaki kila mmoja atapata kifuta jasho cha Sh. 100,000.