// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); NIYONZIMA HUYU, NA YULE MICHAEL PAUL ‘NYLON’… - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE NIYONZIMA HUYU, NA YULE MICHAEL PAUL ‘NYLON’… - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Sunday, June 02, 2013

    NIYONZIMA HUYU, NA YULE MICHAEL PAUL ‘NYLON’…

    IMEWEKWA JUNI 2, 2013 SAA 12:00 ASUBUHI
    MWAKA 2007, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) liliipokea kanuni mpya ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) kwamba kuanzia msimu wa 2012-2013 klabu za Ligi Kuu ambazo hazitakuwa na Uwanja maalum, sekretarieti na timu za vijana kuanzia chini ya umri wa miaka 14 (U-14) U-17 na U-20 haitaruhusiwa kushiriki michuano ya Afrika.
    FIFA iliagiza mambo kadhaa na TFF ikayaunga mkono, miongoni mwake ni hilo la klabu ambazo hazitakuwa na Uwanja, sekretarieti na timu za U-14, U-14, U-17 na U-20 haitaruhusiwa kushiriki michuano ya Afrika.

    Klabu kubwa nchini, Simba na Yanga zilipingana na TFF na zikalalamika mno. Mwenyekiti wa Simba SC, Ismail Aden Rage, alisema kwamba TFF haijali kuhusu klabu na haizingatii hali halisi ya kiuchumi ya klabu, badala yake imekuwa ikipitisha maamuzi kibabe.   
    “Naishangaa mno TFF kwa kutowasilisha matatizo yetu, hasa ya kifedha huko FIFA na badala yake, kila siku wamekuwa wakitudidimiza tu. TFF wanatakiwa watusaidie ni kwa jinsi gani klabu zitaongeza mapato yake, ambayo yatatusaidia katika kujenga viwanja vya mazoezi na hata kuwa na ofisi kwa klabu ambazo hazina ofisi, ikiwa ni pamoja na kuboresha menejimenti za klabu,” alisema Rage wakati wa semina ya kujadili yaliyofikiwa kwenye azimio la Bagamoyo mwaka 2007, iliyofanyika mwaka juzi Dar es Salaam. 
    Kweli kwa wakati huu tulionao hali halisi ya kiuchumi ya klabu nyingi za Tanzania ni mbaya na hata zile ambazo zinaonekana kuwa njema kifedha, lakini zinajiendesha kwa hasara.
    Azam FC wapo vizuri kiuchumi, lakini ukipiga hesabu za mapato na matumizi yao, unagundua wanajiendesha kwa hasara - pengine wanafanya hivyo kwa matumaini ya mambo kuwa mazuri baadaye.
    Klabu nyingi suala la kulipa tu mishahara ya wachezaji ni tatizo, unapozifikiria kuwa na ofisi na Uwanja, lazima kwanza ufikirie namna ya kuzisaidia kujikomboa kiuchumi kwanza.
    Lakini kama TFF itakuwa inapokea na kupitisha kanuni kwa kuziangalia Azam, Simba na Yanga pekee kama zitamudu hali hiyo au la, hakika tutakuwa tunaichimbia kaburi soka yetu.
    Tukumbuke huko nyuma timu kama Mseto ya Morogoro, Pamba ya Mwanza, African Sports na Coastal Union za Tanga, Reli Morogoro, Majimaji Songea, Tukuyu Stars ya Mbeya, JKT Ruvu, Mtibwa Sugar zimekwishawahi kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya Afrika, tutarajie soka yetu ikiendeshwa kwa misingi ya haki na usawa, hata Ashanti United nayo siku moja itapata nafasi hiyo.
    Kwa hivyo tunaona kuna umuhimu wa kuijengea mazingira mazuri Ligi yetu, kwa kuhakikisha kila timu inajiweza. Unahitajika ushirikiano baina ya TFF na klabu kujadili namna ya kuinua hali ya uchumi ya klabu na si malumbano, kwa sababu upande wa pili wa shilingi, mabadiliko hayaepukiki. 
    Lakini katika Azimio la Bagamoyo, yalijadiliwa mambo mengine ya msingi na yenye manufaa makubwa kwa mustakabali wa soka yetu, kubwa likiwa suala la idadi ya wachezaji wa kigeni. Ilifikia timu inasajili wachezaji 10 wa kigeni na huo ndiyo wakati ambao Tanzania ilipoteza kabisa wachezaji na timu ya taifa ikaporomoka.
    Maana watu walikuwa hawajishughulishi na wachezaji wazawa, wanasajili tu wageni, lakini kupunguzwa kwa idadi hadi wachezaji watano tahfifu imeonekana na hata timu yetu ya taifa sasa ina wachezaji bora, si bora wachezaji.  
    Ilikubaliwa katika Azimio la Bagamoyo lililohusisha na viongozi wa klabu pia, kwamba kuanzia msimu wa 2013/2014 klabu zisisajili zaidi ya wachezaji watatu wa kigeni, lakini wiki hii, Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah Malabeja alisema kwamba watakaa kwanza na Klabu kujadili suala hilo, ili kupata maoni yao.
    “Lazima tukae kwanza na klabu ili tupate maoni yao. Kwa sababu ilikuwa tuanze mapema tu kutumia sheria hiyo, lakini klabu zikaomba katika Azimio la Bagamoyo tuanze msimu wa 2013/2014,”alisema Osiah.
    Nastaajabu kidogo TFF kusema itakaa kwanza na klabu kujadiliana nazo. Nazikumbuka zile makala alizokuwa anaandika kaka yangu Angetile Osiah katika safu yake ya Kurunzi kwenye gazeti la Mwanaspoti. Natamani aendelee kuwa mtu wa mitazamo na misimamo ile ile.
    Hakuna haja ya kujadili upya, ilikwishajadiliwa katika Azimio na ilikuwa sheria hiyo ianze mara moja, lakini klabu zikaomba zipewa muda kwa sababu nyingine zilidai zina mikataba mirefu na wachezaji wao wa kigeni. Sasa muda umefika, tunaanza kujiuma uma ili iweje?
    Tukumbuke sababu ya msingi ya uundwaji wa sheria hii, ni kutoa fursa kwa wachezaji wazawa zaidi katika Ligi ya nchini mwao. Najua hapa tatizo ni Simba na Yanga tu- hakuna kingine, TFF inashindwa kuamua kwa sababu ya hizo timu mbili.
    Lakini lazima tukubali mabadiliko haya ni ya maana sana kwa mustakabali wa soka yetu na ni muhimu mno kuyapokea na kuyatekeleza mara moja. Yanga pale, ilikuwa panga pangua kipa namba moja Mghana Yaw Berko, lakini akaumia katika Robo Fainali ya Kombe la Kagame mwaka jana na kuingia Ally Mustafa ‘Barthez’, aliyedaka mechi zote zilizofuata hadi timu ikatwaa Kombe.
    Barthez ameendelea kudaka msimu wote huu hadi Yanga imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu, naye amerejeshwa timu ya taifa. Je, asingepata nafasi Barthez saa ngapi angeonyesha uwezo wake?
    Katika kikosi cha Taifa Stars hivi sasa kuna mchezaji anaitwa Haroun Chanongo, nani alikuwa anamjua huyu wakati tunaanza msimu uliomalizika?  Pale Simba gumzo alikuwa Salim Kinje, ambaye alisajiliwa kwa mamilioni kutoka Kenya, lakini dogo alipopewa nafasi na makocha waliobaini kipaji chake, hatimaye naye ameingia katika orodha ya nyota wa Ligi Kuu.
    Zamani viongozi wetu, walikuwa wakiona mchezaji mzuri nje, walikuwa wakijitahidi kusaka mchezaji mzuri zaidi hapa nyumbani na ndiyo maana walitokea wataalamu wengi wakati huo. Haruna Niyonzima ni mchezaji mzuri, lakini nikikumbuka vitu vya Nico Njohole au Charles Boniface Mkwasa enzi zao, nasikitika tu. 
    Mbali sana huko, kuna Msukuma mmoja alitikisa kwa kipindi kifupi tu katika soka ya Tanzania, akapewa jina Nylon, namzungumzia Michael Paul. Anayemkumbuka anitumie ujumbe kuniambia soka ya Niyonzima inayotuchengua hivi sasa, imefikia kiwango cha Michael Paul ‘Nylon’?
    Watapatikana tu wachezaji wazuri kuliko hao wageni, iwapo tutaamua kuwekeza kwa wachezaji wetu kuanzia katika umri mdogo, kwa sababu hata hao tunaowababaikia nao wamejengewa uwezo nchini mwao. Jumapili njema.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments
    Item Reviewed: NIYONZIMA HUYU, NA YULE MICHAEL PAUL ‘NYLON’… Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top